Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu maisha ya aliyefanyiwa upasuaji na kutolewa viberiti, mswaki, betri tumboni

24621 Habari+pic TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nguvu ya ushirikina ndiyo iliyotawala tukio la Robert Novart mkazi wa Kijiji cha Katembe Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, aliyefanyiwa upasuaji na kukutwa na vyuma tumboni.

Wengi hawaamini kuwa ni tukio la kawaida pamoja na madaktari kuthibitisha kuwa vijiko, viberiti vya gesi, mswaki na betri ni vitu vinavyoweza kupita kwenye koo na kuingia tumboni.

Hatua ya vifaa hivyo kupita salama kwenye koo la Robert na kuingia tumboni hadi vilipotolewa kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Mugana, ni jambo lililowaacha wengi na mshangao.

Hata hivyo, kuna mambo mengi yasiyofahamika kuhusu Robert ambaye kwa mujibu wa taarifa za familia na madaktari ana tatizo la afya ya akili na miezi michache kabla ya kufanyiwa upasuaji alikuwa Hospitali ya Mirembe mkoani Dodoma akipatiwa matibabu.

Maisha baada ya upasuaji

Robert alifanyiwa upasuaji baada ya hali yake kiafya kuonekana ni mbaya.

Tangu alipofanyiwa upasuaji Septemba 28, mwaka huu, katika Hospitali Teule ya Mugana iliyopo wilayani Missenyi, Kagera na kurejea nyumbani, amekuwa akifungiwa katika chumba maalumu na si kila mtu anayeweza kumuona.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Katembe, Innocent Muganyizi ni miongoni mwa viongozi waliomtembelea baada ya

kurejea kutoka hospitali ambaye anasema sasa mgonjwa huyo amekuwa akifungiwa ndani kwa lengo la kuhakikisha ulinzi na usalama wake pamoja na kumdhibiti dhidi ya matukio yasiyo ya kawaida ambayo pia yanaweza kuwa hatarishi.

Anasema baada ya kurejea tu kutoka hospitali alipanda kwenye nguzo ya umeme na kusababisha umeme kukatika.

“Amefungiwa ndani ili kumdhibiti dhidi ya vitendo hatarishi. Baada ya kutoka hospitali alipanda nguzo na kusababisha umeme kukatika, kutokana na hali hiyo ukimuacha huru anaweza hata kujidhuru,” anasema Muganyizi.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo anasema pamoja na hofu iliyopo kwa wananchi kuhusu uwezekano wa kusababisha madhara, kwa sasa hawawezi kuchukua hatua yoyote zaidi ya kuongeza uangalizi dhidi yake kuhakikisha hakuna madhara anayoweza kusababisha.

“Huyu mtu hakuja kinyemela hapa kijijini utaratibu umetumika, hatuwezi kufanya lolote kwa sasa,” alisema.

Baba awa mbogo

Hata hivyo, licha ya Robert kufungiwa ndani, mzazi wake Novart Bigimbwa hataki kufuatiliwa taarifa za mtoto wake kwa undani baada ya kukataa kutoa ushirikiano pale alipofuatwa na Gazeti la Mwananchi kwa ajili ya kupata maelezo kuhusu maendeleo ya mtoto wake baada ya kufanyiwa upaseaji.

“Nimekwambia sihitaji msaada kama kuna msaada ungeletwa wakati tulipokuwa hospitali…sitaki kuulizwa tena, nawashukuru madaktari. Niliwahi kuulizwa nikashauri huduma ziboreshwe zaidi,” anasema.

Hata baada ya kutumia uongozi wa kijiji hicho kuomba kuingia kwenye nyumba inayodaiwa mgonjwa huyo amefungiwa hilo halikufanikiwa baada ya baba huyo kueleza kwa njia ya simu kwamba hawezi kuacha shughuli zake za shamba.

Kwa mujibu wa viongozi wa kijiji na majirani, katika nyumba hiyo anaishi mzazi wa Eliud na mfanyakazi na muda wote milango inaonekana kufungwa kwa kufuli huku mgonjwa akidaiwa kufungiwa ndani.

Jinsi alivyopelekwa Mirembe

Aliondoka kijijini hapo mwaka 2012 baada ya kuhusishwa na mauaji ya mtoto Faris Isack aliyekuwa na umri wa miaka mitatu ambapo katika utaratibu wa kisheria alilazimika kupelekwa hospitali ya wagonjwa wa akili Mirembe, mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa kaka yake aitwaye Gilbert Novart, mdogo wake aliachiwa huru na Mahakama Kuu katika vikao vyake baada ya kuthibitika ana tatizo la afya ya akili wakati akitenda tukio lililosababisha kifo cha mtoto huyo.

“Ilionekana hana hatia wataalamu wa hospitali ya Mirembe walimleta na gari na kumkabidhi nyumbani, walikuja naye na kutuachia dawa za kichaa. Wakati huo alikuwa bado anaumwa hata kuzungumza alikuwa hawezi,” anasema Gilbert.

Anasema mdogo wake hakuzaliwa na ugonjwa huo bali aligundulika kuwa na tatizo la afya ya akili baada ya kuonyesha tabia zisizo za kawaida ikiwemo kukaa kimya muda mwingi bila kuzungumza ambapo walichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kupelekwa kwa viongozi wa dini kwa ajili ya kumuombea.

Apokelewa kijijini

Kurejea kwa Robert baada ya miaka mingi tangu alipohusishwa na mauaji ya mtoto kuliibua hisia, maswali na kufufua mjadala wa tukio hilo la mauaji kijijini hapo.

Mwenyekiti Muganyizi anaeleza kuwa Robert alipokelewa kijijini hapo Mei 13, mwaka huu katika ofisi ya Kijiji cha Katembe mbele ya viongozi, baba na maofisa kutoka Hospitali ya Mirembe.

Muganyizi anasema waliomrejesha Robert kijijini hapo walikuja na barua iliyoelekezwa kwa mzazi wake na kukabidhiwa mbele ya mamlaka za serikali ya kijiji.

“Aliondoka baada ya mauaji. Wakati anafanya tukio hilo alikuwa hajawa mgonjwa sana. Tangu alipochukuliwa hatukujua kilichoendelea wao kule ndio wataalamu tuliamini ama ataendelea kuwa huko au atarudishwa baada ya afya yake kutengemaa. Hatukutegemea kama atarudi katika hali hii,” anasema Muganyizi.

Naye Mwenyekiti wa Kitongji cha Katembe ’A’ Filbert Mushema anasema tukio la mauaji ya mtoto Faris liliwashitua wengi katika kitongoji chake na kuwa siku anakabidhiwa akitokea Mirembe alikuwa mmoja wa mashuhuda na ofisi yake kupewa nakala ya barua ya kukabidhiwa.

Babu asimulia mjukuu wake alivyouawa

Tukio la mauaji ya Faris Isack aliyeuawa Februari, 2012 bado linakumbukwa na familia ya Dauda Abdalah ambaye alihusika kumfikisha mtoto huyo kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa taarifa na baadaye kumuwahisha Hospitali ya Nyakahanga ambako wataalamu walithibitisha kuwa amefariki dunia.

“Alipigwa kwa fimbo nilimpeleka kwa pikipiki kituo cha Polisi na baadaye hospitali ya Nyakahanga lakini kabla ya kupewa matibabu alikata roho. Robert alikuwa na mazoea ya kupiga watu,” anasema Abdalah.

Anasema kwamba tangu mtuhumiwa alipokamatwa na kusafirishwa hawakujua mwenendo wa kesi au kilichoendelea hadi miezi michache walipoambiwa ameachiwa huru na Mahakama baada ya kuthibitika alikuwa na tatizo la ugonjwa wa akili.

Anasema ni kweli watu wana hofu kijijini hapo baada ya kurejea kwake. “Hofu imeongezeka baada ya taarifa za kutolewa vyuma tumboni ingawa hakuna hatua yoyote tunayoweza kuchukua kwa sasa”.

Madaktari hawashangai

Mmoja wa madaktari wa hospitali ya Mugana walioshiriki upasuaji huo Eliud Nyonyi anasema ni kweli vifaa hivyo vilikutwa tumboni na kuwa si kila jambo linalohusu mgonjwa linaweza kuelezwa waziwazi.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Dk Hamis Abdalah alisema mgonjwa huyo alifika Hospitali ya Mugana akitokea Hospitali ya Nykahanga wilayani Karagwe.

Alibainisha kuwa baada ya kufanyiwa kipimo cha X-Ray Robert alionekana kuwa na vitu tumboni hivyo kulazimu afanyiwe upasuaji tarehe 28, Septemba na kukutwa na vijiko, mswaki, betri ndogo, viberiti vya gesi na ganda la limao.

Dk. Abdalah anasema kama mgonjwa huyo angecheleweshwa kupelekwa kwenye matibabu angepoteza maisha kwa kuwa utumbo ungechanika huku akisema kitaalamu vitu hivyo vinaweza kupita kwenye koo.

Alisema hadi anafikishwa hospitali vifaa hivyo vilikuwa havijakaa zaidi ya saa 48 tumboni.

Katika maoni yake kuhusu tukio hilo, Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Zaituni Bohari alisema matukio ya aina hiyo mara nyingi huwakuta watoto.

Alisema ni aina ya matukio ya wagonjwa ambayo huwa hayaelezeki ambapo baada ya mgonjwa kufanyiwa kipimo cha X-ray baadhi hukutwa na vitu mbalimbali tumboni kama lundo la nywele na kucha.

Chanzo: mwananchi.co.tz