Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk. Leyna: Madini joto shida kubwa katika lishe ya umma

LISHE Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk. Germana Leyna

Thu, 16 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jitihada kitaifa zaishia kugota 60% Ukichezea; ujauzito, ukuaji ‘umeumia’

UPUNGUFU wa madini joto imo katika katika matatizo makuu ya lishe nchini. Inashika nafasi ya tatu kwa ukubwa katika matatizo ya lishe, ikitanguliwa na upungufu wa nishati na utomwili (protoni) na upungufu wa wekundu wa damu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Chakula Tanzania (TFNC), Dk. Germana Leyna, anasema tatizo hilo linaathiri afya na maendeleo ya jamii, ikiwa ni pamoja na uzalishaji mali na uchumi.

Anasema madhara yatokanayo na upungufu wa madini joto ni mengi na yanaathiri makundi mbalimbali katika hatua za ukuaji kuanzia ujauzito, utoto, ujana na utu uzima.

“Athari hizi ni pamoja na kuharibika mimba, kuzaa mtoto mlemavu, uvimbe wa tezi ka shingo, udumavu, ulemavu na akili na mwili,” anaeleza Dk. Leyna.

Anasema mikakati ya kuzuia upungufu wa madini joto nchini, ilianza kwa kuhusisha matibabu kwa kutumia vidonge, matone na sindano za madini joto kama mkakati wa muda mfupi.

Dk. Leyna anasema kutokana na mkakati huo kuwa wa gharama kubwa na usio endelevu, mwaka 1994, mkakati wa kuweka madini joto kwenye chumvi ulianzishwa katika namna endelevu na ya kudumu.

Anasema, mkakati huo wa uwekaji madini joto kwenye chumvi huliwa na watu wengi kila siku kwa kiasi kisichotofautiana, teknolojia na vifaa vinavyotumika katika kuchanganya chumvi na madini hayo, ni rahisi chumvi iliyowekewa madini haibadiliki rangi, harufu wala ladha yake.

Anaeleza kuwa bei ya chumvi hiyo ni nafuu, ikilinganishwa na vyakula vya chumvi, vinatumiwa kama njia ya kufikishia madini joto hayo kwa mlaji.

CHUMVI INAVYOTUMIKA

Dk. Leyna anasema, takwimu kitaifa za matumizi ya chumvi yenye madini joto, yanaonyesha kaya zinazotumia chumvi hizo zimeongezeka kutoka asilimia 90 hadi 96.4.

Aidha, kaya zinazotumia chumvi yenye madini joto toshelevu zimeongezeka kutoka asilimia 47 hadi asilimia 61, ila changamoto kubwa katika mikoa inayozalisha chumvi kwa sababu kaya zinazotumia chumvi bado zipo kwa ngazi ya chini.

Daktari huyo anasema, taasisi hiyo imekuwa ikifanya mikakati ya kuhakikisha chumvi yenye madini joto toshelevu, inapatikana kwa wingi.

Anataja mikakati hiyo, ni kutoa mafunzo kwa maofisa afya na wazalishaji wa chumvi kuhusu umuhimu wa madini joto mwilini na madhara yatokanayo na upungufu wa madini, uzalishaji chumvi bora na yenye madini joto na ufuatiliaji wake.

Vilevile, anasema wanahamasisha viongozi wa kamati za ulinzi na usalama katika ngazi zote kutoa elimu ya umma kupitia vyombo vya habari na mawasiliano vilivyopo.

WAANZISHA CHAMA

Dk. Leyna anasema, wameanzisha Chama cha Wazalishaji wa Chumvi, lengo kuu likiwa ni kuwaunganisha wazalishaji chumvi na wadau wengine, ili kuwapo yzalisha chumvi bora yenye madini joto yanayojitosheleza.

Ahadi nyingine, ni kwamba wanadhamiria kuhakikisha uzalishaji wa chumvi yenye madini joto na upatikanaji madini joto kwa namna mbalimbali.

Mkakati mwingine anaoutaka ni kuwapo kwa Kamati ya Kitaifa inayoratibu mpango wa kudhibiti upungufu wa madini joto yenye uwakilishi kutoka sekta mbalimbali.

Dk. Leyna anasema, walianzisha Sheria ya Chumvi iliyopitishwa bungeni mwaka 1994, ili kusimamia na kuhakikisha kuwa chumvi yote inayozalishwa au kuingizwa nchini kwa matumizi ya binadamu na wanyama, imechanganywa na madini joto.

“Sheria hii Kuu ya Madini ya Mwaka 1979 na ile ya Chakula ya Mwaka 1978, vifungu hivi vimefanyiwa mapitio mwaka 2003 na kuwa kanuni mwaka 2010,” anaeleza Dk. Leyna.

Anasema taasisi ya Chakula na Lishe, kwa kushirikiana na wadau wa chumvi, ilisambaza mashine za kupima kiasi cha madini joto kwenye chumvi katika halmashauri zote zinazozalisha bidhaa hiyo nchini.

Mtaalamu huyo anasema wamekuwa wakiwafuatilia kila mara wazalishaji na wauzaji chumvi katika maeneo yote nchini, kupata picha halisi ya mwenendo walio nao.

“Vilevile wauzaji na wasambazaji wakubwa na wadogo walipatiwa mafunzo kuhusu umuhimu wa kuuza chumvi yenye madini joto yenye ubora katika baadhi ya halmashauri nchini," anaeleza Mkurugenzi huyo.

Dk. Leyna anasema, mwaka 2016 taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau, walifanya mapitio ya mkakati wa uongezaji wa madini joto kwenye chumvi na kubainisha changamoto zilizopo katika sekta hiyo.

Anasema tathimini ilibaini uwapo wa wazalishaji wa chumvi wengi wadogo wadogo na kati katika maeneo ambayo hawayafikii kirahisi na wanaozalisha chumvi isiyo na ubora.

Pia, kuna suala la kushindwa kuanzisha biashara zenye faida kiuchumi na matumizi ya teknolojia duni katika kuweka madini joto kwenye chumvi.

Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na tathimini hiyo, Dk. Leyna anayataja ni kuandaa miundombinu inayojumuisha wazalishaji chumvi wadogo, wa kati na wakubwa, kufanya utafiti katika sekta ya chumvi ili kupata maelezo ya kina kuhusu uandaaji miundombinu ya wazalisha chumvi nchini, ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji bora wenye madini joto.

Dk. Leyna anasema, katika kuwasaidia wazalishaji chumvi waweze kuzalisha kwa ubora yenye madini joto, mwaka 2019 taasisi kwa kushirikiana na wadau ilisambaza mashine za usalishaji wa madini joto katika baadhi ya halmashauri nchini.

Anataja baadhi ni Kilwa, Meatu na Hanang, akianisha sababu zake ni pamoja na maeneo hayo kuzalisha chumvi nyingi, lakini isiyo na madini joto.

“Ni matarajio yetu kwamba, tutatoa fursa ya kupata uelewa kuhusu masuala ya udhibiti wa tatizo la upungufu wa madini joto nchini,” anasema.

Pia, anataja kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa matumia ya chumvi yenye madini joto, ili kuepuka madhara yatokanayo na tatizo hilo.

Anasema, pia wanaelimisha jamii kuhusu uhifadhi sahihi wa chumvi yenye madini joto kwenye kaya na kuelimisha wazalishaji, wasambazaji na wauzaji kuhusu uuzaji na uhifadhi sahihi wa chumvi yenye madini joto.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live