MRADI wa Elimu Jumuishi chini ya kanisa la FPCT unakusudia kujenga kituo cha kuchunguza na kuwabaini watu wenye ulemavu tofauti na magonjwa mengine ili kusaidia kupata tiba na huduma zinazolingana na matatizo yao.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa wadhibiti ubora wa elimu kutoka wilaya za Dodoma na Bahi mkoani Dodoma, Mratibu wa Mradi wa Elimu Jumuishi, Jane Mdigange, alisema mazungumzo yanaendeleje baina yao na Ofisi ya Rais, Tamisemi ili kuanzisha kituo hicho katika Shule ya Msingi Nkuhungu iliyopo Dodoma.
Alisema kwa sasa Mradi wa Elimu Jumuishi unavyo vituo viwili vya kusaidia kuwabaini watu wenye ulemavu nchini katika mikoa ya Rukwa na Katavi ambavyo vimekuwa msaada mkubwa katika kuwabaini watoto wenye ulemavu na wengine wenye maradhi mengine.
"Tangu vituo hivyo viwili vilipoanza mwaka 2018/19, vimefanya kazi kubwa ya utambuzi wa watu wenye ulemavu zaidi ya 300 wanaojulikana bayana na watu wenye maradhi mengine yanayoweza kutibika," alisema.
Alisema kituo hicho kitakachokuwa na wataalamu waliobobea kitasaidia kubaini na kuwatambua watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu ili kupata huduma stahiki kwa wagonjwa kupewa rufaa kwenda kutibiwa.
Kituo hicho kitakachotumia darasa moja la shule hiyo litakaloboreshwa na kuweka vifaa vya kisasa vya kuchunguza, kitasaidia kutoa elimu kwa watumishi mbalimbali wakiwemo wakurugenzi, madiwani na watendaji wengine ili kujua haki mbalimbali za watu wenye ulemavu ikiwemo elimu jumuishi.
Aidha, kitakuwa kituo cha kupokea watu wenye ulemavu au wagonjwa kutoka katika maeneo mengine mkoani Dodoma ili kuwapa huduma za utambuzi na kuwahudumia walengwa.
Alisema msisitizo mkubwa ni kuwahimiza watendaji wa maeneo hayo kuwapa elimu jumuishi na wanafunzi wengine, badala ya kuwabagua na kuwapa elimu maalumu hali inayoendelea kuwadumaza.
Kwa mujibu wa Mdigange, lengo la kuanzisha vituo hivyo ni kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanasoma pamoja na watoto wengine kadiri ya Sheria ya Watu wenye Ulemavu Namba 9 ya Mwaka 2010.
“Lengo ni kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata elimu pamoja na wenzao bila kuwapa elimu maalumu inayowatenga na kuwafanya wakose nafuu na kushindwa kusoma na wenzao,” alisema Mdigange.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wadhibiti ubora wa elimu katika shule kutoka Bahi na Dodoma walisema, watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawasaidia watoto wenye ulemavu kusoma pamoja na watoto wengine kupitia mpango huo wa elimu jumuishi.