Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu jinsi ya kudhibiti homa ya mgunda

Nose Bleedoingg (600 X 392) Fahamu jinsi ya kudhibiti homa ya mgunda

Wed, 20 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wataalamu wa Afya wamesema ugonjwa wa Homa ya Mgunda ulioelezwa juzi na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu katika Mkoa wa Lindi, unazuilika na kutibika.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, ugonjwa huo unaoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu uligundulika mwaka 1886, ambapo uliripotiwa katika nchi mbalimbali duniani.

Akizungumza na HabariLEO, Mkurugenzi Msaidizi wa Epidemiolojia na Udhibiti wa magonjwa Wizara ya Afya, Dk. Azma Simba, amesema ni muhimu wananchi kuepuka kugusa maji yaliyochafuliwa na mkojo wa mnyama na kunywa maji safi na salama.

"Nawatoa hofu ugonjwa huo unazuilika na kutibika, wananchi wachukue hatua ikiwemo kuepuka kugusa maji yaliyochafuliwa na mkojo wa wanayama.

“Pia wajitahidi kunywa maji safi na salama yaliyochemshwa au kutibiwa kwa dawa,"amesisitiza Dk. Simba.

Amesema ugonjwa huo unaosababishwa na bakteria unasambazwa na wanyama kama panya, pimbi, swala na wanayamapori wengine.

"Inaonekana hata ng'ombe anaweza kusambaza, hawa bakteria wanaweza kuhama kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu, kupitia vyanzo vya maji au ardhi, yule mnyama kama atakojoa kwenye ardhi au maji na ule mkojo unaweza kuwepo bakteria anayeweza kuishi wiki moja," alieleza Dk Simba.

Amesema binadamu anapogusa kama ana mchubuko hata kama ni midogo anaweza kuambikizwa ugonjwa.

"Anapogusa maji, udongo unachukua chakula chenye bacteria hao anaweza kupata, anaweza kupata kwa kuogelea kwenye mito, vijito, ziwa, mafuriko ambayo yamechafuliwa na mnyama mwenye bakteria,” amesema.

Dk Simba amesisitiza kuwa endapo mtu atakuwa na dalili kama homa, kichwa kuuma, damu kutoka puani, kuchoka aende kwenye kituo cha kutolea huduma za afya.

" Kwa upande wake daktari bingwa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Elisha Osati amesema utafiti unaonesha kuwa ugonjwa huo ulishawahi kutokea nchini eneo la Kaskazini kwa jamii ya wafugaji.

"Lakini ni bakteria huyo anapatikana kwa wanayama kma popo, kangaroo, panya , ng'ombe, mbwa, nguruwe,” amesema.

Amesema bakteria hao wanaingia kwa njia ya mkojo wa wanyama na kwenda kwenye figo na kibofu.

"Kama ukigusa mkojo wenye bakteria na mkono na ukishika nao pua au macho anaweza kuingia,” amesema.

Amesema dalili za ugonjwa zinaonekaa kuanzia siku mbili hadi 30, kwani mdudu anapoingia mapafu yanaathirika.

Amesema ni muhimu kujikinga wakati wakihudumia wanyama kama vile kuvaa viatu aina ya buti na kunawa mikono baada ya kuhudumia wanyama.

"Wananchi wasiwe na wasiwasi, kwani unatibika ni bakteria ambao dawa zao inajulika wawe na utulivu na kuchukua tahadhari na kufatilia kwa makini.

"Nashauri mifugo ipewe chanjo au dawa zinazoweza kuzuia wadudu wasiingie na ushahidi unaonesha kuwa ugonjwa kutoka kwa mtu kwenda kwa mwingine ni nadra, lakini inaweza kutokea,” amesema.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk. Shedrack Mwaibambe amebainisha kuwa ni muhimu sehemu zenye upungufu wa maji ya kunywa safi na salama, serikali ifikirie kuwapatia wananchi suluhisho la kudumu.

"Vyanzo vya maji ndivyo hivyo hutumika kwa wanyama, basi wachemshe maji ya kunywa wajikinge na madhara yatokanayo na huu ugonjwa yanatibika, hivyo wafike hospital," amesisitiza Dk Mwaibambe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live