Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gwajima aanika chanzo cha ugonjwa wa akili

6f7c6368ef106eb1523fddafd909a069 Gwajima aanika chanzo cha ugonjwa wa akili

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Dorothy Gwajima ametahadharisha Watanzania kutambua kuwa matumizi ya vilevi kupita kiasi, ukatili na msongo wa mawazo ni mambo yanayosababisha ugonjwa wa afya ya akili miongoni mwa Watanzania wengi.

Dk Gwajima alitoa tahadhari hiyo wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Mayenga (CCM) aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani kusaidia watu wenye afya ya akili, wanaojichukulia hatua za kisheria huku hatua za kuthibitisha tatizo lao zikichukua muda mrefu.

Akijibu swali hilo, alikiri kuwa tatizo la afya ya akili linasababishwa na mambo mengi ikiwemo vinasaba vya kibailojia, lakini pia sababu kubwa ni namna watu wanavyoishi katika maisha yao ya kawaida.

“Naomba muelewe kuwa matumizi ya kila kitu kupita kiasi si mazuri. Matumizi ya vilevi, bangi, pombe kupita kiasi yanaweza kusababisha tatizo la afya ya akili. Kuna watu wanafanyia wenzao ukatili, hili sijambo jema, linaweza kusababisha msongo na kupata ugonjwa huu,” alisisitiza waziri huyo.

Aliwatahadharisha Watanzania kuepuka kufikiria na kuwaza sana kuhusu maisha yao. “Kuna wengine wanawaza namna maisha yao yalivyo magumu, hali inayosababisha msongo wa mawazo na wakati mwingine huishia kwenye tatizo la afya ya akili,” alisema.

Katika swali lake la msingi, Mbunge waViti Maalumu, Mariam Kisangi (CCM) alitaka kujua nini chanzo cha ugonjwa huo wa tatizo la afya ya akili na serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia wagonjwa wenye tatizo hilo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Godwin Mollel, alisema kitaalamu hakuna sababu moja inayosababisha ugonjwa wa afya aya akili.

Alisema sababu za tatizo hilo ni mjumuiko wa sababu au vichocheo, ambavyo mhusika amebeba kwenye vinasaba vyake, hivyo zikikutana katika mazingira muafaka huweza kusabisha msongo wa afya ya akili na kuzaa ugonjwa.

“Katika sababu za kibailojia, uwepo wa vinasaba katika mwili vinaongeza uwezekano wa mtu kupata ugonjwa wa afya ya akili, maradhi ya muda mrefu na matumizi ya vilevi kama bangi, pombe na aina nyingine za vilevi zinaweza kuwa vichocheo hasa kwa mtu mwenye vinasaba vya uhatarishi wa ugonjwa,” alieleza.

Alisema katika kuwasaidia wagonjwa wa afya ya akili, serikali imeandaa Sheria ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Akili ya mwaka 2008 ambayo inatoa mwongozo na utaratibu wa namna ya kuwapokea na kuwahudumia watu wenye ugonjwa wa akili.

Alisema sheria hiyo pia inajumuisha wagonjwa wa afya ya akili kuwa miongoni mwa makundi maalumu yaliyopewa msamaha katika sera ya afya.

Alisema pia serikali imehakikisha kuwa huduma za matibabu ya ugonjwa wa afya ya akili ikiwa ni pamoja na dawa, zinatolewa kuanzia ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa hadi Hospitali Maalum ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe.

“Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu ushiriki wa wazazi katika kuwalea na makuzi ya watoto. Kuongeza udahili wa wanafunzi wa uzamivu kutoka wanafunzi watatu hadi watano ilipofika mwaka 2015 na kufikia udahili wa wanafunzi 10 hadi 15 kwa mwaka ilipofika 2020. Pia kuongeza idadi ya vyuo vikuu vinavyotoa shadaha ya uzamivu kutoka kimoja mwaka 2015 hadi vitatu mwaka 2020,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz