Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dozi milioni 1 za chanjo zawasili

A0cc89b2690268ade451f14683b83fd1 Dozi milioni 1 za chanjo zawasili

Mon, 26 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kupelekwa kwanza kwa Mkemia Mkuu Kipaumbele mikoa 8, wazee, madaktari, wenye magonjwa sugu

SERIKALI imepokea dozi milioni moja za chanjo aina ya Johnson & Johnson kwa ajili ya ugonjwa wa corona.

Chanjo hiyo iliyopokelewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima, kabla ya kuanza kutumika, itapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuchunguzwa na kisha kuanza kutolewa bure kwa makundi maalumu.

Akizungumza baada ya kupokea chanjo hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dk Gwajima alisema chanjo hiyo ni sehemu ya utekelezwaji wa agizo la Rais Samia Suluhu la kutaka iwepo mkakati wa kukabili ugonjwa wa corona kama nchi nyingine zinavyofanya kwa kuwa Tanzania si kisiwa.

Miongoni mwa waliohudhuria hafla ya kupokea chanjo hizo ni Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright, wawakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef).

Mkemia kuzikagua Waziri Gwajima alisema katika kuhakikisha kuwa chanjo hizo ni salama, zinapelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kupimwa. Alisema zitaanza kutumika muda si mrefu baada ya kukaguliwa.

Alifafanua kwamba, uamuzi wa kuziwasilisha ofisi ya mkemia pia ni utekelezwaji wa ushauri aliowahi kuutoa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, Januari 27 mwaka huu kuwa wizara ijiridhishe kwanza kabla ya kuanza matumizi ya chanjo za corona.

“Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wananufaika na chanjo kama njia mojawapo ya kukabiliana na corona na kwa kuanzia leo (jana), tumepokea dozi zaidi ya milioni moja za chanjo aina ya Johnson & Johnson,” alisema.

Alisisitiza: “Lakini si kwamba ndio moja kwa moja leo tunaanza kuchanja, hapana leo tumeziingiza nchini na kisha mkemia akishamaliza kazi yake na ndipo itaanza kutumiwa kwa makundi maalumu kwanza kabla ya kuingia kwa kila Mtanzania anayetaka.”

Alisema: “Ifahamike kuwa, maabara yetu ya Mkemia Mkuu ni kati ya maabara bora kabisa hivyo hakuna wasiwasi kuhusu uwezo wake katika kupima ubora wa chanjo hii na uchunguzi ukikamilika, itaanza kwa makundi maalumu kwanza.”

Makundi maalumu Gwajima alitaja kundi la kwanza kunufaika na chanjo hiyo ya bure litakuwa ni wauguzi wa sekta ya afya, kisha wazee kuanzia umri wa miaka 50 na watu wanaougua magonjwa sugu.

Alisema serikali imeamua kuanza na makundi hayo, hususani madaktari kwa kuwa ni la kwanza kukutana na wagonjwa wa corona wakati wa kuwahudumia hospitalini.

Kwa upande wa wazee, alisema uamuzi wa serikali umezingatia kwamba wamekuwa wakikumbana na magonjwa nyemelezi hivyo serikali imeona ni vema kuwawahi zaidi kwa kuwapatia chanjo.

Mikoa ya kipaumbele Alitaja mikoa itakayoanza kupewa huduma hiyo ni Mwanza, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Kigoma, Singida, Dodoma, Iringa na Mtwara.

Kwa mujibu wa Gwajima, wakati uchanjwaji ukiendelea katika mikoa hiyo, dozi nyingine itakuwa imeshaagizwa.

Alisema chanjo hizo zitakuwa zikipatikana katika vituo vya afya nchini pamoja na vituo maalumu vitakavyotambulishwa kuanzia ngazi za kata, wilaya na mikoa.

Wapotoshaji waonywa Waziri Gwajima aliwaondolea hofu wananchi wanaodhani kwamba chanjo hiyo ina madhara kwa kuwataka wafahamu kuwa madhara kwa chanjo yoyote hutokana na mwili wa mtu.

