TANZANIA na dunia kwa ujumla ipo katika jitihada za kuboresha lishe ya jamii kupitia mafunzo, utafiti na ulimaji wa mazao mbalimbali yakiwemo mazao lishe ambayo yana vitamini na madini kwa wingi.
Urutubishaji kibayolojia ni mchakato wa kuboresha lishe kwa kuongeza kiwango na wingi wa vitamini na madini katika mazao ya chakula kwa kutumia njia za kawaida za uzalishaji vipando au mbegu zilizoboreshwa kupitia utafiti, utunzaji wa mazao shambani au matumizi ya bayoteknolojia.
Mfano wa madini na vitamini yanayoweza kuongezwa kwa kutumiwa katika urutubishaji kibayolojia ni pamoja na vitamin A, madini ya zinki na madini ya chuma.
Msingi wa makala haya ni uzinduzi wa mradi wa kubiasharisha mazao lishe (kuyafanya mazao lishe kuwa ya kibiashara) uliofanyika katika ngazi ya taifa tarehe 20 Agosti mwaka 2020 katika jiji la Dodoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali na viongozi wa kiserikali.
Kwa lugha ya kimombo mradi unajulikana kama Commercialization of Biofortified Crops (CBC) unaotekelezwa na mashirika ya kimataifa ya Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) na Harvest Plus.
Mashirika hayo yanashirikiana na wakulima, wachakataji wa mazao lishe na mashirika yasiyo ya serikali.
Malengo ya mradi ni kuongeza mbegu za mazao lishe na nafaka, uchakataji na matumizi ya mazao lishe. Mazao lishe ya kipaumbele katika mradi huu ni pamoja na mahindi lishe na maharage yenye madini chuma kwa wingi.
Kwa miaka mingi wadau wa mazao lishe wamekuwa wakishirikishwa katika harakati za kuboresha lishe kama ilivyokuwa katika miradi ya kuwafikia waleta mabadiliko (Reaching Agents of Change) na Kapu la Mazao Lishe (Building Nutritious Food Baskets).
Miradi hiyo ilitekelezwa na shirika la kimataifa la International Potato Centre, miradi iliyohamasisha matumizi na uwekezaji wa mazao lishe kwa afya.
Kwa ufupi matunda ya waleta mabadiliko katika lishe waliopatikana ni kulima, kuvuna na kutumia maharage yenye madini chuma, mahindi na viazi lishe vyenye vitamin A kwa wingi.
Waleta mabadiliko wengine wameingia katika ujasiriamali wa kusambaza mahindi, maharage, unga na biskuti za viazi lishe.
Kimsingi zipo aina tatu za kupata mazao yaliyorutubishwa kibayolojia.
Mosi, njia ya kawaida ya kutumia uzalishaji kwa kutambua mazao yenye virutubisho vingi vinavyohitajika ambapo mazao mawili yenye sifa zinazohitajika kama vile kuhimili ukame au kutoa mavuno mengi katika eneo fulani hutumika kuzalisha aina ya mazao yaliyorutubishwa (likiwa na vitamin A, madini ya zinki au chuma).
Pili, urutubishaji wa mazao kibayolojia kwa kutumia agronomia ambapo hufanywa shambani kwa upuliziaji wa madini ya zinki au chuma kwenye majani ya zao husika, uwekaji wa madini husika kwenye udongo na hatimaye mazao hufyonza aina ya madini yanayohitajika kutoka shambani.
Tatu, urutubishaji kibayolojia kwa kutumia uingizaji wa jeni inayohusika na virutubishi kutoka aina moja ya zao kwenda kwenye vinasaba (DNA) vya aina nyingine ya zao linalokosa virutubishi vinavyohitajika.
Ifahamike kwamba urutubishaji kibayolojia hauhusishi kubadilisha kiini tete na hivyo si mchakato wa kupata mbegu za GMO.
Urutubishaji kibayolojia hufanyika kama mojawapo ya jitihada za kupambana na utapiamlo wa vitamini na madini.
