Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu walichosema viongozi wa Serikali katika mjadala magonjwa yasiyoambukiza

10499 Pic+fahamu TanzaniaWeb

Mon, 2 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Suala la kupambana na magonjwa yasiyoambukiza si la Serikali pekee, bali wananchi wote kwa kuwa msingi wake mkubwa ni aina ya maisha wanayoishi watu.

Ndivyo unavyoweza kufupisha ujumbe wa maofisa wa Serikali katika kongamano la Jukwaa la Fikra lililofanyika Alhamisi jijini Dar es Salaam kujadili tatizo la magonjwa yasiyoambukiza.

Mmojawao alikuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambaye alizungumzia umuhimu wa kila mmoja kuhusika katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ili kuisaidia Serikali kupunguza mzigo wa gharama za matibabu.

“Serikali imejitahidi kuboresha sekta ya afya lakini kuna mzigo mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza na jambo hilo limeongeza mzigo mkubwa kwangu,” alisema Waziri Ummy.

Alitoa mfano wa Hospitali ya Ocean Road inayopokea wagonjwa 50,000 wa saratani kila mwaka, akisema huenda idadi ni kubwa zaidi kwa kuwa wengine hawafiki hospitalini kutibiwa.

Waziri Mwalimu alisema hata bajeti ya kuhudumia hospitali hiyo katika dawa imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 ndani ya miaka miwili kutoka Sh700 milioni hadi Sh7 bilioni.

Alisema changamoto nyingine ni kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani wanaofika Ocean Road, wanakuwa wameshafikia hatua ya nne ya ugonjwa, ambayo matibabu yao ni shufaa (palliative care).

Matibabu hayo ni kwa ajili ya kumsaidia mgonjwa asife kifo chenye maumivu au kuongeza siku za kuishi.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya aliwataka wananchi kusoma maelezo yaliyoandikwa kwenye bidhaa wanazotumia ili kuepuka matumizi ya kemikali hatarishi.

Dk Ulisubisya alikuwa akizungumzia ushauri uliotolewa na mmoja wa wachangiaji wa mjadala huo, aliyependekeza yawekwe maelekezo ya kiwango cha sukari kilichopo katika bidhaa.

“Ni vizuri wananchi wakawa makini kusoma kile kilichoandikwa kwenye bidhaa wanazotumia. Changamoto ni kuwa wengi hawapendi kusoma,” alisema.

“Madhara ya sigara yameandikwa tena kwa herufi kubwa, lakini mtu ananunua na anavuta tu. Wengi wetu hatusomi hata maelezo yaliyopo kwenye juisi tunazokunywa.”

Alifafanua kuwa wazo la kutoa tahadhari ni zuri hasa kwa bidhaa za sukari, sigara na mafuta.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Profesa Yunus Mgaya alisema kasi ya kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa, hivyo ni vyema itengwe bajeti kubwa kupambana nayo.

“Lakini kuna upungufu kwa wananchi, hawana uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa haya. Hizi tafiti zinatakiwa ziwepo wizarani na ziwekwe kwa namna ambavyo zitaeleweka,” alisema Profesa Mgaya.

Alisema kutokana na ongezeko la magonjwa hayo, jitihada za ziada zinapaswa kufanywa na kila mmoja ili kupambana nayo.

Profesa Mgaya alisema tafiti za Nimr kwa sasa zinajikita katika kuangalia namna ya kutokomeza au kupunguza kabisa maradhi hayo badala ya kutibu.

Katika kutafuta huduma ya matibabu kwa magonjwa hayo, mdhibiti wa ubora kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk Raphael Malaba alisema wananchi wanapaswa kushirikishwa na kufahamu faida za matumizi ya bima ya afya.

Dk Malaba alisema nia ni kuwa na uhakika wa kupata matibabu pindi yanapohitajika si kujiunga wakiwa tayari wameugua.

“Wengi wanakuja kujiunga na bima wanapoona matibabu yao yanahitaji fedha nyingi, jambo ambalo limekuwa gumu kwetu na hatuwezi kupokea mtu akiwa mgonjwa hivyo tunalazimika kutoa elimu ili kuhakikisha wanakuwa na bima ya afya hata kama si wagonjwa,” alisema Dk Malaba.

“Lakini bado gharama za wanachama hawa zinaongezeka na idadi yao kuongezeka, kwa mfano wagonjwa wanaosafisha figo hutumia zaidi ya Sh46 milioni kwa mwaka kwa mgonjwa mmoja na sasa wako 189 nadhani, unaona gharama kiasi gani tunatumia.”

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kama visababishi vya magonjwa ya kuambukiza vitadhibitiwa, robo tatu ya magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari aina ya pili na asilimia 40 ya saratani yangezuiwa.

Viongozi hao wa Serikali waliwataka wananchi kuchukua hatua madhubuti za kupambana na maradhi yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yanachangia asilimia 30 ya vifo vya Watanzania.

Kongamano hilo ambalo ni la kwanza liliandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) linalochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. MCL ilishirikiana na kampuni ya ITV/Radio One ambayo vituo vyake vya redio na televisheni vilirushmoja kwa moja mjadala huo uliohudhuriwa na zaidi ya watu 400.

Miongoni mwa waliohudhuria ni wanafunzi wa udaktari kutoka vyuo vikuu tofauti vya jijini Dar es Salaam.

Chanzo: mwananchi.co.tz