Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Ndugulile ataja sababu sekta ya afya Wilaya ya Tunduru kuimarika

Wed, 16 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali mbili na vituo vya afya 14 vimejengwa Wilaya ya Tunduru katika kipindi cha miaka minne huku hali ya upatikanaji wa dawa ikiongezeka kutoka asilimia 60 mpaka 92.5.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Oktoba 16, 2019 na naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile katika kijiji cha Chiola wilayani Tunduru Mkoa wa Lindi katika ziara ya Rais wa Tanzania,  John Magufuli.

“Tunampongeza Rais kwa kuja kufanya ziara, kutembelea wananchi na kufuatilia maendeleo ambayo Serikali yake imekuwa ikifanya. Sekta ya afya tumepiga hatua kubwa ikilinganishwa na kipindi cha nyuma,  wananchi wana afya njema na huduma imeboreshwa hasa za afya zinazidi kuwasogelea wananchi,” amesema.

Dk Ndugulile amesema katika kipindi cha miaka minne Serikali imefanikiwa kujenga hospitali mbili za wilaya, vituo ya afya 14.

“Tumeboresha vituo vya afya na zahanati pia lakini hali ya upatikanaji wa dawa ilikuwa chini ya asilimia 60 kwa sasa ni zaidi ya 92.5,” amesema Dk Ndugulile.

Naye naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Rais amefanya ziara hiyo wakati muafaka ambao zao la korosho lipo katika msimu mpya.

Pia Soma

Advertisement
Amesema zao hilo ni kati ya mazao yanayookoa wananchi wa eneo hilo na Serikali imeweza kufanya uamuzi  makini wa kusaidia wananchi kupitia zao hilo na matunda yameonekana.

“Ziara hii na sisi tunapita na kupewa maagizo tutakayoyafanyia kazi, kati ya maagizo aliyoyatoa zao la korosho litanunuliwa moja kwa moja na wafanyabiashara na tutaweka utaratibu wa wazi kwa maana awali wale ambao hawakuwa shambani ndiyo walionufaika zaidi ikilinganishwa na wakulima wenyewe,” amesema Bashe.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Esha Mkukumia amesema, “Rais ametutembelea aliyekuwa na dukuduku aseme na kumpongeza watu tulikuwa na hali mbaya hasa katika korosho mwaka huu tumepata hela kwa kweli tunaomba usimamizi huu uendelee.”

Chanzo: mwananchi.co.tz