Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Halmashauri yanunua boti kusafirisha wagonjwa visiwani

14183 Pic+boti TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Muleba. Halmahauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera imenunua boti tatu maalum kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa wanaohitaji huduma ya dharura na rufaa kutoka kwenye zahanati zake tano zilizoko maeneo ya visiwani.

Akizingumza na waandishi wa habari leo Agosti 27, 2018 kuhusu upatikanaji wa dawa, vifaatiba na vitendanishi vya maabara kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dk Modest Burchard amesema boti hizo zitatoa huduma ya kusafirisha wagonjwa kutoka zahanati tano za halmashauri hiyo zilizoko kwenye visiwa vya Ziwa Victoria.

“Kupatikana kwa boti hizi kutasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji rufaa na huduma za dharura kutoka zahanati za visiwani, hasa wanawake wajawazito na watoto,” amesema Dk Burchard.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, mganga mkuu huyo amesema halmashauri yake inapokea dawa muhimu kwa wastani wa asilimia kati ya 90 hadi 98.

“Dawa zote muhimu zinapatikana kuanzia kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali. Hakuna mgonjwa anayefika eneo la huduma akakosa dawa, labda kama dawa husika haipatikani eneo la huduma kulingana na hadhi na aina ya dawa,” amesema.

Hata hivyo, amesema zipo dawa ambazo bado hazipatikani kulingana na ngazi ya eneo la huduma na kufafanua kuwa zipo dawa zinazotolewa katika ngazi ya zahanati, kituo cha afya, hospitali za wilaya, mikoa na rufaa.

Timu ya waandishi wa habari na maofisa wa MSD wanatembelea mkoa wa Kagera kuangalia huduma ya usambazaji wa dawa kwenye vituo vya huduma.

Kuhusu watumishi, Dk Burchard amesema halmashauri ya Muleba bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi na wataalam wa afya licha ya kupokea watumishi wapya 16.

Mjumbe wa kamati ya afya ya zahanati ya Kisiwa cha Mazinga wilayani Muleba, Abdurauf Kietema ameiomba Serikali kuajiri watumishi wa sekta ya afya ili kuwapunguzia adha ya kufanya kazi muda mrefu watumishi katika maeneo ya huduma za afya za umma.

“Zahanati yetu ya Mazinga inayohudumia wananchi zaidi ya 7,000 kutoka visiwa vinane ina watumishi wawili pekee ambao ni mganga mfawidhi na muuguzi mmoja. Hii inakwamisha lengo la Serikali la kuongeza upatikanaji wa dawa na kuboresha huduma,” amesema Kietema.

Tayari, Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika imetangaza nafasi za ajira zaidi ya 6,000 katika sekta ya afya kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kote nchini.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz