Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Epuka tabia hizi ili usipate corona

99139 Corona+pic Epuka tabia hizi ili usipate corona

Mon, 16 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watanzania wanajulikana kuwa na utamaduni wa kukaa pamoja na kujadiliana mambo. Ni watu wenye ukaribu, utamaduni na imani ya kuishi kwa kushirikiana.

Lakini sasa tabia na utamaduhuo vitalazimika kubadilishwa na mazingira, kwa kuzingatia tishio la maambukizi ya virusi vya corona. Ugonjwa huo sasa umethibitika kuingia katika nchi jirani za Kenya, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Nyingine za karibu ni Sudan na Ethiopia.

Tabia na tamaduni za mawasiliano ya Watanzania vitalazimika kubadilika kwani tabia za kushikana mikono wakati wa kusalimiana, kushika maiti, kudharau ugonjwa wa mafua na shughuli zote zinazohusisha mikusanyiko, ni mambo yanayotajwa na wataalamu kuwa yanachangia maambukizi ya virusi vya corona.

Mwanasaikolojia katika kitengo cha elimu cha Hospitali ya Aga Khan, Justus August anasema kuna haja ya kutoa mafunzo kuhusu ugonjwa huo.

“Watu watabadilisha utaratibu wa kusalimiana kama wataeleweshwa kuhusu ugonjwa huo,” alisema August.

Kaimu mkuu wa kitengo cha sayansi ya tabia na maadili katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki, Nadia Ahmed alisema njia rahisi ya kubadilisha tabia ni kutoa elimu, kuwaelimisha watu dalili za awali za ugonjwa wa corona, unavyoenea na taarifa nyingine muhimu.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Hiyo itasaidia kubadilisha tabia na baada ya hapo itakuwa rahisi kuwaeleza njia za kujikinga,” alisema.

Aliongeza kuwa mabadiliko ya tabia za kusalimia yanawezekana, lakini yatachukua muda kwa sababu kushikana mikono ni sehemu ya salamu. Hata hivyo, alisema muhimu ni kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile alisema, “Kwa sababu hakuna hata mgonjwa aliyeripotiwa kuugua ugonjwa huo, tunatahadharisha ili kuondoa hofu miongoni mwa wananchi.”

“Tumeanza kutoa elimu ya umuhimu wa kunawa mikono kwa kutumia taulo safi, kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima na jinsi ya kuwatambua watu wenye maambukizi ya ugonjwa wa corona,” alisema.

Alisema Serikali imekuja na mikakati mbalimbali ambayo ni pamoja na kupita kwenye skana katika viwanja vyote vya ndege na kwamba zina uwezo wa kuchunguza watu 100 ndani ya dakika 10 na kubaini mtu mwenye dalili za homa.

Alifafanua kuwa taulo za kusafisha mikono zimewekwa katika viwanja vya ndege kwa ajili ya watumiaji wa viwanja hivyo na kwamba wanazitumia kabla ya kuondoka katika maeneo hayo.

Alisema pia kipo chumba maalumu ambacho kama mtu atagundulika kuwa na maambukizi atawekwa kwa ajili ya matibabu ya awali, kabla ya kupelekwa hospitali ya karantini. Alisema yapo magari maalumu ya wagonjwa katika viwanja vya ndege.

Kuhusu usafiri wa umma ambao kwa kawaida huwa na msongamano wa abiria, Dk Ndugulile alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia kwa sababu ugonjwa huo haupo.

Hata hivyo, Mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Abel Kinyondo alisema upatikanaji wa vifaa vya kujikingia kama maski na taulo za kujisafishia utakumbwa na vikwazo vya kiuchumi kutokana na upatikanaji wake na kwamba gharama zake zitawakwaza Watanzania.

Alisema ugonjwa huo ukizuka Tanzania utaibua tatizo kubwa la kiuchumi, akitoa mfano wa nchi zilizoendelea kama Uingereza, China na Marekani ambazo licha ya uwezo wake kiuchumi zilikwazwa na gharama za vifaa vinavyohitajika.

“Wakati tukiwa bado tunahangaika na magonjwa kama kichocho ambao nchi nyingine zilishasahau, kitu cha kuomba asije akatokea mtu anayeumwa ugonjwa huo, lakini kama ikitokea hatua za haraka inabidi zichukuliwe ili usisambae,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli juzi alitoa wito wa kutolewa kwa elimu ya ugonjwa huo uliosababisha vifo vya maelfu ya watu duniani. Alivitaka vyombo vya habari kutoa elimu kwa umma akisema wahariri wa magazeti wanapaswa kuweka hata mistari miwili ya tahadhari kwenye magazeti yao.

Kwa upande wa televisheni alisema kila kabla ya taarifa za habari kuwepo na maelezo ya athari za ugonjwa huo ambao Shirika la Afya Duniani (WHO) limeshautangaza kuwa ni janga duniani.

“Ni wakati wa watu kusikiliza tahadhari zinazotolewa,” alisema juzi jijini Dar es Salaama wakati akizindua karakana ya jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) uliofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani.

Chanzo: mwananchi.co.tz