Ukimwi ni kundi la dalili za magonjwa mbalimbali ikiwamo magonjwa nyemelezi zaidi ya 20 pamoja na saratani mbalimbali ambazo hujitokeza baada ya kupata maambukizi ya VVU na kinga kushuka
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi mwaka huu ilikuwa “Tuziache jamii ziongoze”. Katibu Mkuu UN alishindilia kwa kusema “Ukimwi unapigika, Hebu tumalize kazi kwa kuziunga mkono jamii”
Kaulimbiu hii inatoa nafasi kwa jamii kujiongoza katika mapambano dhidi ya Ukimwi, ili dunia iumalize Ukimwi ifikapo 2030 kama moja ya malengo ya wadau wa afya wa duniani waliojiwekea.
Kuanzia ngazi ya familia, wazazi na walezi wanashauriwa kuzungumza na watoto wao ili kuwaelimisha kuhusu kujikinga, upimaji, matibabu, kujenga uaminifu katika mahusiano na kuepuka mienendo hatarishi.
Ukimwi ni kundi la dalili za magonjwa mbalimbali ikiwamo magonjwa nyemelezi zaidi ya 20 pamoja na saratani mbalimbali ambazo hujitokeza baada ya kupata maambukizi ya VVU na kinga kushuka.
VVU huenezwa kwa njia ya kuongezewa damu yenye VVU, kuwa na jeraha la wazi au michubuko na kugusana na damu au maji maji ya mwilini ikiwamo yale ya sehemu za siri yenye VVU.
Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hutokea wakati wa ujauzito, uchungu, kujifungua na kunyonyesha.
Kuchangia vitu vyenye ncha kali kama vifaa vya kunyolea, kutogea masikio na pua na kuchorea tatuu huchangia maambukizi kati ya asilimia mbili hadi nne.
Kujamiana kwa njia ya mdomo, hatari ya maambukizi ni ndogo kutokana na mate kuwa vimengeng’enya vinavyofifisha virusi. Ingawa unaweza kupata maambukizi kama kuna michaniko au fizi zinavuja damu.
Mate, jasho na mkojo havina virusi vya kutosha kuweza kumuambikiza mtu mwingine.
Endapo VVU wakifanikiwa kuingia kupitia nyuso za seli nyeupe hizo, hujidurufisha na kuendelea huvamia seli nyingine hatimaye kinga kushuka.
Upimaji na ubainifu wa virusi hutegemeana na aina ya kipimo. Kwa sasa vipimo vilivyopo ni vile vinavyobaini virusi-antigen, askari mwili waliotiririsha-antibody na tindikali ya nucleic.
Ingawa kuna kipimo cha kisasa cha kuweka chini ya ulimi ambacho kimeonyesha ufanisi mkubwa katika kubaini maambukizi. Vipimo vya kawaida vya haraka vinaweza kubaini VVU kwa uhakika baada ya siku 18 hadi 90 tangu kupata maambukizi.
Hivi sasa katika maduka ya dawa muhimu inapatikana kifurushi cha vipimo vya kujipima mwenyewe kwa usiri. Ingawa muhimu kufika katika huduma za afya.
Ikumbukwe kuwa kupima tena baada ya miezi mitatu inatoa uhakika zaidi kujua kama una maambukizi au hapana.
Matumizi ya kondomu yanasaidia kupunguza kasi ya maambukizi, lakini usahihi wa uvaaji na kuitumia usipofuata unaweza kupata maambukizi.
Vile vile matumizi ya vilainishi kama kupaka mafuta ya ziada katika mipira ya kiume yanaziharibu na kuongeza hatari ya kupasuka wakati wa tendo.
Matumizi ya vilainishi kama mafuta mazito na jeli yamekua yanatumika kiholela mtaani kwa baaadhi ya wasiotumia mipira na kuzungumzwa zaidi mitandaoni kama njia inayopendwa, ingawa haizungumzwi.
Kisayansi ni kweli mbinu hiyo inaweza kupunguza hatari ya kupata michubuko, lakini bado haizuii moja kwa moja kugusana na maji maji ya sehemu za siri ambayo ndio huwa na kiwango kikubwa cha VVU.
Kujamiana kinyume na maumbile kunaongeza hatari ya kuambukizwa VVU mara 30 zaidi kulinganisha na njia ya ukeni.
Watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga wanaoshirikiana vifaa wanaambukizwa VVU. Hali ya uraibu huwafanya kutokujali kuchukua tahadhari za njia za kujinga.
Ukimwi hauna tiba, isipokuwa zipo dawa za kufubaza makali ya virusi (ARVs) ambazo zimesaidia kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa zaidi ya asilimia 90.
Ni salama kujamiiana na muathirika wa VVU endapo tu ameshikamana na matibabu na kutumia dawa za ARVs, huku kiwango cha virusi ni kile kisichoweza kubainika.
Makundi yaliyo katika hatari ya kupata VVU kama vile wahudumu wa baa na wanaojiuza wanapewa dawa za kujikinga wanazotumia kabla ya kujamiana bila kinga.
Ukimwi upo na unaua. Ni wakati wa jamii wa kujiongoza katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu.