Wakati akisherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa mfadhili wa Yanga, Ghalib Said Mohamed 'GSM'amefika Hospitali ya Ocean Road na kutoa vifaa tiba vitakavyotumiwa na wagonjwa.
GSM amefika hospitali hiyo akiambatana na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.
Akizungumza hospitalini hapo Hersi alisema GSM ameamua kusherehekea siku yake kwa tofauti na kuamua kutoa vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh137 milioni.
Hersi amesema vifaa hivyo vitakwenda kuwasaidia wagonjwa wa saratani wanaofika hospitali hiyo ukiwa ni mchango wa GSM katika kusherehekea siku yake hiyo.
"Mara kadhaa sisi Yanga tumekuwa tukifika hapa na kuona mahitaji makubwa yanayohutajika kwa wagonjwa licha ya vitu tulivyokuwa tunaleta lakini tuliona bado Kuna uhitaji zaidi," amesema Hersi
"Kwa kutambua hilo basi GSM akaona kumbukumbu ya siku hii yake ya kuzaliwa aifanye kwa utofauti kwa kuwakumbuka watu wanaokuja kupata matibabu haya hapa hospitali.
Naye Mkuu wa Mkoa Chalamila amemshukuru GSM kwa kuguswa na mahitaji ya hospitali hiyo huku akiwataja wengine kukumbuka jamii yenye mahitaji kama alivyofanya mfanyabishara huyo.
"Hiki alichofanya GSM ni mfano mkubwa wa kuigwa angeweza kwenda kufanya kitu kingine Cha kustarehe lakini akaguswa na mahitaji haya ya wale ambao wanakuja hapa kupata matibabu," amesema Chalamila.