Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gharama vipimo vya maabara kupungua kwa asilimia 50

Gharama Pic Data Mashine 728 zimesambazwa nchi nzima

Mon, 7 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bohari ya Dawa (MSD) imesema manunuzi ya mashine kuu za uchunguzi wa magonjwa pomoja na vipimo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, itasaidia kupunguza gharama za malipo ya vipimo vya maabara kwa zaidi ya asilimia 50.

Mashine hizo ambazo tayari zimeshasambazwa katika vituo vya afya na hospitali za wilaya zipatazo 728 ni pamoja na ile ya kupima hematolojia ya mwili ‘full blood picture’, kupima kemia ya mwili ‘body chemistry’ na ile ya kupimia mkojo ‘urine chemistry’.

Hayo yamesemwa na Ofisa mdhibiti ubora MSD, Joseph Kitukulu wakati akitoa mada wakati wa mkutano kati ya Wizara ya Afya, waandishi na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu huduma za magonjwa ya figo nchini.

“Kati ya vituo vya afya na hospitali za wilaya zilizo chini ya Halmashauri 848, vinavyofanya kazi sasa hivi mpaka sasa tumeshasambaza mashine hizi katika vituo 728 bado 120 ambavyo vilikuwa vinamalizia ukarabati na vitu vingine mpaka mwezi Mei tunatarajia vituo vingine vitakuwa vimepelekewa mashine,” amesema Kitukulu.

Kitukulu amesema mashine ya kupimia mematolojia ya mwili (Hematology analyzer 3 Part Diff) kabla ilikuwa ikinunuliwa Sh14 milioni sasa baada ya kuingia mikataba moja kwa moja na watengenezaji tunainunua kwa Sh7.5 milioni.

Amesema mashine ya kupimia wingi wa damu kabla ilikuwa Sh800,000 na sasa MSD inanunua kwa Sh240,000.

Advertisement Aidha amesema mashine ya kupimia sukari katika damu (Glucometer) zamani ilikuwa kati ya Sh35,000 mpaka Sh55,000 sasa itapatikana kwa Sh11,000.

“Pamoja na punguzo hilo la gharama katika ununuzi wa mashine hizo, pia vitendanishi vya kutumika katika mashine hizo vimepungua kwa zaidi ya asilimia 50 kwa bei ya kununulia. Mfano kipimo cha Hematolojia ya Mwili (Full Blood Picture) ilikuwa Sh4500 sasa itakuwa Sh2000.

“Kipimo cha kupima sukari ilikuwa Sh500 Sasa itakuwa Sh150, kipimo cha wingi wa damu ilikuwa Sh2000 sasa itakuwa Sh600,” amesema Kitukulu.

Amesema si vituo vyote ambavyo vina mashine zote tatu, bali kuna vingine vina mashine mbili kutegemeana na kituo huku akisema mpaka kufikia Mei mashine zote tatu zitakuwepo katika vituo vyote 848.

Amesema mara baada ya mashine hizo kufikishwa, bei itapungua kwa kuwa MSD imenunua mashine hizo kwa bei ya chini kutoka kwa wazalishaji hivyo wanaviuzia vituo kwa gharama ya chini pia.

“Gharama zitapungua kwa zaidi ya asilimia 50 ukilinganisha na gharama za sasa na lengo la MSD kufikia mwaka 2014 tuweze kufanya makubaliano upya na wazalishaji wapunguze tena gharama,” amesema.

Kitukulu amesema gharama za vipimo zitatofautiana kwa ngazi za halmashauri na mkoa, “Itategemea na bei ambazo MSD inauzia vituo tutakaa chini na kuja na kutoa bei elekezi.”

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meja Jenerali Gabriel Mhidze amesema tangu MSD ifanye maamuzi ya kwenda moja kwa moja kwa wazalishaji kununua dawa, vifaatiba na vitendanishi wamekuwa wakipata bidhaa hizo kwa gharama nafuu zaidi ikiwemo mashine za kusafishia damu kwa wagonjwa wa figo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live