Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fanya haya baada ya mazoezi makali

33204 Dk+Shita+Samwel Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni kawaida wafanya mazoezi mepesi hadi yale magumu mara tu baada ya kumaliza mazoezi kukumbana na hali fulani ya mwili kupata uchovu, maumivu au kupa majeraha ya mwili.

Na hali hiyo huweza kuwa ovyo zaidi kesho yake mara tu baada ya kuamka asubuhi, unaweza kupata hisia ya kuwa huenda ni dalili ya magonjwa mengine ikiwamo malaria.

Yako mambo yanayoweza kufanyika ili kuepukana na hali hiyo ambayo huchangiwa na uchovu katika viungo vya mwili hivyo kurudisha utimamu wa mwili na kukufanya kuwa na hamu ya mazoezi.

Jambo la msingi kabla ya mazoezi hakikisha umejenga hulka ya kupenda kunywa maji mengi kabla ya kuanza mazoezi ya kila siku, kiafya inashauriwa kunywa maji mengi masaa mawili kabla ya mazoezi.

Kunywa maji angalau lita 2-3 au glasi 8-10 kwa siku, maji hayo yawe safi na salama. Kumbuka maji ndani yake huwa na madini ambayo hukurudisha maji na madini yaliyopotea kwa njia ya jasho.

Mara nyingi kukamaa kwa misuli husabababishwa na upungufu wa maji mwilini hasa kwa wafanya mazoezi wanaocheza katika maeneo ya joto.

Baada tu ya kumaliza mazoezi hakikisha unatumia angalau dakika tano kufanya mazoezi yakulainisha na kunyoosha viungo vya mwili halafu baada ya hapo kunywa maji mengi.

Mbinu hii inasaidia kuondoa mkazo wa misuli na kuifanya misuli iwe tepetepe hivyo kukufanya usihisi hali ya uchovu au mwili kuuma. Ukiweza fanya usingaji wa mwili (massage) kwani ni moja ya tiba rahisi ya kuondokana na uchovu na maumivu ya misuli, vile vile kukupa utulivu wa kimwili na kiakili.

Uogaji wa maji ya moto na ya baridi ni moja ya tiba rahisi za kuupa mwili nafuu baada ya mazoezi magumu, inatakiwa baada ya kuumwagia mwili maji ya moto una malizia kuoga na maji baridi.

Maji ya moto huifanya mishipa ya damu kutanuka na kupeleka damu zaidi kutoka katika viungo vya ndani kwenda katika ngozi.

Wakati maji ya baridi yanaifanya mishipa ya damu juu ya ngozi kusinyaa kidogo hivyo damu nyingi hutoka katika ngozi na kuelekea kwa wingi katika ogani za ndani.

Mbinu hii huvifanya viungo vya mwili kuwa salama na kupata jotojoto hivyo kuongeza ufanisi wa viungo hivyo.

Baada ya kuoga pumzisha mwili katika maeneo yenye hewa safi ya kutosha na kisha jenga tabia ya kula matunda kwani kukupa na maji na sukari ambavyo vinaurudishia mwili nguvu na maji kwa haraka.

Baadaye kula mlo wako wa jioni ukizangatia kanuni za afya, kula chakula mchanganyiko na mlo uwe mwepesi na ule masaa mawili mpaka matatu kabla ya kulala.

Vyakula vya wanga vinakurudishia nguvu iliyotumika kwa haraka wakati protini inasaidia koponesha majeraha na kujenga mwili ikiwamo misuli

Baada ya hapo hakikisha unalala mapema, angalau ulale masaa 6-8 kwa usiku mmoja.

Mbinu hizi ndizo zinawafanya wafanya mazoezi makali kumka siku ya pili akijiona ni mpya, kama utazidi kuhisi uchovu au viungo kuuma fika katika huduma za afya kwa ushauri.



Chanzo: mwananchi.co.tz