Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Glasi moja tu ya pombe, huweza kusababisha kifo

13940 POMBE+PIC TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Utafiti mpya umebaini kuwa hata ukinywa glasi moja tu ya pombe, unajiweka katika hatari ya kupata maradhi ikiwamo saratani.

Ripoti ya utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Tiba cha Washington na kuchapishwa na Jarida la Afya la Lancet uliangalia unywaji wa pombe na madhara yake katika nchi 195 duniani.

Utafiti huo unaeleza kuwa hakuna kiwango salama cha unywaji wa pombe na kila glasi ina madhara yake.

Utafiti huo ulioangalia wanywaji wa pombe kuanzia wenye umri wa miaka 15 hadi 95, umebainisha kuwa mgonjwa mmoja kati ya kumi alifariki kwa sababu ya pombe.

Pia utafiti huo ulionyesha kuwa kati ya watu 100,000 wasiokunywa pombe ni 914 tu ndio wanasumbuliwa na matatizo ya kiafya kama saratani au moyo.

Lakini watu wanne au zaidi wanapata madhara kama wanakunywa pombe hata chupa au bilauri moja kwa siku.

Lancet limeeleza utafiti huo ulifanywa kati ya mwaka 1996 hadi 2016 na ulilenga kuangalia kiwango cha pombe na madhara yake kiafya.

Katika utafiti wao watafiti hao walisema walilinganisha watu ambao wanakunywa pombe hata chupa moja kwa siku na wale wasiokunywa kabisa.

Kiongozi wa utafiti huo, Dk Max Griswold kutoka Taasisi ya Health Metrics and Evaluation (IHME) katika Chuo cha Washington alisema wale wanaokunywa pombe hata chupa mbili kwa siku, 63 kati yao huanza kupata mabadiliko ya kiafya.

“Lakini wale ambao hutumia chupa tano kila siku, utafiti huu unaonyesha watu 338 wanapata madhara zaidi kiafya,” alisema.

Alibainisha katika utafiti huo kuwa upo uhusiano mkubwa wa matumizi ya pombe na hatari ya kupata saratani pamoja na magonjwa ya kuambukiza.

Daktari kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi, Kituo cha Tiba Muhimbili, Tawi la Mloganzila Shindo Kilawa alisema ni sahihi kuwa pombe inaweza kusababisha magonjwa zaidi ya 200 ikiwa mtumiaji atatumia kupita kiasi.

“Zaidi ya vifo milioni tatu duniani hutokana na matumizi mabaya ya pombe,” alisema.

Alieleza kuwa mwanaume anashauriwa kutumia glasi moja ya mvinyo (2-2units) na mwanamke (1-1.5 units).

“Kwa mfano matumizi mabaya ya pombe yanaweza kuathiri ini, mfumo wa chakula, figo, magonjwa ya ngozi, akili na hata saratani,” alisisitiza.

Dk Kilawa alisema watumiaji wa pombe kupita kiasi huweza kufanya jambo asilotarajia kama ngono zembe na mwisho, kuambukiza magonjwa ya ngono ikiwamo Ukimwi kwa sababu hali ya kufikiri huweza kuathiriwa na ulevi.

“Hata hizi ajali za barabarani, watu wengi wamepoteza maisha kwa sababu ya pombe, unapoiathiri akili yako kufanya kazi ya kawaida maana yake umeipa ugonjwa, huwezi kufikiria kama mtu mzima,tumepoteza watu wengi kwa sababu ya pombe,” alisisitiza.

Mtaalamu wa Lishe kutoka Jukwaa la Lishe nchini (Panita), Debora Essau alisema ni rahisi kwa wanywaji wa pombe kupita kiasi kupata utapiamlo.

“Mtu akinywa pombe kupita kiasi anakosa hamu ya chakula kwa sababu kwenye pombe kuna kalori (calories) nyingi hivyo mnywaji atahisi kushiba muda wote na mwisho anaanza kudhoofika,” alisema.

Alisema pia kwa sababu pombe huchujwa kwenye ini, mnywaji yupo katika hatari ya kupata ugonjwa wa ini ambalo huchoka kwa kazi hiyo.

“Kwa sababu pombe zinatofautiana, wanywaji wa pombe zinazotengenezwa kwa shayiri, hujikuta wakitumia kilevi hicho na nyama na hivyo hupata mafuta ambayo mwisho wake huwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo.” alisema.

Alisisitiza kuwa kihalisia pombe haina lishe hivyo mnywaji anapoitumia zaidi na kushindwa kupata lishe bora huwa kwenye hatari ya kupata magonjwa mengi zaidi.

Watumiaji

Baadhi ya watumiaji wa pombe wamekielezea kinywaji hicho kama viburudisho vinavyowasaidia katika mambo mengi ikiwamo kupambana na msongo wa mawazo. “Binafsi huwa nikipatwa na ‘stress’ zozote hata za kazini pombe huwa msaada wangu mkubwa, labda tuzungumzie kupunguza kiwango cha unywaji lakini si kuacha kabisa,” alisema Deosdedith Tarimo, mkazi wa Dar es Salaam.

Mtumiaji mwingine wa pombe, Nehemia Charles alisema yupo kwenye mazoezi ya kuachana na kilevi hicho baada ya kushauriwa kutokana na madhara aliyopata kwenye ini.

Chanzo: mwananchi.co.tz