Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fedha sherehe za Uhuru kukamilishia hospitali

E2aeb9921d95ca0ae1e73ea0a702d8ea Fedha sherehe za Uhuru kukamilishia hospitali

Fri, 4 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA kuadhimisha miaka 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara, serikali imesema hakutakuwa na matukio ya sherehe na Sh milioni 835.4 zilizotengwa kwa sherehe hizo, zitatumika kununulia vifaa vya Hospitali ya Uhuru ya mkoani Dodoma.

Imesema siku hiyo ambayo huadhimishwa Desemba 9 kila mwaka, kila mmoja atasherehekea pale atakapokuwa na akifanya kazi za kijamii.

Vifaa vitakavyonunuliwa katika hospitali hiyo ni vitanda, samani za ndani, vifaa tiba, maabara, kujenga barabara za ndani ya hospitali na kuiweka hospitali hiyo katika uzio.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati anazungumzia maadhimisho ya miaka 60 ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE). Alisema kuwa siku hiyo watu wanatakiwa kuwajibika kufanya kazi.

Majaliwa alisema maadhimisho kama hayo, sherehe zake zilisitishwa kufanyika mwaka 2018 na Sh 995,182,000 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho hayo zilielekezwa na Rais John Magufuli kujenga hospitali.

Alisema hospitali iliyojengwa kutokana na fedha hiyo inaitwa Uhuru, ambayo iko umbali wa mita 200 kutoka barabara ya Chamwino mkoani Dodoma na imefikia asilimia 92 ya ukamilikaji wake.

Alifafanua kuwa gharama za ujenzi wa hospitali yenye ghorofa mbili ni Sh bilioni 4.2, na Rais Magufuli aliongeza Sh bilioni 2.4 kukamilisha ujenzi huo. Fedha hizo zilitokana na gawio kutoka Kampuni ya Simu ya Airtel.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Novemba 20, mwaka huu, Rais Magufuli aliongeza fedha Sh bilioni 1.6 ili hospitali hiyo ikamilike na kutoa huduma kwa wananchi, na matarajio ni mwishoni mwa mwaka huu ianze kazi.

Chanzo: habarileo.co.tz