Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hali ni tete upatikanaji damu nchini

Damu Uptika Ajiii Hali ni tete upatikanaji damu nchini

Sun, 20 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Hali ya upatikanaji wa damu katika vituo vya afya nchini imeelezwa kuwa ni tete huku makundi muhimu yanayohitaji damu yakipambania kidogo kinachopatikana.

Utafiti uliofanywa na gazeti hili katika maeneo tofauti umeonyesha Hospitali ya Taifa Muhimbili, KCMC, Bugando, Rufaa Mbeya, Ocean Road na Benjamin Mkapa na baadhi ya hospitali za mikoa na wilaya bado upatikanaji damu si wa kuridhisha.

Makundi yaliyotajwa kuwa hatarini zaidi ni yale yenye idadi ndogo ya watu yaani asilimia 1 ya Watanzania ambayo ni makundi hasi yaani ‘negative’ yakihusisha A- B- AB- na O-.

“Mgonjwa wetu alilazwa Amana, ilitukuchua saa nyingi kupata damu. Haikupatikana kwa wakati mpaka ilipokwenda kufuatwa benki ya damu. Ukiangalia benki ya damu pale ipo karibu inakuwaje kwa mgonjwa aliyepo mkoani?,” alihoji Naomi Ilomo.

Ufinyu wa upatikanaji wa damu unaelezwa kuwa umetokana na kupungua kwa mwamko wa uchangiaji damu miongoni mwa jamii.

Advertisement Hali ilivyo

Baadhi ya vituo vya afya mikoani na kanda vimeeleza kuwa uwepo wa ufinyu wa wachangiaji umesababisha kupungua kwa idadi ya damu iliyopaswa kukusanywa katika kipindi cha mwishoni na mwanzoni mwa mwaka huu.

Ofisa mipango na uhamasishaji wa damu salama Kanda ya Kaskazini, Feisal Abubakari alisema upatikanaji wa damu katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba mwaka 2021 ulikuwa chini ya kiwango.

Alisema badala ya kukusanya chupa za damu 7,896 zilikusanywa chupa za damu 3,708 sawa na asilimia 48.2 huku akisema sababu ni kutokana na shule pamoja na vyuo kufungwa.

Feisal alitaja mpango wao ni kukusanya chupa za damu 60 hadi 100 kwa siku ili kuweza kukidhi mahitaji ya damu katika Hospitali mbalimbali.

Alisema kuanzia Januari mwaka huu upatikanaji wa damu ulikuwa wa kusuasua kwa sababu asilimia kubwa ya wachangiaji walikuwa ni wanafunzi wa sekondari na vyuo.

“Timu ya ukusanyaji wa damu ilijitahidi kufika maeneo mbalimbali ikiwemo misikitini, makanisani na maeneo mengine lakini mwitikio haukuwa mkubwa na kusababisha kupatikana kwa kiwango cha damu hafifu kulingana na matarajio yetu,” alisema.

Alisema kipindi cha Januari hadi Februari 2022 hali ya upatikanaji wa damu umeanza kuimarika na kwamba, matarajio ni kukusanya chupa za damu zaidi 15,000 kwa mwaka kwa Kanda ya Kaskazini kutokana na malengo waliyojiwekea.

Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ilieleza kuwa inatarajia kukusanya chupa za damu 46,496 kwa kipindi cha mwaka huu ili kukabiliana na changamoto za huduma hiyo.

Meneja Mpango wa Damu Salama wa Kanda hiyo, Dk Lelo Baliyima alisema matarajio yao kwa mwaka huu ni kukusanya kiasi hicho cha damu katika kukabiliana na changamoto ya huduma hiyo kwa wahitaji.

Baliyima alisema kwa sasa kanda hiyo haina ukosefu mkubwa wa damu licha ya kwamba changamoto kwa jamii katika kujitolea imekuwa tatizo kubwa hadi kutegemea zaidi wanafunzi wa sekondari na vyuo.

