Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu kuhusu kitita cha NHIF kitakachoanza Ijumaa

Nhif Bernad Konga 13.png Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernad Konga.

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetangaza kuanza kutumika kwa maboresho mapya ya Kitita cha Mafao kwa wanachama ambapo yatataanza rasmi siku ya Ijumaa ya tarahe 1 Machi, 2024.

Akitangaza kuanza kwa maboresho hayo, jana tarehe 28 Februari, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernad Konga amesema Kitita cha Mafao ni orodha ya huduma za matibabu ambazo zinatolewa kwa wanufaika wa NHIF na zitakuwa kwa bei nafuu zaidi ya hapo awali.

Konga amefafanua kuwa katika maboresho ya mwisho ya Kitita cha Mafao kinachotumika sasa yalifanyika Juni, 2016 lakini kwa kuzingatia hali ya maisha pamoja na maoni mbalimbali ya wadau wamelazimika kufanya maboresho hayo mapya.

“Ni takribani miaka nane sasa, hivyo kuwepo umuhimu wa kufanya marejeo yake kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo,” amesema Konga.

Amesema, miongoni mwa manufaa ya kitita ni pamoja na wanachama wanaotumia dawa za shinikizo la damu na sukari sasa wanaweza kupata dawa ngazi za chini lakini pia wanachama wanaopata huduma ya uchujaji damu gharama imeshushwa chini.

“Na huduma za kibingwa na bingwa bobezi kama matibabu ya moyo, saratani, figo zitapatikana kwenye ngazi za kanda pia na sio lazima mwanachama aende mpaka hospitali za ngazi taifa,” amesema Konga.

Konga amesema katia maboresho hayo NHIF wameongeza aina mpya za dawa zaidi 247 kwenye kitita, hivyo kumfanya mnufaika wa mfuko huyo kutokutana na changamoto ya kukosa dawa katika kituo chochote atakachoenda kupata huduma.

Baadhi ya waandishi wa habari wakimfuatilia Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernad Konga (hayupo pichani).

Amesema maboresho hayo pia yamekuja na nafuu kwa wanufaika wa mfuko huwa katika gharama za ushauri, dawa na matibabu.

Konga amesema gharama za maboresho hayo hazimgusi mwanachama bali ni kati ya NHIF na watoa huduma ili kuboresha zaidi huduma karibu na wananchi nchini.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, maeneo muhimu yaliyofanyiwa maboresho ili kuleta unafuu huo wa gharama ni ada ya usajili na ushauri wa daktari huduma za dawa na tiba za upasuaji na vipimo.

Konga ameongeza kuwa, mfuko huo unaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau kuhusu kitita hicho na pale maboresho yatakapofanyika wataendelea kutoa taarifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live