Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu nguvu ya mazingira anayokulia mtoto

14321 Cristian+Bwaya TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Umewahi kufikiri kwa kiasi gani mazingira ya ndani na nje ya familia yanavyoweza kuathiri tabia ya mwanao? Unafanyaje kugundua athari za mazingira anayokulia?

Mwanasaikolojia nguli wa stadi za malezi, Urie Bronfenbrenner anatupa mwangaza kulijibu swali hili. Kwa kuanzia, anafafanua kuwa mazingira ni aina ya watu wanaomzunguka mtoto.

Mfano wa watu hao ni sisi wazazi, marafiki, majirani, walimu na watu wengine wanaoishi na mtoto wenye mchango katika kufinyanga tabia na mienendo ya mwanao.

Katika makala haya, tunaangazia mchango wa familia, majirani na mazingira ya shule katika kujenga au kubomoa tabia ya mwanao.

Mazingira ndani ya familia

Wazazi tunatofautiana kwa hulka na haiba zetu. Wapo wazazi wakali, wengine wapole; wapo waongeaji, wengine wakimya; wapo wenye upendo, wengine wagumu kuonyesha upendo.

Mchanganyiko wa tabia kama hizi kwa kawaida, hutengeneza ‘sheria’ fulani zisizoandikwa lakini zenye nguvu ya kumuongoza mtoto vile atakavyoishi na watu.

Fikiria mtoto aliyezaliwa kwenye mazingira ambayo baba na mama wanatukanana mbele yake. Mtoto huyu tangu anazaliwa, ufahamu wake utaamini kuwa ugomvi ndio mfumo rasmi wa maisha unaoweza kumfuata hata atakapokuwa mtu mzima baadaye.

Namfahamu ndugu mmoja mwenye tabia ya kulipuka kwa hasira. Ingawa hapendi tabia yake hiyo, lakini bado hujikuta akifoka. Baadaye nilibaini kuwa alilelewa kwenye mazingira ya hasira. Leo na yeye anafanya yaleyale asiyoyapenda.

Unaongeaje na mke au mume wako? Je, watoto wanakufahamu kama mtu mkali, mgomvi au mtu mwenye upendo na mwelewa? Je, unaweza kuwa na ujasiri wa kutamani watoto wawe na tabia kama hiyo uliyonayo?

Kumbuka kwamba kile unachotaka mtoto akifanye lazima kwanza wewe ukifanye. Hakuna miujiza. Ukitaka mtoto awe na tabia ya kusalimia watu, aombe msamaha, atoe pole kwa walioumia, lazima wewe mwenyewe uonyeshe mfano kwa hayo.

Unayoyafanya wewe ni shule kwa mtoto anayekutazama. Tabia zako zina nguvu ya kugeuka kuwa sheria kwa mwanao. Kuwa makini na yale unayoyafanya mbele ya mtoto.

Watoto wanaocheza na mwanao

Katika umri wa kati ya miaka mitatu na kumi, shughuli kubwa inayomvutia mtoto ni michezo. Kwa sababu mtoto anathamini michezo, ni wazi kuwa wale anaocheza nao watakuwa na nguvu kubwa ya kuamua afanye nini, afikiri nini, aende wapi na wakati mwingine awe mtu wa namna gani.

Kupitia urafiki unaojengwa kwenye michezo ni rahisi mtoto kukutana na watoto waliolelewa kwenye misingi tofauti na ile aliyolelewa nayo nyumbani kwao. Mtoto, katika mazingira haya, atakutana na wenzake anaowapenda sana lakini wanaofanya mambo tofauti na yale aliyojifunza akiwa nyumbani.

Mwanzoni inaweza kuwa rahisi kwake kuona tofauti na pengine akajitahidi kusimamia kile alichojifunza nyumbani kwao. Lakini kadri urafiki unavyoimarika na kwa sababu anatamani kuendelea kuwa karibu na watu anaocheza nao, hatua kwa hatua, anaanza kujifunza mambo mapya.