Alifafanua kwamba, hata chanjo ya surua wapo watoto wanaochanjwa, lakini wanajikuta wakiumwa na kulazimika kuchanjwa tena.

“Najua mimi nawashangaa sana hawa madaktari hewa yaani hawa ambao wapo mitandaoni na hata hawajulikani anuani zao, sasa hao ndio waongo wa kwanza katika kuwatia hofu watu kuhusiana na chanjo hizi,” alisema.

Akaendelea: “Ifahamike kuwa Tanzania ipo makini katika chanjo na imekuwa ikisifiwa kila kona ya dunia kutokana na kuwa imeanza kutumia chanjo muda mrefu na hivyo tuna uzoefu nazo, ndio maana hata hizi zinapimwa kwanza na mkemia.”

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alisema msaada huo wa chanjo kutoka Marekani, umetokana na uhusiano mzuri na nchi hiyo.

Aliwataka Watanzania wasiwe na wasiwasi kuhusu matumizi ya chanjo hiyo iliyotolewa na nchi hiyo rafiki.

Marekani yatia neno Balozi wa Marekani nchini, Wright alisema msaada huo wa chanjo ni sehemu ya utekelezwaji wa Sera ya Marekani katika kusaidia Sekta ya Afya kwa Tanzania, sera ambayo Marekani imekuwa ikiitekeleza kwa muda mrefu.

“Wananchi msiwe na wasiwasi kuhusiana na hizi chanjo kwanza ifahamike kuwa inatoka kwa marafiki zetu na pia kama ni kuchanjwa, hata mimi nimechanjwa tangu mtoto na hadi leo nipo hai, kwa hiyo hakuna haja ya kuogopa chanjo na tuwashukuru Marekani kwa kutusaidia chanjo hii; tena inatolewa bure,” alisema.

Alisema tangu corona iingie nchini, Serikali ya Marekani imetoa zaidi ya Dola za Marekani milioni 26 kama msaada wa moja kwa moja kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema pia msaada huo ni sehemu ya utekelezwaji wa sera ya urafiki kati ya Tanzania na Marekani.

Kwa mujibu wa Balozi Wright, msaada huo ni sehemu ya ahadi ya Marekani ya kuanza kutoa angalau dozi milioni 25 kwa Afrika, kati ya dozi milioni 80 zilizoahidiwa kwa barani.

Alisema Marekani inashirikiana kwa karibu na Umoja wa Afrika na Kituo cha Afrika Kudhibiti Maradhi (Afica CDC) hasa katika kuhakikisha chanjo inagawiwa kila nchi kupitia mpango wa usambazaji chanjo kimataifa wa COVAX.

WHO yapongeza Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini, Dk Tigest Mengestu alibainisha kuwa, hatua ya Serikali ya Tanzania kukubali na kuagiza chanjo ni ya kupongezwa kwa kuwa ugonjwa umekuwa ukigharimu maisha ya watu sehemu mbalimbali duniani.

Alisema, kwa takwimu za hivi karibuni watu milioni 191 wameugua na milioni nne wamefariki huku kwa Afrika, watu milioni 4.5 wameugua na 10,8000 wamefariki dunia.

Onyo uingizaji holela Chanjo hiyo ya bure imewasili jana nchini ikiwa ni siku chache tangu serikali itoe onyo kwa wafanyabiashara pamoja na taasisi zenye nia ya kuingiza chanjo, ikizitaka zizingatie masharti na kwamba haitavumilia uingizwaji holela.

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi, alisema serikali imeagiza aina nane za chanjo zitakazoingia baada ya miezi mitatu hadi minne.

Tofauti ya chanjo iliyowasili jana ambayo ni ya bure kwa msaada wa Marekani kupitia mpango huo wa Covax, aina nyingine zitakazoruhusiwa zitatoa nafasi kwa Watanzania kuchagua wanayoitaka.

Chanzo: www.habarileo.co.tz