Licha ya kutotaja akiba waliyonayo sasa, alieleza kuwa hali si mbaya kwani hakuna mtu anaweza kupoteza uhai wake kwa kukosa damu akifafanua kuwa upatikanaji ni wa kawaida na akiba ipo.

Alisema kutokana na mwitikio mdogo wa jamii katika kujitolea damu, wameandaa programu mbili maalumu ambazo ni kutembelea shule na vijiji pamoja na kuandaa vipindi maalumu kwenye redio ili kuhamasisha uchangiaji damu.

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha Hospitali ya Benjamin Mkapa, Jeremiah Mbwambo alisema kwa sasa kiasi cha damu salama kinatosheleza.

“Katika hospitali yetu huwezi kusikia kashfa ya uuzaji wa damu kwa wagonjwa. Tunajitosheleza, lakini jitihada ni kuweza kufikia malengo yetu ya kukusanya chupa 300 kwa mwezi,” alisema.

Alisema mahitaji makubwa ya damu yapo katika hospitali hiyo kutokana na aina ya huduma wanazotoa ikiwa ni ufunguaji wa moyo na upandikizaji wa figo.

Mbwambo alisema pea moja ya kupandikiza figo inahitaji chupa kati ya 20 hadi 30 katika operesheni moja.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ibenzi Ernest alisema mahitaji ya damu salama katika hospitali hiyo ni chupa 40 kwa siku.

Hata hivyo, alisema mahitaji hutegemea ukubwa wa shughuli za siku hiyo na kuwa kunapokuwa na ajali za barabarani nyingi mahitaji ya damu huwa ni makubwa.

“Changamoto kubwa huwa ni kwenye group (makundi) ya damu hasa negative huwa mara nyingi tunakuwa hatuna na hivyo inatulazimu kuomba kwenye hospitali za wilaya ama kwenye benki ya damu salama,” alisema.

Mahitaji halisi

Kaimu Mkuu wa Idara ya ukusanyaji damu, Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Kizito Tamba alisema bado hawajafikisha makusanyo ya asilimia 100 ya damu kama ilivyo mpango wa mwaka kukusanya chupa 550,000 ikiwa ni asilimia moja ya idadi ya watu milioni 55 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi.

“Ilikuwa tufikie makusanyo ya chupa 600,000 kutokana na idadi ya watu kufikia milioni 60 kwa sasa, lakini bado tunaihesabu ile 550,000. Mpaka sasa tuna uwezo wa kukusanya damu chupa 315,000 mpaka 320,000 kwa mwaka,” alisema Kizito.

Kizito alisema idadi hiyo pia bado haijafikia malengo ambayo walijiwekea ya angalau kukusanya asilimia 70 mpaka 75 ya mahitaji ya nchi yaani chupa 350,000 kwa mwaka.

Alisema katika makusanyo ya damu, kuna makundi manne yanayolengwa zaidi wakiwemo wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wagonjwa wa ajali na magonjwa mengine ikiwemo selimundu, saratani na malaria.

“Tunahudumia wagonjwa 3,000 kwa mwezi wenye saratani wanaohitaji kuongezewa damu, lakini ukiangalia kundi la watoto chini ya miaka mitano ni kama asilimia 40 ya Watanzania,” alisema.

Kizito alisema jukumu la kukusanya damu lipo chini ya Wizara ya Afya kupitia mpango wa taifa wa damu salama na Ofisi ya Rais – Tamisemi.

“Sisi taasisi ya Serikali tunakusanya damu na mipango ni kupata asilimia 40 na kwa upande mwingine ni halmashauri ambazo zipo chini ya Tamisemi ambao wao jukumu lao ni kukusanya asilimia 60,” alisema.

Nini sababu

Licha ya kuwepo kwa mipango hiyo, Kizito alisema katika makusanyo bado hawawezi kupata asilimia zote kutokana na changamoto zilizopo.

“Kuwafikia wachangiaji ndiyo changamoto kubwa. Inawezekana miundombinu bado si rafiki kuna maeneo ya vijijini hayafikiki na mijini watu wapo bize na mambo yao, ili kuwafikia elimu inahitajika zaidi. Ili kupata damu tunahitaji watu zaidi, binadamu asipochangia hakuna damu hata tukiwa na matrilioni ya fedha hatutaipata,” alisema.

Kizito alisema mwamko bado ni mdogo na kundi kubwa wanalolitegemea zaidi ni wanafunzi wa shule za sekondari na vyuoni lakini huko kwa sasa kuna changamoto nyingi. Alitaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni pamoja na kundi la wanafunzi wengi msingi mpaka sekondari kuwa na umri wa chini ya miaka 18.

“Miaka ya sasa watoto wanawahi kuingia shule anaanza darasa la kwanza akiwa na miaka mitano anamaliza na miaka 12 anaingia sekondari akiwa na miaka 13 anamaliza na miaka 16 sasa huyu kuja kumpata ni chuoni ambako hata hivyo bado changamoto zinakuwepo,” alisema na kuongeza;

“Lazima awe na miaka 18, lazima awe na uzito wa kilogramu 50 na zaidi, asiwe na magonjwa ya kurithi na awe na afya bora anapochangia hivi ni vigezo vikuu kwa mchangiaji sasa hapa tunawaacha wengi pia.”

Hata hivyo, alisema ufinyu unaoonekana sasa umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa makusanyo kipindi cha Desemba na Januari.

Aliongeza kuwa baadhi ya maeneo wamekuwa wakishindwa kwenda kufanya makusanyo ya damu kutokana na asilimia 20 ya damu kuwa haifai ‘maambukizi’ hivyo maeneo hayo mara nyingi wamekuwa wakishindwa kurudi tena kwa mara nyingine.

“Kuna maeneo mnaweza kwenda kukusanya tukapata damu zenye maambukizi ya virusi mbalimbali ikiwemo homa ya ini, hatuwezi kurudi tena eneo hilo,” alisema.

Katika mambo ambayo wengi hawayajui ni kuhusu mgawanyo wa damu. Kwa mujibu wa Kizito chupa moja ya damu inaweza kuwatosha wagonjwa watatu watu wazima na watoto watano mpaka sita.

“Kuna mazao mbalimbali ambayo yanaweza kuvunwa na kuwekewa binadamu wakiwemo wajawazito na waliotoka kujifungua, chembe sahani wanaweza kuwekewa wagonjwa wa saratani na chembe nyekundu wanapewa watoto chini ya miaka mitano, walioumwa malaria na wagonjwa wengine,” alisema.

Makundi adimu

Makundi hayo adimu ya damu ni yale yenye vinasaba (-) ambayo yana uwezo wa kuyachangia makundi yote, mfano kundi la damu la O- (O negative). Kuna makundi makuu manne ya damu ambayo ni A, B, AB, O na kila kundi lina aina yake ya vinasaba ambavyo (+) na (-).

Kizito alisema licha ya kukusanya damu nyingi, bado wanakabiliwa na uhaba kwa kundi la wenye vinasaba hasi yaani ‘negative’.

Alisema asilimia moja ya Watanzania wana kundi maalumu liitwalo ‘negative’ huku asilimia 99 yao wakisalia kuwa kundi ‘positive’.

“Hili kundi la negative A- B- AB- 0- kwa ujumla wake wana shida na kwenye hospitali nyingi damu zao hazipo, wao hawapokei damu nyingine vinginevyo zaidi atapokea wa kundi lake au mwenye kundi O-, ambaye anaweza kumpa yeyote mwenye negative ila yeye hapokei nyingi zaidi ya O- mwenzake,” alifafanua Kizito.

“Wenye damu za vinasaba positive ni wengi damu zao zipo tu mara nyingi haisumbui ila wale wa negative ni wachache ni asilimia 1 tu ya Watanzania unaweza kukuta hata hapa Dar es Salaam wapo 100 sasa hawa kuwapata ni vigumu na ili kuwe na ahueni lazima wawe na utamaduni wa kuchangia damu.”

Alipoulizwa iwapo kuna hatua zozote za kufuatwa iwapo mtu akiwa anahitaji damu, Kizito alisema:

“Daktari akisema unatakiwa kuongezewa damu kuna utaratibu wa kuitafuta na hospitali ndiyo wanatafuta, ndugu kutafuta damu ni hulka yao kwa kuwa wengi wanajua anaweza kukosa matibabu au kupoteza maisha ila si kazi yao ni kazi ya hospitali,” alisema Kizito.

Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Lulu Chirande alisema changamoto damu ni chache, lakini kuna aina ya makundi yenye uhitaji zaidi.

“Tunawahitaji zaidi wenye makundi ya O wachangie kwa wingi kwa maana hii inahitajika zaidi na wanapewa wengi zaidi ikilinganishwa na mengine.

Damu na sifa zake

Kuna makundi makuu manne ya damu ambayo ni A, B, AB, O na kila kundi lina aina yake ya vinasaba ambavyo (+) na (-).

Kuna makundi mengine ni nadra kupatikana kwa watu. Kundi hilo lina uwezo wa kuyachangia makundi yote, mfano kundi la O negative, lakini yeye anachangiwa na mwenye kundi lake pekee.

Watu wenye kundi A+ wanaweza kuongeza damu kwa wenye kundi A+ na AB na kupokea damu kutoka kundi A+, A-, O+ na O-, kundi B+ wanaongeza damu kwa kundi B+, AB+ na kupokea damu kutoka kundi B+, B-, O+ na O-.

Pia watu wenye kundi O+ wanaongeza kwa wenye kundi O+, A+, B+ na AB-, huku wakipokea kutoka kundi O+ na O-. Kundi AB+ anaongeza damu kwa kundi lake pekee na kuwapa wote wa makundi mengine.

Kwa mwenye makundi adimu A- anaongezwa damu na kundi A+, A-, AB+ na AB- na kupokea kutoka kundi A- na O-, kundi B- anaongeza kwa makundi B+, AB+ na AB-, huku lenyewe likipokea damu kutoka kundi B- na O-.

Nalo kundi la AB- linaongeza damu kwa AB+ na AB- na kupokea kutoka kundi AB-, A-, B- na O- wakati kundi O- lina uwezo wa kusaidia wagonjwa wote wenye kuhitaji damu, lakini yeye watu wote hawawezi kumsaidia pindi anapokuwa na uhitaji isipokuwa mwenye damu inayooana na yake pekee.

Mikakati ikoje

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale alisema kuanzia mwaka 2017/2018 takwimu za ukusanyaji damu zinaripotiwa kulingana na mwaka wa fedha wa Serikali Julai-Juni, ambayo inaendana na utekelezaji na bajeti ya Wizara ya Afya.

Alisema kwa mwaka 2020/2021 takwimu zinakusanywa kwa miezi mitatu mitatu inayoitwa robo mwaka ambapo jumla ya chupa 331,279 zilikusanywa ambayo ni sawa na chupa 6 kwa kila wananchi 1,000 sawa na asilimia 60 ya mahitaji.

Aliitaja mikakati ya kuongeza ukusanyaji damu ikiwemo uelimishaji na uhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa uchangiaji damu wa hiari kupitia michezo, mitandao ya kijamii na njia zingine.

Dk Sichwale alisema mpango utaweka utaratibu wa kuwa na ushirikiano wa muda mrefu na wadau, taasisi, na vikundi mbali mbali mfano taasisi za dini, wanamichezo, wasanii.

Alisema mikakati mingine ni kuhakikisha wagonjwa wahitaji wanapata damu kwa wakati, uwepo wa rasilimali watu, fedha, vifaa, vifaatiba na vitendanishi.

Imeandikwa na Herieth Makwetta (Dar), Janeth Joseph, Saddam Sadick na Sharon Sauwa.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz