WAKATI huu mgumu wa janga la virusi vya corona wengi ulimwenguni wamelazimika kutumia muda wao mwingi kukaa majumbani mwao ili kujikinga na maambuzi.
Sio kwa kutaka bali baadhi ya serikali zimetumia njia ya kuweka marufuku kutoka nje ovyo - kafyu ili kuwaepusha wananchi kupata au kusambaza ugonjwa wa COVID-19.
Wataalamu wanasema kuna hatari kubwa katika kulala sana, jihadhari hasa kipindi hiki cha coronavirus. Wataalamu wanasema kulala muda mrefu kitandani ni hatari sana kwa afya ya binadamu.
Katika hali kama hii, wengi wanaofanyia kazi nyumbani hujipata muda mrefu wakijikalia ama kulala kwenye masofa au vitandani mara wanapomaliza kufanya kazi zao, na wasiwe na likingine la kujishughulisha nalo.
Lakini wakati janga hili likiisha, wengi watagundua wana maradhi ambayo hawakuyatarajia huku wakijikinga dhidi ya virusi vya corona - maradhi hayo yanatokana na mtu kulala muda mrefu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Neurology Advisor ya Februari 26, 2015, ilibainika kutoka kwa wataalamu wa afya kuwa kulala zaidi ya saa 9 usiku na zaidi ya dakika 90 wakati wa mchana kunaweza kuongeza hatari ya mtu kupigwa na kiharusi.
Kulingana na ripoti iliyochapishwa kwenye jarida la "Neurology" la nchini China, watu 31,750 wenye umri wa takriban miaka 62 walifanyiwa utafiti na ikagunduliwa hivyo.
Ripoti hiyo kwa mujibu wa utafiti ilisema kuwa, wale ambao hawakuwa na tatizo la kupooza au shida zingine kubwa za kiafya ni wale wanaolala chini ya saa nane ikilinganishwa na wale ambao hulala saa tisa.
Hatari ya kupooza ilionekana kuongezeka kwa asilimia 25 kwa watu ambao walipumzika kwa zaidi ya dakika 90 mchana mara kwa mara, ikilinganishwa na waliopumzika kwa saa isiyozidi moja au ambao hawakulala usiku.
Pia ilibainika kuwa, wale ambao hulala kwa muda mrefu usiku na kulala muda mrefu wakati wa mchana wana uwezekano wa 85% wa kupatwa na hali ya kupooza mwili.
Wakati utafiti huo ukifanywa, watu walichunguzwa kwa muda wa miaka sita na 1557 kati yao walipooza kwenye harakati za kuchunguzwa.
Kwa kawaida mtu mzima mwenye umri wa kati ya miaka 18-64 anahitaji saa 7-9 za kuala kila usiku, Wakfu wa Kitaifa wa Usingizi unasema.
Kwa hivyo ni bora kuzingatia kwa makini ripoti hii ambayo ni muhimu na itakayokufaa kipindi hiki ili kikimalizika usijikute na maradhi ambayo hukujua chanzo chake.