Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Ndugulile- Lugha nyepesi italeta matokeo chanya tafiti za kisayansi nchini

Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi na Afya Muhimbili (Muhas) kimetakiwa kutumia tafiti zinazofanywa chuoni hapo katika kuisaidia Serikali kutimiza majukumu yake kwa kuwasilisha tamko la kisera mara baada ya kuzitangaza.

Hayo yamesemwa leo Septemba 26, 2018 na naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alipokuwa akizindua kongamano linalohusisha zaidi ya tafiti 21 za watu walioathirika na dawa za kulevya zilizofanywa na chuo hicho.

Amekitaka chuo hicho kutoa tafiti zao kwa lugha nyepesi huku wakiishirikisha Serikali ili kuendana na kipaumbele kama taifa na kuhakikisha wanatengeneza matamko kisera.

“Tunachoangalia ni namna gani tunaweza kuwasaidia watu wanaotumia dawa za kulevya, mwelekeo tulionao awamu hii ya tano ni kutengeneza sera, uamuzi na uendeshaji unaozingatia takwimu zilizopo na tunawaangalia ninyi kama wazalishaji wakubwa wa takwimu,” amesema Dk Ndugulile.

Amesema Serikali inategemea takwimu kutoka kwa wanasayansi watafiti lakini kumekuwa na upungufu mkubwa katika hilo.

“Tangu niwe Naibu Waziri yapata miezi 10 sasa, sijaona tafiti zenu mkizitengeneza kwa lugha nyepesi ili imsaidie yule mwananchi wa kawaida, haina maana sana kama tafiti zenu zikachapishwa katika majarida makubwa duniani lakini usiisaidie nchi.”

“Kuanzisha utoaji wa tafiti hizi ninaona ni mwanzo mzuri, nitoe rai kwa vyuo vingine vikuu kuwa chimbuko la tafiti na takwimu ili kuboresha sera,” amesema.

“Tafiti zenu ziwe maeneo ya kipaumbele na sisi tufanyie kazi msifanye tafiti kwa sababu mmepata fedha, bali zitakazosaidia jamii, tunatarajia mtafanya tafiti zenye kuleta maana na kuisaidia Serikali kiutendaji.”

Hata hivyo, aliishukuru Muhas kwa kushirikiana na Hospitali ya Muhimbili katika kutibu waathirika wa dawa za kulevya na kwamba nchi inahitaji tafiti zaidi ili kuondokana na tiba za sasa na kuja na tiba za juu zaidi ili waathirika kumaliza tiba za methadone kwa uharaka zaidi.

“Mahitaji bado ni makubwa zaidi, tunahitaji huduma hii ifike mpaka ngazi za mikoa ili kusaidia waathirika tafiti zenu ni muhimu kwa maendeleo ya nchi ila nasisitiza mzitoe katika lugha nyepesi,” amesema Dk Ndugulile.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema Muhas imepokea maoni ya Wizara ya Afya na kuahidi kuyafanyia kazi.

Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Andrea Pembe amesema, “Tumepokea na tupo katika mchakato wa kutengeneza tamko la kisera kwa ajili ya hizi tafiti zaidi ya 21 zinazohusu watu walioathirika na dawa za kulevya.”

Chanzo: mwananchi.co.tz