Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Ndugulile aonya utoaji wa dawa kwa mifugo, asema unaathiri walaji

29919 Ndugulile+pic TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tatizo la masalia ya dawa kwenye nyama, maziwa na mayai limetajwa kuathiri walaji kutokana na baadhi ya wafugaji kutozingatia matumizi ya kutoa dawa kwa mifugo yao.

Kutokana na tatizo hilo Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile ameziagiza mamlaka husika kuongeza kasi ya uchunguzi ili kulidhibiti.

Akizungumza leo Jumatatu Desemba 3, 2018 wakati akifungua mafunzo ya kikanda ya Afrika juu ya masalia ya dawa katika bidhaa za mifugo, Dk Ndugulile amesema jitihada zinahitajika kutokomeza tatizo hilo kabla halijaleta athari kubwa zaidi.

"Mnyama akila dawa, kesho yake akachinjwa zile dawa zinahama kutoka kwa mnyama na kwenda kwa binadamu na zinapelekea kuleta usugu na kupata reaction (aleji) kwa walaji," amesema.

Ameitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuongeza uwezo wa kimaabara katika kuchunguza bidhaa zote zinazoingizwa sokoni pamoja na zile zinazoingizwa toka nje ya nchi ili ziwe na viwango stahiki.

Amesema mkakati uliopo ni kuwalinda walaji kwa kuhakikisha matumizi ya dawa yanadhibitiwa ikiwa ni pamoja na kuzuia uuzaji wa dawa za mifugo kiholela.

"Ni lazima tuhakikishe kwamba tuna maduka mahususi yanayouza dawa na kemikali na kuhakikisha mnunuaji anapewa elimu ya matumizi ya hizi dawa," amesema.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Adam Fimbo amesema tatizo hilo limeongeza usugu wa dawa kwa baadhi ya watumiaji wa bidhaa hizo huku wengine wakipata matatizo ya kiafya bila kujua nini chanzo chake.

"Tunaona kuna usugu wa dawa hasa 'antibiotics' ambao unafanya watu wakipewa dawa hawaponi na masuala ya reaction ya dawa  kumbe alikula nyama ambayo ina masalia ya dawa anakuwa hajui," amesema.

Amesema wao wamejipanga kuanza kufanya uchunguzi wa bidhaa hizo kwenye masoko mbalimbali pamoja na zile zinazoingia kutoka nje ya nchi  ili ziweze kuwa na ubora unaohitajika.

Mafunzo hayo yamehusisha nchi 22 za Afrika kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuongeza ushirikiano katika masuala ya udhibiti wa dawa.



Chanzo: mwananchi.co.tz