Mbinu nyingine ni ulaji wa vyakula mchanganyiko na utoaji wa elimu ya lishe. Urutubishaji kibayolojia hufanywa katika mazao yanayotumiwa kwa wingi katika eneo husika.
Urutubishaji huu unalenga kuwafikia wakazi wa mijini na vijijini ambao wana uwezo mdogo wa kupata vyakula vilivyoongezwa virutubishi katika viwanda vikubwa.
Virutubishi katika mchakato huu wa kibayolojia unahusisha kundi la vitamini na madini ambavyo vinahitajika mwilini kwa ajili kazi mbalimbali muhimu na ukuaji wa mwili kikamilifu.
Imekuwa ikielezwa kwamba Watanzania wengi hawana shida ya protini, mafuta na wanga katika miili yao, isipokuwa madini na vitamini.
Ulaji wa vyakula vilivyorutubishwa kibayolojia unaongeza upatikanaji kwa wingi wa virutubishi lengwa, hali ambayo kutegemeana na afya ya mtu, inaweza kuboresha kiasi cha cha virutubisho mwilini na hivyo kuepuka madhara ya njaa iliyofichika.
Ulaji wa vyakula vilivyorutubishwa una manufaa kwa makundi katika jamii ambayo yapo katika hatari ya kupata upungufu wa virutubisho vinavyohitajika vya madini ya zinki, chuma na vitamin A.
Makundi hayo ni pamoja na wanawake wanaonyonyesha, wajawazito na wale wanaopata mlo duni kutokana na kipato. Aidha, watoto wana mahitaji makubwa ya virutubisho kuliko watu wazima kwa kuwa wao bado wanakua.
Serikali kupitia idara mbalimbali na nyakati tofauti imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha kwamba wananchi wanalima na kutumia vyakula vyenye lishe ya bora.
Hii ni kutokana na ukweli kizazi chenye afya bora ndicho kinachofanya kazi sana na hivyo kuleta maendeleo mijini na vijijini.
Kwa kutambua hilo serikali ilianzisha na kutekeleza mpango kazi wa masuala ya lishe (2017/21) ambao unatoa dira ya uboreshaji wa lishe Tanzania.
Mpango kazi huo unabainisha mchango wa wadau mbalimbali katika lishe bora.
Wapo wadau mbalimbali ambao wanafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba suala la lishe duni Tanzania linakuwa historia ikizingatiwa kwamba mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula ndiyo inayoongoza kwa udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Kwa sasa mazao ya kipaumbele katika miradi ya mazao lishe ni pamoja na viazi lishe vyenye vitamin A kwa wingi, mahindi yenye vitamin A pamoja na maharage yenye madini chuma na zinki. Tafiti mbalimbai zinaendelea ili kujumuisha mazao mengine yawe mazao lishe.
Kazi kubwa iliyobaki ni kuendelea kuelimisha jamii juu ya masuala yote yanayohusu urutubishaji kibayolojia. Jamii ikielewa vema juu ya urutubishaji kibayolojia itachukua hatua na kuhamasika kupanda mazao hayo kwa ajili ya biashara na lishe.
Ni muhimu wadau mbalimbali wajitokeze kufanya kilimo na biashara ya mazao lishe na kuwafikia walaji wengi kwa ajili ya lishe na biashara. Vijana na wanawake wajitokeze kufanya biashara hii ambayo itawaongezea kipato na kujikwamua kimaisha.
Wataalamu waendelee kuwaelimisha wakulima juu ya kilimo cha mazao lishe kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wenye tija katika maeneo yao.
Aidha, mashirika yanayojihusisha na kilimo, lishe na biashara watoe kipaumblele kwa miradi ya mazao lishe ili kuwafikia wanufaika zaidi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Hongera kwa wadau wa chakula wa Global Alliance for Improved Nutrition, ofisi ya Tanzania na Harvest Plus kwa kuona umuhimu wa kuyafanya mazao lishe kuleta kipato kwa wanawake na vijana pamoja na kuboresha lishe Tanzania.
Mwandishi ni Mwenyekiti wa kikundi cha Population and Development Initiative (PDI), Kigoma. Barua pepe: [email protected]. Simu: 0686355005