Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Ndugulile azionya hospitali zinazozuia maiti kwa madeni

13241 Pic+ndugulile TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali mbili kubwa nchini; ile ya Taifa ya Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam na ya Mloganzila ya mkoani Pwani zimetajwa kuwa ndizo zinazoongoza kuzuia ndugu kuchukua maiti kwa sababu ya madeni ya gharama za matibabu.

Licha ya kutajwa, zimetakiwa pamoja na hospitali zote nchini kuacha utaratibu huo kuanzia sasa kwa kujipanga mapema kuhakikisha kuwa kila kitu kinamalizika vizuri na mapema kati yao na wafiwa.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndungulile ndiye aliyezionya hospitali hizo juzi, katika hafla ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulipokabidhiwa cheti cha ubora wa kimataifa (ISO) jijini Dar es Salaam.

Dk Ndugulile alisema, “siyo jukumu la Serikali kuzika, maana kung’ang’ania mwili wakati ndugu wanahitaji kumhifadhi ndugu yao inaleta maana gani?” alihoji.

“Nimewasisitiza wajipange vizuri kuepuka mgogoro na wananchi.”

Awali, naibu waziri alisema endapo kila Mtanzania atakuwa na bima ya afya itasaidia kupunguza gharama za matibabu na kesi za miili kuzuiwa hospitali pindi ndugu wanaposhindwa kulipa madeni.

“Kesi hizo nakutana nazo zaidi Mloganzila na Muhimbili na baadhi ya ndugu wakilazimika kuwaondoa wagonjwa wao hospitalini kabla ya kumaliza matibabu kwa kuhofia gharama zitakuwa kubwa na watashindwa kuzilipa.”

Akifafanua zaidi kuhusu maiti kuzuiwa hospitali, Dk Ndungulile alisema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakidai kukataliwa kuchukua miili ya ndugu zao hadi walipe gharama wanazodaiwa.

“Nimewaagiza ni vyema wakajipangia utaratibu mzuri wa kukusanya gharama hizo za malipo badala ya kuacha matatizo hayo yasababishe hadi kuzuiwa miili, hivyo kuwaongeza majonzi na usumbufu kwa ndugu waliofiwa,” alisema.

Alisema kuwa anaamini uongozi wa hospitali hizo ukiwa makini katika kufuatilia malipo ikiwamo kutoa maelezo mazuri kwa wale wanaostahili kupata msamaha wa gharama za matibabu hakutakiwa na malalamiko.

Naibu waziri huyo alisema Serikali inawajibika kuhakikisha wananchi wanapata matibabu ya uhakika na pale inapotokea ndugu kushindwa kulipia gharama kwa sababu mbalimbali ni vyema viongozi wa hospitali husika wakaangalia njia bora ya kudai.

Mapema, Dk Ndugulile ambaye pia ni mbunge wa Kigamboni alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari Agosti 21, akizungumzia jambo hilo akiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kigamboni.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano cha Hospitali ya Mloganzila, Hellen Mtui alisema inabidi uongozi wa hospitali uangalie namna ya kuifanyia kazi kauli ya naibu waziri.

“Inabidi tukae na kujadili kuona itakuwaje, hapa mambo mengi hutokea, wapo ambao wanashindwa kulipa gharama za matibabu na ndugu anapofariki, basi tunakaa na kuangalia wakiweza wanalipa kidogokidogo, wakishindwa wanalipa walichonacho,” alisema.

Uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili haupatikana kuzungumzia suala hilo.

Chanzo: mwananchi.co.tz