Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Elimu, lishe na tatizo la vichwa vikubwa

483aa1a1a03986fbc42c418e692c586f Elimu, lishe na tatizo la vichwa vikubwa

Thu, 17 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WATANZANIA wengi tukisikia neno 'utapiamlo', tunapata picha ya mtu, hususani mtoto aliyekonda kutokana na upungufu wa lishe.

Ni wachache wanaohusisha mtoto kuzaliwa na kichwa kikubwa au mgongo wazi na utapiamlo kwa maana ya kwamba mjamzito alikuwa na upungufu wa madini na vitamini ya foliki mwilini mwake ndio maana akazaa mtoto wa aina hiyo.

Kadhalika, wengi hatuhusishi ugonjwa wa kuvimba shingo (goita), mtoto kudumaa mwili na akili, uoni hafifu, upungufu wa damu (anemia) na kwamba hata mtu kuwa na uzito uliozidi (kitambi), hususani kwa watu wazima, ni matatizo ya utapiamlo pia.

Kuna kampeni moja iliwahi kuendeshwa miaka michache iliyopita,wananchi wakawa wanatangaziwa kwenda kuwaona madaktari wanaotibu maradhi ya watoto waliozaliwa na vichwa vikubwa au migongo wazi.

Madaktari hao wakapiga kambi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kutoa tiba bure.

Hatua hiyo ilikuwa ni njema sana kwa madaktari wetu kuchukua hatua kutibu matatizo hayo hasa kwa kuzingatia kwamba yanatibika.

Tatizo lingine ni ukweli kwamba kuna uhaba wa madaktari bingwa wa magonjwa hayo nchini kwani wakati ule ilisemekana kwamba hawafiki 15 nchi nizma.

Kampeni hiyo ambayo sina hakika kama imerudia tena iliandaliwa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili (MOI) kwa udhamini wa GSM Foundation.

Ingawa madaktari hao walikuwa wakitoa tiba hiyo bure kutokana na udhamini wa GSM Foundation, ilielezwa wakati ule kwamba gharama za upasuaji kwa mtoto mmoja mwenye kichwa kikubwa au aliyezaliwa akiwa na mgongo wazi ni Sh 700,000.

Ni vyema jamii ikaelewa pia kwamba suala la elimu ni muhimu zaidi hasa kwa mama anayejiandaa kubeba ujauzito ale nini, wakati wote wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua kwani anamwepusha mwanawe na ugonjwa huo au kulipia hayo malaki ya pesa mtoto atakapohitaji kufanyiwa upasuaji.

Pia mama huyu ajue ni nini hasa mtoto wake anapaswa kula baada ya kujifungua.

Wakati ule ilielezwa kwamba madaktari waliokuwa kambini walikuwa pia wanatoa elimu, lakini hiyo ilimaanisha kwamba walionufaika na elimu hiyo ni wale tu waliofika kwenye kambi hizo.

Kama ndivyo, watanzania wengi bado wako gizani na hivyo watoto wenye matatizo hayo yanayotokana na utapiamlo wataendelea kuzaliwa kila mwaka.

Takwimu zinaonesha kuwa watoto zaidi ya 4,000 wanazaliwa na vichwa vikubwa au migongo wazi nchini mwetu kila mwaka lakini wanaokwenda hospitalini kupatiwa matibabu hawazidi 400!

Imani iliyopo ni kwamba, kwa vile matatizo hayo ya vichwa vikubwa na migongo wazi pamoja na mengine yaliyoorodheshwa mwanzo wa makala haya yanatokana na kushindwa kutumia lishe inayotakiwa, elimu ndio jambo la muhimu zaidi katika kukomesha maradhi haya kwani hata wahenga wanasema 'kinga ni bora kuliko tiba'.

Kwa mujibu wa Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), upungufu wa chakula (utapiamlo) unaweza kuwa ni wa protini na wanga. Upungufu pia unaweza kuwa wa virutubisho vya vitamini na madini na pia, kama ilivyodokezwa hapo juu; utapiamlo unaweza kuwa unatokana na unene kupita kiasi na hapa ni kula zaidi ya kile mwili inahitaji.

