Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatari kwa wanawake wanaojifukiza sehemu za siri zatajwa

Hatari Pic Data Hatari kwa wanawake wanaojifukiza sehemu za siri zatajwa

Mon, 1 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Kushamiri kwa biashara ya urembo mtandaoni kumeleta bidhaa ambazo nyingine ni hatari kwa afya ya viungo vya uzazi kwa wanawake.

Bidhaa hizo za urembo zimeshamiri kutokana na matangazo yake na hasa madai ya uwezo wa kumtuliza mwenza pale mwanamke atakapoitumia kusafishia sehemu yake ya siri kwa njia ya kujifukiza na maji ya moto yaliyowekwa dawa hizo.

Mbali na kutumiwa kusafisha, pia zinadaiwa na wauzaji wa bidhaa hizo zinasaidia kupunguza ukubwa wa uke, kuondoa ukavu na kukaza misuli ya uke na hivyo kumvutia mwanamume.

Wafanyabiashara wa mtandaoni ndio wameiteka biashara hii inayohusisha mchanganyiko wa majani yanayoitwa ‘yoni steaming herbs’.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wamepinga njia hiyo ya kutumia mvuke wakisema muundo wa uke unaruhusu kujisafisha wenyewe, huku wakitahadharisha njia hiyo ina madhara kwenye viungo vya uzazi vya mwanamke na inaweza kusababisha saratani ya kizazi.

Mwananchi ilimtafuta mfanyabiashara mmoja anayeuza dawa hiyo ambaye alijibu:

Advertisement “Ni majani ya asili hayana madhara, yanasaidia kuondoa uchafu na kuacha uke ukiwa na harufu nzuri, nadhani maelezo yanatosha tuma pesa mtu wa boda akuletee popote ulipo”.

Jinsi inavyotumika

Kulingana na maelekezo ambayo yapo mitandaoni, majani haya huchemshwa na maji ya moto kisha maji hayo kuwekwa kwenye chombo ambacho kitaruhusu mvuke kutoka na mwanamke anachuchumaa au kukaa kwenye chombo hicho katika mtindo ambao umvuke utapita kwenye sehemu yake ya siri.

Wapo ambao mvuke wa maji wanayotumia ni yale yanachanganywa na iliki, karafuu, majani ya mgagani au majani ya asumini ambayo yanasifika kuwa na harufu nzuri.

Kauli ya watumiaji

Mmoja wa watumiaji wa njia hiyo ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake anasema kabla ya kuwa na mchanganyiko maalumu ambao anautumia kwa kuweka kwenye maji alikuwa akitumia maji ya kawaida yenye chumvi.

“Mimi mtu wa kusini, sisi kwetu tunafundishwa usafi na umuhimu wa hivi viungo vya mwanamke, nakumbuka wakati nachezwa niliambiwa naweza kujisafisha kwa mvuke wa maji ya moto uliochanganywa na chumvi.

“Hii ni njia ya asili kabisa na haijawahi kuwa na madhara kwangu wala mtu yeyote kule kwetu.

“Basi ilikuwa utaratibu wangu baada ya muda fulani nachemsha maji naweka chumvi kisha naweke kwenye beseni nachutama, ule mvuke unaingia baada ya dakika 10 hadi 15 natoka. Ila siku hizi kuna unga kabisa niliupata huko kwenye mizunguko yangu ndio nauweka kwenye maji ya moto,” alisema.

Mwananchi lilizungumza na kungwi mmoja anayenadi bidhaa zake mitandaoni na kukiri kufahamu mvuke unatumika kusafisha uke na kubainisha kuwa hafahamu ufanisi wa njia hiyo, ila anajua kuna viungo vya jikoni ambavyo vinatumika katika kunogesha uke na hutumiwa na wanawake.

Kungwi huyo aitwaye Mwanaasha Amir anasema mojawapo ya viungo hivyo ni nyanya ambayo hutumika kuongeza ladha wakati mwanamke anapojamiiana, huku akiitaja iliki kama njia bora ya kusafisha uke.

“Ukitaka kujiweka msafi pamoja na kujisafisha na maji kawaida wakati mwingine unaweza kutumia iliki. Unachofanya ni kuzisafisha iliki na kuziloweka kwenye maji safi kwa siku tatu kisha unayatumia yale maji kutawazia, njia hii inakufanya uke wako uwe safi usitoe harufu wala uchafu wa aina yoyote, kama kulikuwa na shombo yote inaisha”.

Wataalamu wa afya

Wataalamu wa afya, hasa waliobobea katika magonjwa ya wanawake wamepinga njia hiyo ya kusafisha uke kwa mvuke wa maji ya moto wakieleza ina madhara kiafya.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Abdul Mkeyenge alisema amewahi kuona taarifa za wanawake wanaotumia njia ya mvuke wakichanganya na bidhaa zenye manukato au dawa kwa lengo la kuweka harufu nzuri na kusafisha uke.

Hata hivyo, alisema njia hiyo haijawahi kushauriwa kiafya, kwani ina madhara ikiwemo kuua bakteria wenye kazi ya kulinda uke.

Alisema mvuke unasababisha joto kwenye uke na hali ikiwa hivyo ni rahisi kuzalishwa kwa fangasi ambao kwa asili wanapenda joto, hivyo mtu anayetumia njia hiyo si ajabu kusumbuliwa na fangasi za sehemu za siri mara kwa mara.

“Hawa fangasi wakikomaa wanaweza kuingia ndani na kuleta shida zaidi kwenye via vya uzazi, ndio maana nasema hii sio njia nzuri na haishauriwi mtu kufanya hivi, usafi unaweza kufanyika kwa maji ya kawaida siyo kuongeza kitu kingine chochote,” alisema Dk Mkeyenge.

Akizungumzia hilo, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Living Colman alisema uke haupaswi kusafishwa wala kuwekewa kitu kwa lengo la kusafisha kwa kuwa umetengenezwa kwa namna ambayo unajisafisha wenyewe.

“Uke una bakteria ambao kazi yao ni kulinda kiungo hicho, kuingiza kitu chochote ninaposema chochote si sabuni, kidole, manukato wala mafuta yanayopaswa kuingizwa huko. Inapokuja hili suala la mvuke naweza kusema ni hatari zaidi.

“Kuzifusha sehemu za siri kunaweza kuathiri vijidudu hivyo na kusababisha kuwashwa, kuruhusu kushambulia kwa sababu kutakuwa hakuna ulinzi na hili linaweza kusababisha hata kupata saratani ya shingo ya kizazi,” anasema.

Takwimu za saratani

Wakati wataalamu wakieleza hayo, takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha wanawake ndio waathirika wakubwa, huku saratani ya shingo ya kizazi ikiongoza kwa asilimia 36.

Daktari bingwa wa saratani, Lucas Kiheji alisema kitendo cha kufukiza uke kwa maji ya moto si kitu kinachoshauriwa, kwani inaweza kumsababishia mtu michubuko na hata uwezekano wa kupata saratani kulingana na aina ya dawa zilizotumika kuchanganywa kwenye hayo maji ya moto.

“Kitendo cha kuweka kemikali kwenye hayo maji kisha mvuke kuelekezwa ukeni kuna uwezekano wa kupata saratani ‘dyplsia cancer’, ila vipo vitu ambavyo vimethibitishwa kabisa kusababisha saratani ambavyo ni ugoro na tumbaku. Kuna wanawake wanaweka hivi kwenye sehemu zao za siri, ni hatari sana,” alisema Dk Kiheji.

Majeraha ukeni

Dk Mariam Mabula alisema mbali na maradhi, athari nyingine anayoweza kupata mtumiaji wa mvuke ni majeraha kwa kuwa ngozi laini pembezoni mwa sehemu za siri inaweza kuungua au kubabuka.

“Hakuna uwezekano wowote wa kuondoa discharge au harufu mbaya kwa kutumia mvuke, kwanza si rahisi mvuke kuingia ndani ya uke ambako vitu hivyo vinatoka, matokeo yake utaishia juu ambapo utaleta athari kubwa kwenye hilo eneo la juu.

“Unaweza ukaweka dawa au ukafukisha ukaishia kuvimba, kubabuka na kuungua. Ukiungua itakusababishia makovu ambayo yatakufanya uzichukie sehemu zako na hii itakuathiri kisaikolojia. Kingine kwa namna uke ulivyoundwa unapoingiza kitu chochote ndio unatengeneza mazingira ya bakteria kuingia na kushambulia.

Kuhusu matumizi ya mimea ya asili katika mbinu hiyo, mtaalamu huyo anaeleza kuwa uasili huo hauzuii kuleta madhara endapo itatumika katika eneo lisilotakiwa, akitolea mfano uke.

Dk Mariam alisisitiza kuwa masuala yanayohusu viungo vya uzazi yanahitaji wataalamu.

“Ukijihisi una shida yoyote sijui ukavu, harufu mbaya ni vyema kwenda hospitali ukapate ushauri wa kitaalamu na tiba na sio kuweka vitu ukeni, wanawake wanapaswa kufahamu kwamba harufu mbaya ukeni mara nyingi inasababishwa na infections, hivyo ili upone ni lazima utibiwe,” alisema.

Chanzo: Mwananchi