Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatuna Upungufu wa Chanjo, Mzigo Mwingine Upo Njiani - Video

Video Archive
Sat, 16 Oct 2021 Chanzo: globalpublishers.co.tz

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania haina uhaba wa chanjo ya Uviko – 19 kwani chanjo ipo ya kutosha na chanjo nyingine ipo njiani inakuja.

Rais Samia amesema hayo leo wakati akihutubia katika hafla ya Miaka 50 ya Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro iliyoambatana na ibada ya misa ya shukrani ambapo Mhe. Rais Samia alikuwa mgeni Rasmi.

“Nawapongeza kwa kufanya hospitali hii kuwa ya kisasa inayoendana na utoaji wa huduma za afya kwa kutumia vifaa vya kisasa vyenye uwezo mkubwa, hongereni kwa kuboresha huduma katika idara ya mionzi, kununua mashine za MRI, CT Scan na Digital X-Rays.

“Nawapongeza kwa kutoa huduma za vipimo vya uzito, sukari, usikivu, shinikizo la damu, macho pamoja na magonjwa ya ngozi na magonjwa ya zinaa bila malipo. Hospitali hii ya KCMC imekuwa ikitoa tiba, mafunzo na kufanya tafiti bila ubaguzi wa aina yoyote. Hospitali ya KCMC imepewa ya hadhi ya kuwa ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini. 

“Katika kutekeleza ilani ya CCM, tulisema tutajenga jengo la tiba ya saratani kwa mionzi litakalogharimu shilingi bilioni 4, bilioni 1 imeshafika na bilioni nyingine moja iko njiani kuja. Tutahakikisha ujenzi unakamilika haraka ili huduma ianze kutolewa.

“Serikali itaendelea kuhakikisha kufadhili vijana wengi zaidi na kutoa miongozo mbalimbali katika Chuo hiki cha tiba (KCMC) ili kuhakikisha inatoa vijana bora kukidhi soko la ajira.

“Katika azma ya kuwa na Utalii Tiba, kwa sasa wagonjwa watakuwa wanakuja kutibiwa pale Dar es Salaam na wengine watakuwa wanakuja KCMC. Pia niwapongeze KCMC na taasisi nyingine zinazoendelea kufanya tafiti mbalimbali kwa magonjwa yanayowakabili binadamu.

“Muongeze wigo wa kufanya tafiti, kwa kufanya tafiti katika magonjwa mapya na magonjwa ya mlipuko na hatua hii itasaidia serikali katika kujiandaa na kuyakabili magonjwa.

“Kulingana na makubaliano yaliyofikiwa baina ya Serikali na Kanisa, Serikali imeendelea kuyatekeleza ikiwemo kulipa mishahara ya Watumishi wa Hospitali ya KCMC inayogharimu Tsh bilioni 10 takwimu zote amezisema Naibu Waziri wa Afya.

“Niendelee kuwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari zote kujipeusha na athari za ugonjwa wa Uviko-19 ikiwemo kuchanja pamoja na kufuata maelekezo ya wataalamu wetu, kwa kuwa hatujui huu ugonjwa utaisha lini. Hatuna upungufu wa chanjo ya UVIKO-19, juzi tulipokea chanjo awamu ya pili, na mzigo mwingine wa chanjo uko njiani unakuja. Nitoe rai tu kwa wananchi kujitokeza kuchanja.

“Askofu Shoo ni mmoja kati ya watu walioniunga mkono mapema mno, siku ile nazindua chanjo baada ya mimi kuchanjwa waliofuata viongozi wa dini yeye alikuwepo kwahiyo sishangazwi tasisi yake hii imeweza kuchanja, hongera sana Baba Askofu.

“Nitaendelea kuwahudumia Watanzania kwa kadri na jinsi Mwenyezi Mungu atakavyoniwezesha, na pia nitaendelea kuwaangalia Watanzania kwa kwa jicho la huruma kama jicho langu lilivyo kwa kadri na jinsi Mwenyezi Mungu atakavyoniwezesha. Naomba mniombee,” amesmeama Rais Samia.

Chanzo: globalpublishers.co.tz