Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu jinsi ya kujikinga na virusi vya corona

Fahamu jinsi ya kujikinga na virusi vya corona

Fri, 6 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ugonjwa wa homa ya virusi vya corona (COVID-19) unasambaa kwa kasi duniani kote hivyo ni muhimu ku kuchukua tahadhari kutokana na mwingiliano mkubwa uliopo kati ya Watanzania raia wa China ambako homa ya virusi hivyo ilianzia, na wa nchi nyingine zilizoathirika na ugonjwa huo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limekua likitoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo ya mlipuko wa virusi hivyo na pia kuelimisha njia ambazo zinatumika kujinga na maambukizi ya ugonjwa huo ambao umeshaua watu 3,200 duniani kote, kuambukiza zaidi ya watu 95,000 na kusambaa katika nchi 80, kwa mujibu wa taarifa za jana.

Moja ya kanuni za kujikinga zinazotangazwa na WHO ni kuosha mikono mara kwa mara kwa sabuni au kemikali maalumu hata kama mikono haionekani kuwa michafu.

Sababu ya kufanya hivyo ni kwamba mtu anapoosha mikono kama inavyoelekezwa, anaweza kuondoa virusi hivyo endapo viko mikononi.

Kama ilivyotangazwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, unatakiwa kutokaribiana na watu. Hii, kwa mujibu wa WHO, inatakiwa kuwa angalau mita moja kati ya mtu na mtu, hasa kwa wale ambao wanakohoa, kupiga chafya au wenye homa.

Kukaa mbali kunasaidia kuepusha kusambaa kwa virusi kwa sababu mtu aliyeathirika na virusi vya corona anaweza kukohoa au kupiga chafya inayoambatana na mate yaliyobeba virusi hivyo. Kama uko karibu, unaweza kuvuta virusi hao.

Pia Soma

Advertisement
Tabia nyingine ya tahadhari ni kutoshika macho, pua au mdomo. Hii ni kwa sababu mikono inashika vitu vingi ambavyo vinaweza kuwa na virusi hao. Ukishika macho yako, pua au mdomo na mikono iliyo na virusi, unaweza kuhamisha virusi hao kutoka katika vitu hadi mwilini mwako.

Kama ilivyoshauriwa na mamlaka za afya, hakikisha unamripoti mtu yoyote mwenye dalili za ugonjwa huo. Na kama ni wewe na umebaini kwamba una homa, kikohozi au unapumua kwa shida, hakikisha unapata matibabu haraka.

Historia yako ya kusafiri ni muhimu. Unatakiwa umweleza mhudumu wa afya kama ulienda China ambako virusi hivyo viliibuka, au kama ulimkaribia mtu aliyetoka China na ana dalili za ugonjwa huo.

Kama utaripoti dalili hizo kwa haraka, wahudumu wa afya wanaweza kutambua mapema hasa kutokana na shida ya kupumua au tatizo jingine lolote mbali na virusi vya corona. Dalili za kifua na homa zinaweza kuwa na sababu tofauti, kulingana na historia yako ya kusafiri na mambo mengine ikiwemo Covid-19.

Kama una maumivu ya kifua na huna historia ya kusafiri katika nchi zilizoathirika, fanya mazoezi ya kupumua na kusafisha mikono. Kaa nyumbani hadi upone.

Kila siku Gazeti hili la Mwananchi litakuwa linakuletea vidokezo vya kujikinga na virusi hivyo kama linavyoonekana pembeni upande wa kulia.

Chanzo: mwananchi.co.tz