Kwa mujibu wa Panita, upungufu wa virutubisho vya vitamini na madini ndiyo unaoathiri zaidi sehemu kubwa ya jamii na kwamba waathirika wakubwa ni watoto walio katika umri wa chini ya miaka mitano na wanawake walio katika umri wa uzazi.

Kwa vile mwili wa binadamu hauna uwezo wa kutengeneza virutubisho vinavyotakiwa, chanzo kikubwa ni kutoka kwenye chakula.

Panita wanasema ukosefu wa virutubisho hivi mwilini husababisha njaa iliyofichika na huchangia kwa kiwango kikubwa katika kusababisha magonjwa na vifo, hususan kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano na akina mama walio katika umri wa kuzaa.

Vitamini na madini hufanya kazi mbalimbali mwilini kama vile kusaidia kuupatia mwili nguvu na joto, kuujenga na kuulinda dhidi ya magonjwa mbali mbali.

Upungufu wa vitamini na madini katika mwili huchangia kwa kiasi kikubwa katika maradhi ya mara kwa mara kutokana na kupungua kwa kinga ya mwili pamoja na vifo, hasa kwa watoto chini ya miaka mitano.

Kingine, kwa mujibu wa Panita ni vifo vya akina mama wakati wanapojifungua kwa kukosa damu ya kutosha kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha madini chuma mwilini, kupungua uwezo wa watoto kujifunza na kuelewa shuleni au kushuka kwa elimu.

Upungufu huo pia huwa sababu ya kupungua kwa tija au uzalishaji kwa watu wazima hasa wakiwa na upungufu wa damu kwa kuwa na kiwango kidogo cha madini chuma katika miili yao. Inaweza pia kuwa sababu ya kutokuona vizuri kwenye mwanga hafifu na hata kupata upofu kutokana na ukosefu wa vitamini A.

Athari nyingine ambayo ndio makala haya yameiangalia zaidi ni baadhi ya watoto kuzaliwa wakiwa na mgongo wazi inayochangiwa na upungufu wa vitamini ya foliki.

Kama ilivyodokezwa hapo juu, akina mama wanapaswa kupata lishe bora, hususani vyakula vyenye alkali nyingi kama vile mboga na matunda ambavyo vinaaminika kuwa na madini mengi pamoja na vitamini, ikiwemo foliki kuliko kula vyakula ambavyo vikifika tumboni huwa tindikali (acid).

Utafiti unaonesha kwamba jamii ya wafugaji huandamwa sana na tatizo la kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi kutokana na kula sana nyama na maziwa huku ulaji wa matunda na mboga ukiwa hafifu sana.

Panita wanatuhimiza kutumia vizuri vyakula vinavyopatikana kiurahisi katika mazingira yetu ili kupunguza gharama na kuhakikisha vyakula hivyo vinakuwa katika makundi yote ya lishe.

Makundi hayo ni kama vyakula vya wanga kutokana na nafaka zisizokobolewa (mahindi, mtama, uwele, ulezi, ngano), vyakula vya protini (maziwa, maharage, mbaazi, nyama), mafuta (karanga, ufuta), vitamini (mboga zote na matunda) na madini ambayo yanapatikana zaidi kwenye mboga.

Elimu hizi zinatakiwa kutolewa sana kwa wananchi kwani inaelezwa kwamba hata mikoa inayoaminika kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula, inaandamwa na utapiamlo na hilo linatokana na jamii husika kushindwa kuzingatia kula chakula kilicho katika makundi hayo hapo juu, kama ilivyo pia kwa jamii za wafugaji.

Kinachotakiwa kufanywa na serikali kwa mujibu wa Panita ni kuongeza bajeti inayoelekezwa katika kuboresha hali ya lishe nchini na bila shaka itasaidia pia suala zima la elimu.

La muhimu wakati makala haya yakifika mwisho ni elimu ya kuhakikisha wajawazito na watoto wanapata lishe inayotakiwa.

Chanzo: habarileo.co.tz