Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatari tano anazoweza kukutana nazo mwanao mtandaoni

43506 Pic+mtandaoni Hatari tano anazoweza kukutana nazo mwanao mtandaoni

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mara kadhaa kupitia wasaa huu tumezungumza juu ya matumizi ya mtandao na athari zake, chanya na hasi. Leo tunaeleza aina tano kuu za hatari anazoweza kukutana nazo mwanao awapo mitandaoni na namna bora ya kukabiliana nazo ili kupafanya mtandaoni mahali salama kwa mwanao.

Mtandaoni kuna maudhui chungu nzima kuanzia nyimbo za ibada hata filamu za utupu. Ingawa waandaaji wa maudhui wanaweza kuweka maangalizo juu ya umri wa nani anapaswa kuona nini, mtandao haubagui na mara nyingi hasa hapa kwetu watoto wetu wanatumia ama simu zetu, kompyuta na pengine ‘tablets’ zetu wazazi kuingia mtandaoni.

Namna hii wanaweza kuangalia tunayotumiwa na watu wazima wenzetu au ambayo tumeshayafungua wakaendelea ‘kufurahia.’

Kufanya mawasiliano na watu wasiofaa. Mtandaoni wapo marafiki tunaowafahamu vyema na tusiowafahamu hata chembe.

Watu wazima kila uchao tunapokea maombi ya marafiki wapya. Mtoto naye hili halikwepi mtandaoni. Wapo watu wasio waaminifu, kutwa wanatafuta watoto wadogo kuwalaghai ama kupitia picha za ngono. Je, unajua utafiti wa hivi karibuni ulionyesha kuwa mtoto mmoja wa Kitanzania ana marafiki hadi zaidi ya 5,000 kwa wastani katika mitandao ya kijamii?

Watoto, kama sisi watu wazima, wanapenda kuwa maarufu. Umaarufu wa mitandaoni umewafanya wapige picha wakiwa watupu, wakiogelea ama wakipata kumbato, mabusu na mambo kama hayo huku wenzao wakiwachukua filamu ama picha.

Yote haya hupakiwa mitandaoni ili kupata ‘likes’ na maoni (comments). Bahati mbaya mtandao hausahau. Picha na filamu hizi zitadumu hata watakapohitimu elimu na wakawa ‘watafuta ajira’ au viongozi.

Matumizi yaliyopitiliza hadi kuleta athari za utegemezi wa mtandao. Upo usemi unaoibuka kwa sasa kuwa maisha hayawezekani pasi na mtandao. Hii kwa watoto ina maana kuwa wataathirika kimakuzi, masomoni, kiroho na hata kimahusiano. Itakuwa nadra kwao hata kujenga hoja wanapokuwa na marafiki hata kwetu sisi wazazi wao. Marafiki wao takribani wote watakuwa penye ‘screen’ za kompyuta, n.k.

Athari za kibiashara. Upo ushahidi wa mzazi mmoja aliyeikuta picha ya mwanaye aliyoipakia mtandaoni katika mabango ya matangazo barabarani (billboards) akiwa safarini nchi jirani.

Makampuni kwa sasa yamehamishia ‘vita’ ya masoko mtandaoni. Kila unapoingia kuperuzi unaulizwa ulipo (location), umri na mawasiliano yako binafsi.

Yote haya mtoto hawezi kuyakabili. Mara nyingi atagawa taarifa hizi kama njugu na mwishowe atakuwa ‘soko-mjinga’ la bidhaa lukuki hata zenye kuhitaji matumizi ya watu wazima pekee.

Ufanyeje? Badala ya kumnyima mtoto mtandao mpe mafunzo ya matumizi bora ya mtandao.

Wewe ndiye mlinzi nambari moja wa mtoto wako. Mpe nyenzo ili kwazo ajikinge na majahili toka kote duniani mtandaoni.

Anza kwa kujifunza wewe namna bora ya kutumia mtandao kwa miongozo chungu nzima inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano hapa kwetu Tanzania.



Chanzo: mwananchi.co.tz