Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mwele alivyoacha alama sekta ya afya

Mwele Who Mwele Ntuli Malecela

Sun, 13 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele katika Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Mwele Malecela amefariki dunia juzi wakati akipatiwa matibabu mjini Geneva Uswisi.

Kifo cha Dk Mwele ambaye kabla ya nafasi hiyo alikuwa Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Espen), wa WHO, Kanda ya Afrika, kimepokelewa kwa mshtuko ndani na nje ya Tanzania huku viongozi na watu kadhaa mashuhuri akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan wametuma salamu za kuomboleza.

Kupitia mitandao ya kijamii ya Twitter na Instagram, Rais Samia alimsifia marehemu Dk Mwele kwa weledi na utumishi uliotukuka kwa Taifa na dunia kwa ujumla

“Nimesikitishwa sana na kifo cha Dk Mwele Malecela, mwana wa Afrika ambaye ametumikia vema Tanzania ndani na nje ya mipaka. Pole zangu zimfikie mzee John Malecela na familia yake yote wakati huu wa majonzi mazito. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amina.” alisema Rais Samia katika ujumbe wake.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu pia alielezea masikitiko yake kwa kifo cha mtaalamu huyo wa afya ya binadamu akisema si tu ni pigo kwa familia, bali pia kwa sekta ya afya Tanzania, Afrika na ulimwengu mzima.

Akizungumzia kifo cha Dk Mwele aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kabla ya kuvuliwa wadhifa huo na Rais John Magufuli Desemba 16, 2016, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Profesa Costa-Ricky Mahalu alisema Taifa na dunia imempoteza mtaalamu mbobevu na aliyetenda kwa weledi katika taaluma yake.

“Kwa kufanya kazi NIMR, Dk Mwele alijua mazingira na changamoto za sekta ya afya Tanzania na Afrika pia. Afrika ilitarajia mchango wake kukabiliana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Ameondoka mapema na pengo lake halitazinbika kirahisi,” ,” alisema Profesa Mahalu, Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia.

Milima na mabonde ya Dk Mwele

Dk Mwele ambaye ni mtoto wa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, aliondolewa NIMR, siku moja baada ya kutoa ripoti ya utafiti wa magonjwa, utafiti ambao ndani yake ilikuwemo taarifa ya kugundulika uwepo wa virusi vya ugonjwa wa Zika katika maeneo ya Morogoro, Geita na Magharibi mwa Tanzania.

Baada ya kutoa takwimu hizo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa pamoja na Dk Mwele aliitisha mkutano na waandishi wa habari kukanusha taarifa hizo kwamba ugonjwa huo bado haujaingia nchini.

Nyota kung’ara Kimataifa

Usemi wa wahenga wa chura kuongezewa mwendo pale anapopigwa teke ilijidhihirisha kwa Dk Mwele baada ya kuteuliwa na WHO kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa vituo vya kudhibiti na kuzuia magonjwa Afrika (Espen) wa shirika hilo Kanda ya Afrika. Uteuzi huo ulifanyika muda mfupi baada ya Rais Magufuli kumtoa katika nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa NIMR. Tangu kuteuliwa kwake, Dk Mwele aliongoza mradi wa Espen ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2016 hadi 2020 ukiwa na lengo la kukabiliana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwa kutoa vifaa tiba, elimu na dawa.

Magonjwa yasiyopewa kipaumbele ni pamoja na matende, mabusha, kichocho, minyoo ya tumbo na usubi.

Aprili, 2021 nyota ya Dk Mwele iliendelea kung’ara baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele katika shirika la WHO, nafasi aliyoishika hadi mauti yalipomfika juzi.

Katika nafasi hiyo mpya, alikabidhiwa jukumu la kusimamia miradi ya kupunguza magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele ambayo yapo katika nchi 149 duniani. Pia Dk Mwele aliyezaliwa Machi 26, 1963 pia aliwahi kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya urais mwaka 2015 kupitia CCM.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live