Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mollel amtaka Dk Kigwangala kurejea shule ‘upigaji nyungu’

376245c856c477ec1422d169a7a391f8.jpeg Dk Mollel amtaka Dk Kigwangala kurejea shule ‘upigaji nyungu’

Sun, 18 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NAIBU Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel amewataka wanasayansi na madaktari nchini kuendelea kufanya utafiti kupata majibu kuhusu changamoto zinazokabili nchi wakati huu wa janga la Corona.

Aidha, amemshangaa Mbunge wa Nzega Dk Hamis Kigwangala kubeza utafiti unaofanywa na wanasayansi wa nyumbani na kumtaka aache kupingana nao akimwambia utafiti unapingwa kwa utafiti na si maneno matupu.

Dk Mollel aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wafanyakazi wa hospitali mbalimbali na vituo vya afya nchini kuhusu wagonjwa wenye changamoto za damu (himofilia) nchini.

Alisema: Dk Kigwangala ni rafiki yangu na mbunge mwenzangu, siku tukikutana nitampa ofa ya kurudi shule akapate maarifa na kufundishwa utafiti ili kumuwezesha kuelewa kuwa nyungu inafanyaje kazi katika kujenga afya ya mwanadamu hususani katika mifumo ya upumuaji.

Alisema tangu serikali ya Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli hadi sasa hivi ya Rais Samia Suluhu Hassan, serikali inawaunga mkono wanasayansi wa Tanzania na pia inawapongeza kwa kuja na tiba ya kujifukiza ambayo gharama zake ni nafuu tofauti na chanjo nyingine.

“Mimi naamini sehemu ambayo tunaweza tukathibitisha hata sisi wizara ya afya umuhimu na uwezo wa nyungu na tunaweza kupata majibu sahihi kuwa nyungu ni sawa au sio sawa, ni kwa nyie muendelee kufanya tafiti zaidi ili tuweze kupata majibu sahihi,” alisema Dk Mollel.

Alisema inasikitisha kuona mtu ambaye amepitia Muhimbili na kupata maarifa ya afya katika Chuo cha Muhimbili anashindwa kuelewa hilo. “Kwa hakika anatakiwa kurudi tena shule kwa sababu elimu aliyo nayo haitoshi,” alisema.

Alisema binafsi amepata matibabu ya nyungu na kuthibitisha kuwa ni nzuri. Alimhimiza Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Maseru kuendelea kufanya kazi nchi ipate dawa ya maradhi ya corona.

Hivi karibuni Mbunge wa Nzega, Mjini Hamis Kigwangala (CCM), alikaririwa akishauri kuondolewa kwa mashine za kujifukiza zilizopo katika hospitali ya Muhimbili akidai hazina uhalisia wa kisayansi na kuagiza taifa lianze mchakato wa kuagiza chanjo kutoka nje ya nchi.

Licha ya majibu ya Naibu Waziri, Dk Mollel, vile vile MNH ilimjibu ikisema ina jukumu la msingi na dhamana ya kutoa elimu, kutibu na kufanya utafiti katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya afya hivyo inatakuwa inatimiza malengo na majukumu yake bila kuingiliwa na mtu yeyote.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha MNH, Aminiel Aligaesha, ilisema kutokana na muktadha huo, hospitali hiyo haitaondoa huduma hiyo kwa kuwa iko kwenye utekelezaji sahihi wa majukumu yake ya kitafiti kama wanavyofanya wanasayansi wengine kote duniani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz