Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

HEKAYA ZA MLEVI: Bingwa wa macho hatibu sikio

73657 Macho+pic

Sat, 31 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbwa ana mambo ya ajabu kidogo. Kwanza inasemekana anaona rangi mbili tu, nyeusi na nyeupe. Panapo kiza yeye huona vitu vyote kuwa vyeupe, na kwenye mwanga huviona kwa rangi nyeusi. Ajabu yake ya pili ni mwepesi kutii amri japo haelewi hata lugha moja. Mara ya kwanza unapomwambia “Toka” atatingisha mkia huku akikutazama usoni. Mara ya pili ataketi, ya tatu atajilaza na mwisho ataondoka.

Anapoona umeridhika ndipo atakapoondoka kila ukisema neno hilo. Usijidanganye kuwa mbwa wako anajua Kiingereza kwani anaketi unaposema ‘Sit’. Bila shaka alipitia zoezi kama hilo hapo juu mpaka alipolipatia.

Mbinu ingine anayoitumia ni kukusoma hisia zako za usoni. Atatingisha mkia kwa furaha au kuufyata kwa woga kutegemea pozi utakalomsimamia unapomweleza. Tafsiri yako ya usoni (kama utajibebesha ndita au tabasamu) ndiyo inayomtafsiria unachomaanisha.

Ukitaka kumchanganya mbwa wako muamuru kwa sentensi. Mwambie “Mwizi yule, kamkamate upesi!” Atasimama akikutingishia mkia bila kufanya lolote akisubiri useme “Kamata!” au “Shika!”

Ukimsifu “Wewe ni mbwa mzuri sana, unakesha getini hata wezi wanaogopa kuingia” atakutingishia mkia. Hata ukimkanyagia na kumpaka “We boya sisi tukilala unaenda kupiga misele kwa michepuko yako!” atafanya vivyo hivyo.

Yeye anasikia kwa lugha yake (default) ya “Wu… wuwu… wuh!!!” Ama unaweza kumfananisha na mtoto anayesikia na kuita “Mma” kila kitu. Tofauti ni kwamba mtoto anabadilika kila akuavyo, lakini mbwa hubaki kama alivyo.

Pia Soma

Advertisement   ?
Kadri mtoto anavyokua anaongeza uwezo wa kuelewa. Katika umri wa chekechea anaweza kusoma sentensi ya maneno matatu mpaka matano bila ya kituo. Na kwa kufuata uasilia wa maumbile ya kibinadamu, mtaala bora kabisa wa Shule ya Msingi ukajengwa.

Mtoto aliingia darasani akiwa na madaftari mawili tu, la vyumba lililotumika kwa hesabu na la mistari miwili miwili la mwandiko. Wakanywa uji, wakaimba na kucheza na kuondoka ilipotimu saa tano asubuhi. Ungemwongezea masomo au muda angesahau kila kitu.

Ujanani binadamu anaweza kumudu kusoma na kuelewa sentensi ya urefu wowote bila kituo, masomo mengi zaidi na kuhifadhi fomula za hesabu zisizo na idadi. Hata hivyo ikumbukwe kuwa “ukitaka kuruka mtaro agana na nyonga yako”. Kadri anavyokuwa mtu mzima anapunguza uwezo huo.

Ni maumbile ya kibinadamu. Alianza kulala, akatambaa, akatembea hadi kukimbia. Lakini anapozeeka anarudia njia ileile ya utoto. Hivyo huwezi kumpata daktari bingwa mmoja wa magonjwa yote hata awe na akili vipi. Bingwa wa macho hawezi kutibu sikio.

Kwa tamaa za kujua kila kitu watu wanaingilia mtaala bila kukumbuka kuwa waliousuka walizingatia asili na maumbile ya mtu. Tena bila hata kuzingatia kuwa kila kwenye mabadiliko makubwa kuna changamoto kubwa. Watu wakataka maendeleo ya ghafla wakimbizane na teknolojia yao.

Tukaona shule za msingi zikifuata mtaala wa shule za kimataifa ili kuzifanya zishindane kimataifa. Utadhani hawakujua kuwa shule za kimataifa zipo kwa ajili ya watoto wa mabalozi na raia wa nje wanaoishi nchini kwa sababu maalum.

Wanafundishwa elimu watakayokutana nayo watakaporejea kwao, lakini na Kiswahili cha kuulizia njia kwa wenyeji wao. Zile za kwetu zikaona donge wenzetu kuongea Kiingereza tangu chekechea, zikabadili lugha na mtaala mzima.

Kila kona ya shule kukawekwa matangazo ya ‘Speak English Only’ na ‘Marufuku kuongea Kiswahili’. Lugha ya Taifa ikaporomoka kwa kiasi kikubwa. Watoto wa chekechea wakapotezewa mfumo wao kwa sababu sasa iliwabidi kujifunza masomo yao na ya wenzao. Ungeona begi la madaftari analobeba kila asubuhi ungetamani begi hilo limbebe yeye! Hakutofautiana na msafiri aliyembeba punda!

Kila nikiitazama fursa iliyotangazwa Sadc natamani kulia. Kila Mtanzania angefaidika na dodo hili lililolala mchangani, lakini tutamfunzaje mgeni kuongea Kiswahili wakati sisi wenyewe tumeshayumba? Amini usiamini kamusi yetu inaelekea kutafsiri “Motorcycle” kuwa bodaboda badala ya pikipiki!

Usirogwe kuuliza maana ya “Mama mia!” kama sikosei utajibiwa “kudadadeki!” Hizo ndizo changamoto za maendeleo yasiyo ya kimtaala. Akiikosa maana shuleni ataitafuta mtaani.

Kila kwenye swali, majibu lazima. Tuna changamoto sekta ya elimu kama uhaba wa walimu, na hii ya walimu wa facebook. Lakini kwenye fursa hii ni lazima tufanye jambo kuionyesha dunia kuwa wenye lugha tupo hai. Mawazo yangu ya mwanzo ni kuwaamsha walimu wastaafu kama nyenzo ya kwanza, wanaweza kuziba baadhi ya mapengo na kuwapiga msasa walimu “bongofleva” warudi njia kuu. Lakini nyenzo ingine ni kuvishawishi vyuo (hasa vyuo vikuu) kuichukulia fursa hii katika uzito wa kipekee. Niliwahi kusikia kuwa wageni hufundishwa pale kwa miezi mitatu kuchukua shahada ya Ualimu wa Kiswahili kwa wageni.

Naona ni jambo la mbolea wao kuwapa motisha Watanzania kuhudhuria kozi hizo ili wakafundishe. Ni sawa wanaijua lugha yao, lakini lazima pia kujua misingi na miiko ya kufundisha. Isije kutokea mwalimu akajibiwa fyongo na mwanafunzi wake, naye akamtwisha gumi la uso!

Chanzo: mwananchi.co.tz