Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu athari za watoto kunywa mafuta ya taa, jiki

11930 Pic+fahamu TanzaniaWeb

Sun, 22 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Si ajabu kukuta chupa za maji za plastiki zimetumika kuhifadhi mafuta ya taa, au dawa ya kuondoa madoa kwenye nguo. Hii hufanyika zaidi nyumbani kwa lengo la kuepusha vimiminika hivyo visimwagike.

Je, umeshawahi kujiuliza ni hatari gani ambayo atakutana nayo mtu atakayekunywa mojawapo ya vimiminika hivyo akidhani ni maji?

Kama hufahamu basi chukua hii, kuna ongezeko kubwa la watoto wanaosumbuliwa na tatizo la kushindwa kumeza kutokana na kunywa dawa za kuondoa madoa au mafuta ya taa.

Akizungumza na gazeti hili, daktari bingwa wa upasuaji kwa watoto, Victor Ngotta alisema tatizo hilo hivi sasa limeongezeka.

“Sina takwimu sahihi ila ninachoweza kusema kesi za namna hii zimekuwa nyingi, awali ilikuwa unaweza kupata wagonjwa wawili au mmoja kwa miezi kadhaa lakini sasa unaweza kukuta wodini kuna wagonjwa watano wana tatizo la kushindwa kumeza na wakati mwingine ikapita mwezi au miezi usipate mgonjwa wa aina hiyo,” alisema.

Dk Ngotta alisema inapotokea mtoto amekunywa kemikali hizo husababisha njia ya chakula kuwa nyembamba hivyo kuzuia upitaji chakula.

Kuhusu matibabu, Dk Ngotta alisema wengi wanapona kwa kutanua sehemu iliyosichaa kwa kuingiza vifaa maalumu.

“Zoezi la kutanua linaweza lisifanyike mara moja kwa kuwa unatanua kidogo kidogo hadi itakapoonekana mgonjwa anaweza kupitisha chakula,” alisema.

Alisema iwapo njia hiyo itashindikana mgonjwa anapelekwa kwenye hatua nyingine ya upasuaji ambao inahusisha kukata eneo lililosinyaa na kuunganisha tena mrija wa chakula kwa kuushona.

“Upasuaji huu unahusisha kufungua kifua na kuipata sehemu iliyosinyaa kisha kuikata na kushona. Ikitokea eneo lililoathirika ni kubwa zaidi inalazimu kuvuta sehemu ya tumbo kuja kwenye kifua,” alisema Dk Ngotta.

Msaada wa maziwa

Dk Ngotta alisema kumpa maziwa mtu aliyekunywa kemikali za aina hizo ikiwamo mafuta ya taa hakumletei nafuu, bali inamweka kwenye hatari zaidi ya kuongeza tatizo.

“Ukimpa maziwa unakwenda kuamsha tabaka la ndani la tumbo, hali hiyo inapotokea upo uwezekano mkubwa akatapika. Anapotapika hapo tatizo jingine linaweza kutokea kwa kuwa anavyovitapika vinaweza kwenda kwenye njia ya hewa,” alisema.

Naye muuguzi katika kitengo cha upasuaji watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Kulwa Kahombwe aliwatahadharisha wanawake kuhusu utunzaji wa vipodozi na kemikali hizo nyumbani.

“Ni nadra kwa mtoto kutambua kilichopo kwenye chupa kwamba siyo maji kwa kuwa kina rangi na muonekano unaofanana na maji hivyo hukimbilia kuweka kinywani,” alisema Kahombwe na kuongeza: “Ukiweka vitu vya hatari kama hivyo kwenye chupa ya maji unamhatarishia maisha mtoto wako, kwa kuwa yeye anajua ni maji,”

Kuhusu matumizi ya mikorogo kwa wanawake wanaonyonyesha, alisema ni hatari kwa kuiweka bila tahadhari kwa kuwa watoto huishia kula sumu.

“Unakuta mtoto kila siku ana mafua anahangaika kupumua wanakimbilia kusema mtoto ana mzio sio kweli ni hiyo mikorogo,” aliongeza.

Chanzo: mwananchi.co.tz