Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EAC yatoa tahadhari ya Ebola

Tue, 23 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetoa tahadhari kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kushirikiana katika kupeana taarifa za kukabiliana na ugonjwa hatari wa mlipuko wa Ebola ambao umeibuka tena katika eneo la Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretariati ya EAC iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano kwa Umma, Richard Owora jana Jumatatu, Julai 22, 2019, imesema tahadhari hiyo ni muhimu kwa sababu Jimbo la Ituri lipo umbali wa kilometa 70 mpakani na nchi Sudani Kusini.

Nchi hiyo ni mwanachama wa EAC na ipo jirani zaidi na nchi ya Uganda.

“Matukio ya mlipuko wa Ebola katika nchi za EAC yaligundulika kwa mara ya kwanza kwa wagonjwa watatu nchini Uganda Juni mwaka huu, na Serikali ya Uganda ilijitahidi kuudhibiti kwa wakati,” imesema na kuongeza

“Kutokana na mwingiliano mkubwa wa kibiashara kati ya nchi za EAC na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, upo uwezekano mkubwa wa ugonjwa huu kusambaa zaidi kutokana na mwingiliano wa watu na bidhaa mbalimbali,” amesema Owora.

Amesema kulingana na tangazo kwa umma lililotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kuhusu hali ya tahadhari inayopasa kuchukuliwa hatua za dharula, Kaimu Mkuu wa Idara ya Afya wa EAC, Dk Michael Katende ametoa wito kwa nchi wanachama kushirikisha jamii zinazoishi maeneo ya mipakani na wafanyabiashara kuwapa ujumbe wa tahadhari.

Chanzo: mwananchi.co.tz