Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gharama zinavyowakimbiza wanaohitaji viungo bandia

62769 VIUNGO+PIC

Sat, 15 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa kawaida hakuna binadamu asiyependa kuishi bila kiungo chochote cha mwili wake.

Watu waliopatwa na matatizo yaliyosababisha kukatwa viungo vya mwili wamekuwa wakipambana kuirudisha furaha ya awali angalau waweze kufanya kazi asilimia chache ya shughuli zao walizokuwa wakifanya awali.

Mtu anaweza kupatwa na ulemavu wa kiungo kutokana na sababu nyingi ikiwamo ajali na kuugua saratani au kisukari.

Gazeti hili lilipiga kambi kwa saa nne katika kitengo cha huduma ya viungo bandia Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi na kushuhudia wahitaji wa viungo hivyo wakiwa katika harakati za kusaka huduma hiyo.

“Asikwambie mtu ulemavu usikie kwa jirani ila usikupate unaweza kukata tamaa ya maisha, ndivyo nilivyokuwa mimi baada ya kukatwa mguu chini ya goti. Nilipata ajali mwaka 2013 huko Kibaha Pwani,” anasema Margaret Matiliga.

Mwingine aliyekuwa akisubiri huduma hiyo, Hellen Mroso anasema hakuwahi kufikiria kuwa angekatwa mguu wake lakini kwa sasa ana matumaini ya kuishi na kuendelea na shughuli zake.

Pia Soma

Mtoto Shukrani Alex mwenye miaka 14 ambaye alizaliwa na ulemavu wa miguu yote miwili na mkono mmoja, anasema viungo bandia vimekuwa na nafasi kubwa katika mwili wake, licha ya kuchelewa kuanza shule kwa wakati kutokana na tatizo hilo.

Alex ambaye kwa sasa yupo darasa la tano katika Shule ya Msingi Mkoka huko mkoani Dodoma, anasema alilazimika kufika KCMC kwa ajili ya kubadilishiwa viungo bandia vya miguu ambavyo amekaa navyo kwa muda mrefu.

Mzee mwenye miaka 60 ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwasababu za kiusalama, anadai kuwa anatumia mguu bandia tangu mwaka 1980 baada ya kuumia kazini.

“Nilipata ajali nikiwa nalitumikia jeshi kwenye majibizano ya vita ya mwaka 1979; adui alinijeruhi, ilibidi nikatwe mguu,”anasema mzee huyo.

Anaeleza kuwa amekuwa akitumia mguu bandia tangu akiwa na miaka 21, hivyo hali hiyo ameizoea na hufika KCMC kila mara kwa ajili ya kliniki ambayo hupangiwa na wataalamu.

Mzee huyo anasema pengine watu wanafikiri kukatwa kiungo ndiyo mwisho wa maisha au shughuli za kimaendeleo lakini kwake ni tofauti kwa kuwa alitumikia nchi mpaka alipostaafu.

Mtaalamu wa viungo bandia azungumza

Prosper Kaaya ambaye ni mkuu wa kitengo cha huduma ya viungo bandia, anasema wagonjwa wanaohitaji viungo hivyo wanazidi kuongezeka kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha na ajali wanazopata.

Kaaya anasema mwaka 2018 walipokea watu 2,000 kutoka maeneo mbalimbali waliofika katika kitengo hicho kwa ajili ya huduma ya viungo bandia.

Anasema ajali zitokanazo na matumizi ya vyombo vya usafiri kama pikipiki zimesababisha mrundikano wa wahitaji wa viungo bandia vya miguu na mikono.

Kaaya anaongeza kuwa yapo magonjwa ambayo hayahusiani na ajali kama lililomkuta mmoja wa watu hao ambaye aliugua fangasi na kukawa mguu chini ya goti.

Anasema kisukari na saratani pia ni tatizo jingine linalochochea idadi kubwa ya wahitaji wa viungo bandia.

“Kwa sasa tunaona mfumo wa maisha umebadilika hasa watu kutozingatia lishe na hii imesababisha kushamiri kwa magonjwa ya sukari na saratani ambayo ndiyo magonjwa mahususi yanayosababisha kukatwa kiungo,” anasema kaaya.

Uanzishwaji wa kitengo cha viungo bandia KCMC

Kitengo kinachojihusisha na utengenezaji wa viungo bandia hospitani hapo kilianzishwa mwaka 1975.

“ Kwa sasa tunaweza kuwahudumia watu wanane hadi kumi kwa siku; kwa mwezi idadi inaweza kufikia 140 hadi 200,” anasema Kaaya.

Hata hivyo, anasema watu hutoka mikoa mbalimbali na nchi za jirani za Kenya na Uganda kufuata huduma hiyo

Changamoto

Kaaya anasema zipo changamoto kadhaa katika kitengo hicho hasa uhaba wa wataalamu.

“Kama mnavyoona watu wanaohitaji huduma ni wengi, lakini wataalamu ni wachache, wahitaji lazima wafanye mazoezi hapa wiki nzima, pindi watakapoanza kutumia kiungo bandia saidizi hadi tutakapojiridhisha,” anasema Kaaya.

Gharama

Licha ya idadi ya wahitaji kuonekana kubwa, lakini idadi ya waliopo nyumbani ni kubwa zaidi kuliko wanaopata huduma hiyo.

Kaaya anasema watu wengi hufika kwa ajili ya huduma, lakini wanapotajiwa kiwango cha fedha huondoka na hawarudi tena.

“Aliyekatiwa mguu chini ya goti anaweza kuchangia zaidi ya Sh900,000; gharama hizi zinakuwa kubwa kutokana na malighafi ambazo tunaagiza kutoka nje ya nchi,” anasema Kaaya.

Mteknolojia wa viungo, Neema Ngowi anasema watu wangeweza kupata huduma hiyo kwa uhakika endapo gharama hizo zingekuwa katika Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) au bima nyingine za afya.

Hata hivyo, Mroso ambaye alikatwa mguu anasema ameweza kumudu gharama hizo kwa kuwa amechangiwa fedha na familia yake.

Wadau wazungumza

Makamu mkuu wa chuo cha utengenezaji wa viungo bandia (TATCOT), Davis Shirima anasema upo uhitaji wa Serikali kuandaa sera zitakazowezesha upatikanaji wa viungo hivyo kwa urahisi kutokana na hali ya uhitaji kuongezeka.

“Kwa sasa uagizwaji wa vifaa vya kutengenezea viungo bandia unafanywa na hospitali, lakini kukiwa na mfumo maalumu wa kushughulikia kama ilivyo Bohari ya Kuu ya Dawa (MSD) gharama za viungo zitashuka na pia vitapatikana kwa urahisi zaidi,” anasema Shirima.

Pia, anasema ni vyema tafiti zifanyike ili kupata takwimu za wanaohitaki viungo, kuzalisha wataalamu wapya pamoja na kuanzisha vituo vya kutolea viungo bandia.

“Chuo hiki cha viungo bandia kina uwezo wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi 15 katika ngazi ya diploma kwa mwaka. Utaona idadi ni ndogo ikilinganishwa na uhitaji wa wataalamu hao, lakini inatokana na hali halisi ya uwapo wa vituo vinavyotolea huduma.

“Hatuwezi kupokea wanafunzi wengi ilhali wakihitimu hakuna vituo watakavyoenda kufanyia kazi, matokeo yake vijana wahitimu na kukaa mtaani bila ajira,” anasema Shirima.

Chanzo: mwananchi.co.tz