Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hasira, unene, usingizi vyatajwa magonjwa

9a13f91ceb257eb1399c7b5316f58330 Hasira, unene, usingizi vyatajwa magonjwa

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATAALAMU wa afya wametaja mambo kadhaa ikiwamo hasira, kuumwa kichwa sana, kizunguzungu, unene uliokithiri, usingizi usio wa kawaida, msongo wa mawazo na uchovu mwingi kuwa ni viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza.

Aidha, wameshauri ili kudhibiti magonjwa hayo, jamii ibadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi ikiwamo kutembea angalau mwendo wa haraka wa dakika 10 kila siku na watu wenye umri kuanzia miaka 45 kuhakikisha wanapima afya kila mwaka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika semina kwa waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya habari hivi karibuni, wataalamu hao walieleza kuwa watu wengi wana viashiria na dalili za magonjwa yasiyoambukiza lakini hawajui.

Muuguzi wa miaka mingi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambaye sasa amestaafu lakini ni mkufunzi wa magonjwa yasiyoambukiza, Elizabeth Licoco alisema hivi karibuni kuwa, unene uliokithiri, hasira, kuumwa kichwa, kizunguzungu, uchovu ni viashiria vya magonjwa hayo.

“Ukiwa na viashiria hivyo upo katika uwezekano wa kuwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Dalili ni pamoja na kunywa maji sana kutokana na kuwa na kiu na kukojoa sana nyakati za usiku.

“Ushauri wa afya ni kujenga utamaduni wa kupima afya kila baada ya miezi sita kwa wenye umri zaidi ya miaka 45 na wenye umri chini ya hapo angalau kila mwaka,” alishauri Licoco.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani (moyo, ukimwi, ebola, covid-19 na pumu) katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Mhazini wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), Dk Tatizo Waane alisema jinsi mtu alivyo ni matokeo ya uamuzi wake.

“Uchaguzi wetu wa namna ya kuishi, nini tunakula, kwa wakati gani ndio sababu ya jinsi tulivyo. Hatari ni kwamba wenye magonjwa yasiyoambukiza wapo hatarini zaidi kupata magonjwa ya kuambukiza hivyo ni vizuri kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara,” alisema.

Dk Waane alitoa mfano kuwa, ugonjwa wa kisukari ambao si wa kuambukiza husababisha uzito kwa mwili kushuka na tatizo hilo linatoa mwanya wa mhusika kupata ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) ambao ni wa kuambukiza kwa njia ya hewa kutokana na mwili kuwa dhaifu.

Meneja wa Programu za Magonjwa Yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Omar Ubuguyu alisema ukuaji wa teknolojia unasababisha wanadamu kutoshughulisha miili yao jambo linalochangia kupata magonjwa hayo.

Alisema hivi sasa hasa mijini watu hawatembei bali hutumia daladala, bodaboda au magari binafsi na kushauri washughulishe miili kwa kutembea kwa mwendo wa haraka angalau kwa wastani wa chini wa dakika 10 kwa siku au dakika 150 kwa wiki.

Magonjwa yasio ya kuambukiza ni pamoja na maradhi ya moyo, kisukari, shinikizo la damu, kifafa cha mimba, kiharusi, saratani, magonjwa ya meno, upofu na upeo mdogo wa kuona, ajali na selimundu.

Chanzo: habarileo.co.tz