Kulingana na mazingira yake, inawezekana akajifunza mambo mazuri. Tunawafahamu watoto waliokulia kwenye familia zenye ugomvi, lakini wakajifunza kupenda watu kwa sababu tu walikutana na watoto wanaopenda watu.

Lakini kwa upande mwingine, iko hatari ya mtoto kuanza kujifunza vitu vya ajabu ambavyo hakuwahi kuvifanya akiwa nyumbani kwao. Wazazi tuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa tunafahamu watoto wetu wanacheza na kina nani.

Watu anaokutana nao shuleni

Mtoto anapoandikishwa shule, mbali na elimu rasmi ya darasani, shule inakuwa ni fursa ya kupanua wigo wa urafiki. Kupitia wenzake anaokutana nao shuleni, mtoto anaweza kujifunza mambo ambayo kwa sababu moja au nyingine hakujifunza nyumbani kwao.

Ukiwachunguza watoto unaweza kugundua kuwa zipo tabia njema watoto hujifunza kwa sababu tu walipata nafasi ya kufahamiana na wenzao wanaotoka kwenye familia zenye desturi tofauti na kule walikokulia wao.

Mfano kama mtoto hakufundishwa kuwavumilia wenzake nyumbani, kupitia uhusiano wake na wenzake shuleni, atajifunza kuwa na subira na kuvumilia tofauti zake na wengine.

Hata hivyo, iko hatari ya kukutana na watoto wenye tabia zisizofaa na akajikuta anaziiga. Tunafahamu kwa mfano, shule inaweza kumkutanisha na wenzake wanaoweza kumtukana, kumzomea na wakati mwingine kumdhalilisha kwa sababu tu yuko tofauti na wao. Mazingira kama haya yanaweza kumwathiri mtoto kisaikolojia.

Wapo watoto wanaopoteza hali ya kujiamini kwa sababu tu ya kuchekwa na wenzao shuleni. Ni muhimu basi kwa mzazi kuwa karibu na mtoto ili kung’oa ujumbe hasi unaopenyezwa kwenye moyo akiwa huko shuleni.

Hulka na mienendo ya walimu

Shule humkutanisha mtoto na watu wazima wanaoweza kuwa na sauti kubwa kuliko wazazi wake. Hapa kuna walimu wanaomfundisha, walezi wanaomhudumia akiwa kwenye mazingira ya shule na wakubwa zake wanaosoma madarasa ya juu.

Watu hawa, kila mmoja kwa sehemu yake, wanaweza kupanda mafunzo mapya mazuri ambayo mtoto hajawahi kuyapata akiwa nyumbani.

Ikiwa, kwa mfano, mtoto hajawahi kufundishwa kuheshimu wakubwa, shuleni atakumbushwa, tena wakati mwingine kwa adhabu. Ikiwa hakufundishwa kujitegemea, shuleni atalazimika kushika hiki na kile na atajifunza shughuli za mikono.

Pia kuna sauti ya mwalimu. Kwa kuwa huyu ndiye anayemfundisha mtoto elimu rasmi darasani, mtoto huamini kile anachokisema mwalimu ndio ukweli. Bila shaka umewahi kumwambia mwanao kitu akakubishia kwa sababu mwalimu wake hakumwambia hivyo. Tafsiri yake ni kwamba kile anachokisema mwalimu kinaweza kuwa na nguvu ya kuamua mtoto atajitazamaje na atawaonaje wenzake.

Katika mazingira kama haya, fikiria mwalimu huyu anasema maneno yanayomuumiza mtoto. Maneno kama, “Lioneni halina akili,” “Mchekeni huyo,” “Mzomeeni hajui hesabu” yanaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa mtoto.

Hivyo tunasisitiza walimu kuwa makini na lugha wanazotumia wanapokuwa na watoto. Mzazi, kwa upande mwingine, anahitaji kufuatilia kwa karibu uhusiano uliopo kati ya mtoto na walimu wake.

Chanzo: mwananchi.co.tz