Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia za Dar kutibiwa kwa Sh150,000 kwa mwaka

Fri, 11 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umetangaza kuanza kuandikisha wananchi wa mkoa huo kutumia kadi ya bima ya afya ya jamii (CHF) ambapo kila familia yenye watu sita itatakiwa kulipia Sh150,000.

Familia hiyo ni ile yenye watoto wanne akiwemo baba na mama, wakati kwa wale ambao hawana familia wao watapaswa kulipa Sh40,000 kila mmoja huku kadi hizo zikidumu kwa mwaka mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamisi Januari 10, 2019, kuhusu namna ya  kupata huduma hiyo, Mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda amesema uandikishaji wa kupata kadi hizo za CHF utaanza rasmi Januari 13, 2019 katika serikali za mitaa.

Makonda amesema wamefikia hatua hiyo kama moja ya njia ya kuwapunguzia wananchi ugumu wa kupata huduma za afya wanapougua kutokana na kukosa fedha na kuongeza kuwa vituo vitakavyokuwa vinatumika ni vile vya serikali.

"Tayari tuna waandikishaji 1,090 ambao ukipiga hesabu za haraka kila mtaa utakuwa na waandikishaji wawili, hima wananchi mkajiandikishe,” amesema Makonda.

Amesisitiza kuwa, "Hatutaki mtu auze bodaboda yake kwa ajili anaumwa au anauguza, au kupita mtaani kuomba msaada wakati bima hiyo nina uhakika kila mtu ana uwezo wa kuimudu kutokana na kuwa katika gharama ya chini."

Wakati kwa wale wenye familia ambayo ina zaidi ya watu sita, Makonda amesema huyo aliyezidi itabidi alipiwe Sh40,000.

Awali, Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Maghembe amesema walichelewa kuanza kutambulisha huduma hiyo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuruhusu kadi moja kutumika katika wilaya zote tano za mkoa huo.

Naye Nicholas Mwangomo, ambaye ni kaimu meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) makao makuu, amesema kadi hizo zitaanza kutumika wiki mbili tangu mtu alipojiandikisha.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz