Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Figo, maini, moyo kuvunwa kutibu wagonjwa

18c0e0c7633c51b5d0f76f62712e532a.jpeg Figo, maini, moyo kuvunwa kutibu wagonjwa

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto imeanza kuandaa muswada wa sheria itakayosimamia uvunaji viungo vya binadamu zikiwemo figo, maini, moyo na mapafu ili vipandikizwe kwa wanaovihitaji.

Ofisa katika kitengo cha magonjwa yasiyoambikiza katika Idara ya Tiba kwenye wizara hiyo, Dk Linda Ezekiel alisema Dar es Salaam kuwa itatungwa sheria ya uvunaji na upandikizaji wa viungo vya binadamu kwa sababu huduma hiyo imeanza hivyo inahitaji sheria.

Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya figo aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds kinachomilikiwa na Kampuni ya Clouds Media ya Dar es Salaam.

Alisema baadhi ya watu huenda wapo tayari wakifariki dunia viungo vyao vitolewe wapewe watu wengine lakini hakuna sheria kusimamia hilo.

Dk Linda alisema suala la kutoa kiungo au viungo kwenye mwili wa binadamu litakuwa la kisheria litakalowahusisha watoaji, familia zao, madaktari na wanasheria.

“Hakuna pesa yoyote inayopaswa kuwepo pale katika ule uchangiaji, ni haramu. Unaweza kuweka bei yoyote kwenye kiungo chochote? Huwezi, uhai unaweza kuweka bei yoyote? Unaona eeh, kutoa kwa kweli ni moyo,”alisema.

Kwa mujibu wa daktari huyo ambaye ni mratibu wa huduma za figo nchini, anatumaini hadi mwakani sheria hiyo itakuwa imetungwa ili kudhibiti na kusimamia uchangiaji viungo vya binadamu yakiwemo macho.

“Mchakato ulianza tangu mwaka juzi na mimi sasa hivi ndio kazi mojawapo ambazo nazisimamia. Tumeshamaliza mchakato wa ndani ya wizara sasa hivi tunakwenda kupata mawazo ya wananchi kujua na wao wanasemaje,”alisema Dk Linda.

Alisema makundi yakiwemo ya kidini, vijana na vyuo vikuu yatahusishwa kwenye mchakato huo ili kupata mawazo yao kuhusu uvunaji huo.

“Unapotoa figo ya mtu ambaye yupo hai sio kusema kwamba eti unamhatarishia misha yake kwa sababu kitu kimoja kizuri ni kwamba tuna figo mbili. Ukikata figo moja kwenye sehemu tatu ina maana una vipande vingapi kama una figo mbili, sita,” alisema Dk Linda na kuongeza:

“Tafiti zipo wazi kwamba, kwa ufanisi wako wewe mpaka unapoishi miaka sitini, themanini au tisini unahitaji kipande kimoja cha hivyo vipande sita kwa hiyo ina maana una vipande vya ziada vitano lakini sasa huwezi kukatakata ukatoa kipande kimoja kimoja kwa hiyo ina maana ile figo moja unapoitoa bado unamuachia reserve (akiba) ya vipande viwili”.

Pia alitoa mfano wa kijana mwenye umri wa miaka 18 aliyepata ajali lakini hakuwahi kuwa na matatizo yoyote yakiwemo ya moyo na kabla hajafariki dunia alielezwa kuhusu kuchukua viungo vyake na alikubali.

“Macho yanaweza yakaenda kusaidia mtu, moyo unaweza ukaenda kusaidia mtu, figo inaweza ikaenda kusaidia lakini hivyo tunahitaji sheria ndio sasa tunashughulikia. Tukishakuwa na sheria tunakuwa na chombo ambacho kinasimamia uvunaji,”alisema Dk Linda.

Alisema watu wanaohusika na tamaduni za Mtanzania watahusishwa kwenye maandalizi ya muswada huo na akatoa mfano wa nchi ya Croatia kuwa hakuna mtu anayepata kiungo kutoka kwa mtu aliye hai na kwamba, viungo vyote vinavyopandikizwa hutolewa kwa watu waliopoteza maisha au wagonjwa mahututi.

“Ajali imetokea Mtwara, mgonjwa yupo kwenye ICU Ligula, yule mgonjwa alishasema mimi siku ya siku ikifika kama limetokezea jamani vitu viende kusaidia. Kwa sababu tuseme ukweli tukizika vinakwenda ardhini, vinapotea. Hivi ni viungo vingewasaidia watu,”alisema Dk Linda.

Alisema mtu akiwa na akili timamu, baada ya kueleweshwa na akisaini kukubali kutoa kiungo chake hatakuwa na kisheria kukidai kiungo hicho baadaye.

“Sio kwamba mtu anasema leo nenda katoe, ni process (mchakato), unakwenda hospitali, unafanyiwa cancelling (unasihi), sio mara moja, mara mbili, mara tatu, unakwenda kwa daktari wa magonjwa ya akili naye anakutathmini kwamba huyu, kusudi sasa kusiwe na element yoyote ya influence (ushawishi)…una familia unakaa nao unawaeleza,”alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz