Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Familia zina mchango ukatili wa kijinsia kwa watoto’

01c6e4e53502997d7d85053eed8753be ‘Familia zina mchango ukatili wa kijinsia kwa watoto’

Mon, 31 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

IMEELEZWA vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto kwa kiasi kikubwa vinachangiwa na wazazi wasiozingatia malezi ya kimaadili katika familia zao, lakini pia wanafamilia kutovipa ushirikiano vyombo vya sheria katika kesi za wanaotenda ukatili huo.

Kwa mujibu wa watetezi wa haki za binadamu, vitendo vingi vya ukatili wa kingono kwa watoto vinafanywa na baadhi ya wanafamilia husika.

Mapungufu hayo ya kifamilia yameendelea kutoa mwanya kwa watu wazima walioporomoka kimaadili kufanya ukatili wa kingono dhidi ya watoto na kukwepa mkono wa sheria.

Matokeo yake baadhi ya watoto waliotendewa ukatili huo huishia kukosa haki zao licha ya vitendo hivyo kuwaathiri kimwili, kiakili na kisaikolojia kama si kuwaharibia mustakabali wa maisha yao ya baadaye.

“Mara nyingi ukatili wa kingono kwa mtoto unafanywa na watu wa karibu na mtoto, siyo watu wa mbali,” anasema Shehe Eliasa Abeid, mjumbe wa dawati la utetezi wa haki za binadamu lililopo Igombe, kata ya Bugogwa wilayani Ilemela, Mwanza.

Abeid aliyezungumza na HabariLEO wilayani Ilemela hivi karibuni, anasisitiza kuwa wazazi wa zama hizi ni kisababishi kikuu cha visa vya ukatili huo katika jamii.

“Baadhi ya familia zinaishi katika mazingira amabayo watoto wanakuwa hawana malezi mazuri, unakuta hadi saa mbili za usiku mtoto hayupo nyumbani. Ukumuuliza mzazi anakwamba eti anacheza na wenziye hapo. Watoto wa kike wanatembea ovyo, muda wanaotakiwa kuwa nyumbani kwa ajili ya kujisomea na kusaidia kazi unakuta wako kwenye madisko, maharusi na mambo mengine yasiyoendana na umri wao.

“Wazazi wa sasa tunawalea watoto kidijitali, mtoto anaachiwa kutazama televisheni hata mambo yasiyofaa kwa tamaduni zetu, anakuwa na uhuru uliopitiliza, hakanywi, hafokewi na haelekezwi, na hayo mazingira mtoto anaanza akiwa na miaka mitano.

“Matokeo yake anakuwa mtoto wa hovyo, hawezi kudhibitiwa, mwishowe anajiingiza kwenye vitendo visivyofaa mpaka anafanyiwa ukatili wa kingono,” anasema Abeid ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Kitaifa la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Mwenyekiti wa dawati hilo, Mwalimu Mashaka Musiba, anasema eneo la Igombe limekuwa na matukio mengi ya ukatili wa kingono kwa watoto kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu kutoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria.

“Kata ya Bugogwa, hususan hapa Igombe ni eneo la uvuvi, kuna mwingiliano mkubwa wa watu wanaotoka mila na desturi tofauti, watu wanakuja na tabia nyingine ambazo ni hatarishi,” anasema Musiba na kuendelea:

“Kwa hiyo vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 vipo, tunashirikiana na Jeshi la Polisi kuchukua hatua lakini baadhi ya kesi zinashindikana kufika mwisho kutokana na upande wa mtoto aliyefanyiwa ukatili kutokwenda kutoa ushahidi mahakamani, hivyo baadhi ya kesi kuishia kufutwa.”

Musiba ambaye ni mwalimu huyo wa Shule ya Msingi Kisundi wilayani Ilemela, anatoa mifano kadhaa ya visa vya ukatili wa kingono kwa watoto vilivyotokea katani Bugogwa kikiwamo cha mwanafunzi aliyepewa ujauzito na baba yake wa kufikia.

“Binti huyo ilikuwa amalize darasa la saba mwaka huu (2020), lakini alipewa ujauzito na baba yake wa kambo,” anasema Mwalimu Musiba.

Anaendelea: “Kilichofanyika, mama yake alimpeleka kimya kimya kupima ujauzito ikagundulika anao, badala ya kupeleka taarifa hizo shuleni hatua zianze kuchukuliwa, alirudi nyumbani akaanzisha ugomvi na mume wake, kuona hivyo mume wake huyo akatoroka.

“Jamaa anatafutwa mpaka leo hajulikani yuko wapi, ingawa hatuna hakuka, lakini inawezekana mama alimwambia ili kumsaidia ni vyema kukimbia. Ilikuwa mwaka jana (2019) mtoto aliposimamishwa masomo na huenda atakuwa ameshajifungua.”

Mwalimu Musiba anataja kisa kingine kuwa ni cha mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Bugogwa mwenye umri wa miaka tisa aliyenusuriwa kubakwa wakati wa likizo ya dharura ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19).

“Mtoto huyo alidanganywa na kijana fulani, kesi yake iko mahakamani, jamaa alikuwa anajaribu kumbaka, majirani wakashtukia lile dili wakapiga kelele akakamatwa,” anasema.

Anataja tukio jingine kuwa ni la mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kayenze Ndogo, mwenye umri wa miaka 16 aliyefichwa siku mbili mfululizo na kijana mwenye umri wa miaka 25.

“Huyo binti alipotea nyumbani kwa siku mbili, kisha ikagundulika alikuwa amefichwa ndani na kijana huyo kule Kayenze Ndogo, suala lake nalo liko mahakamani linashughulikiwa. Kwa hiyo changamoto kama hizi zipo,” anasema Musiba na kuongeza kwamba kesi hizo zinaweza zisifike mwisho kama wazazi watashindwa kutoa ushirikiano kwa mahakama.

Katika mfululizo wa matukio yenye ukakasi, Shehe Abeid anasema mtoto mwingine wa darasa la pili aliyebakwa katani humo mwaka 2017 nusura kesi hiyo ihujumiwe na ndugu wa mbakaji.

“Kipindi cha kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, wazazi wa vijana waliomkamata mbakaji wa mtoto yule walitaka kupenyeza vijisenti ili wale vijana wasiende kutoa ushahidi.

“Uzuri wale vijana ni Waislamu, hivyo nilimwagiza imamu wa msikiti wa lile eneo akawaita tukawaambia kama hawakutoa ushahidi kwa mujibu wa aya na hadithi ni kosa, na wao watakuwa wameshiriki kitendo cha kuzini na mtoto yule.

“Tukawaelimisha kwa mambo ya kidunia watakuwa wamefanya kosa gani na kidini watakuwa wamefanya kosa gani, wakatuelewa wakakubali kutoa ushahidi.

“Tukaenda mbali zaidi, tukawashikisha masahafu tukawaapisha ili tuamini kwamba hawatatugeuka, kweli wakaenda wakatoa ushahidi na yule bwana (mbakaji) akafungwa miaka 30, ingawa baadaye alikata rufaa, akaachiwa katika mazingira ambayo hatujui.

“Kwa hiyo, changamoto huwa zipo za watu kugoma kutoa ushirikiano au kupindisha ukweli kwa makusudi, hasa wazazi husika wanapopewa pesa na wahalifu lakini huwa tunajaribu kupambana nazo,” anaeleza Abeid.

Anita Dotto, Mwanasheria wa Shirika la Wadada Solutions and Gender Based Violence linalopiga vita ukatili wa kijinsia na kingono kwa watoto mkoani Mwanza anasema: “Ushahidi umekuwa ukikosekana na watoto wengine wanatoroshwa na wazazi au watuhumiwa wanatoroka,”

Anaongeza: “Sababu nyingine kubwa ya ukatili wa kingono kwa watoto ni ukosefu wa maadili, watu kutokuwa na hofu ya Mungu, elimu ya jinsi na ujinsia, athari za ukatili huo na ukosefu wa elimu ya haki na afya ya uzazi. Tumekuwa tukipaza sauti kwamba familia ndio sehemu salama kwa mtoto, lakini tumegundua ukatili mwingi unafanywa na wanafamilia.”

utokana na hali hiyo, mwanasheria huyo anatoa mwito kwa jamii kutambua kuwa mlinzi wa mtoto ni jamii nzima.

“Sisi sote tunahusika katika ulinzi wa mtoto, tumlinde mtoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili, na kingine, tuwaruhusu watoto wetu kupata elimu kuhusiana na masuala ya afya ya uzazi,” anasema Dotto na kuendelea:

“Wazazi wengi wanazuia watoto wao wakidai hawajakua, lakini ukatili wa kingono unatendeka sana kuanzia watoto wa miaka tisa hadi 14, hapo wanakuwa hawajielewi, kila wanachoambiwa wanasema ndio.

“Lakini mtoto angepata elimu hiyo (ya afya ya uzazi) na ya kujikinga na vitendo vya ukatili angejua mwili wake hautakiwi kuchezewa na mtu mwingine, angejua hatakiwi kujihusisha na vitendo vya ngono.

“Hivyo wazazi wapate nafasi ya kuongea na watoto wao juu ya mambo hayo, na watoto watambue huu ni wakati wao wa kuwa shule, wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya ngono.”

Kwa upande wake, Shehe Abeid anatoa mwito akisema: “Kwanza, wazazi tuishi na watoto kimaadili kwa sababu tunatarajia wawe watoto wema ili baadaye sisi tukishakuwa wazee wawe watu wazima wema ili watusaidie sisi na jamii kwa ujumla.

“Pili, watu wazima wanaopowafanyia watoto ukatili, wakumbuke kwamba mtoto wa mwenzako ni mtoto wako, jinsi ambavyo wewe mtu mzima huwezi kufurahia mtoto wako kufanyiwa ukatili, pia usiende kumfanyia ukatili mtoto wa mwenzako.”

Ukatili wa kingono kwa watoto pia unapigwa vita na Boresha Project chini ya Ushirikiano wa Kiimani Tanzania (The Tanzania Interfaith Partnership Association - TIP) unaoundwa na taasisi nne za kidini.

Taasisi hizo ni Baraza la Wakristo Tanzania (CCT), Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA, Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC) na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar (MoZ).

Maono ya TIP ni kutengeneza mtandao thabiti wa kiimani unaochangia uwepo wa jamii ya Kitanzania yenye afya, yenye kuthamini na maadili mema na kujenga kizazi kisicho na Ukimwi.

Chanzo: habarileo.co.tz