Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Gwajima ataka mabaraza kuwachukulia hatua wasio na maadili

F9debb98acd95234a502e92e0fe381b2 Dk Gwajima ataka mabaraza kuwachukulia hatua wasio na maadili

Sat, 13 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Dorothy Gwajima ameyaagiza mabaraza na vyama vya kitaaluma kuendelea kukemea na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wanaokwenda kinyume na taaluma zao.

Alisema hayo mjini hapa wakati akifungua mkutano wa wauguzi viongozi.

“Jukumu letu kama viongozi ni kusimamia watumishi walioko chini yetu ili waweze kutoa huduma kwa wateja kwa kuzingatia maadili katika utumishi wa umma na kuepukana na matendo mabaya, niagize mabaraza na vyama vya kitaaluma kuendelea kukemea na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wanaokwenda kinyume na maadili ya taaluma yao,” alisema

Alisema suala la maadili linatakiwa kupewa kipaumbele ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi na kumekuwa na kuporomoka kwa maadili ya watumishi katika sekta ya afya.

“Tunapaswa kujiuliza maadili ya mtumishi wa umma, awe kiongozi au mtumishi wa kawaida ni nini ?Maadili yanafafanuliwa kwamba ni matendo mema kwa hiyo maadili ni viwango vya uadilifu vinavyotazamiwa na wananchi kwa mtumishi yoyote wa umma, maadili huwekwa kwa njia ya misingi,kanuni na miongozo inayotakiwa katika utumishi,” alisema.

Alisema mara nyingi wanapokea malalamiko juu ya ucheleweshaji wa utoaji huduma, upendeleo, mienendo mibaya ya watumishi, ubinafsi katika kazi rushwa, vitendo vya jinai (wizi) na matuumizi mabaya ya madaraka.

Waziri Gwajima alisema wauguzi na wakunga ni raslimali kubwa na nguvu kubwa katika sekta ya afya nchini.

“Ni watoa huduma ya afya ambao wako mstari wa mbele katika kutoa huduma wakati wote kwa kuwahudumia wgonjwa wenye uhitaji wakati wote, hufanya kazi saa 24 siku saba kwa wiki wakitoa huduma za afya kwa zaidi ya asilimia 80 ya huduma zote za afya,” alisema.

Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitenga mwaka 2020 kuwa mwaka wa wauguzi na wakunga duniani na kuadhimishwa katika nchi mbalimbali kama ya kuenzi mchango muhimu unaotolewa na wauguzi na wakunga katika kuleta mapinduzi makubwa katika huduma ya afya na kuongeza kuwa mkutano huo ni sehemu ya maadhimisho hayo japokuwa unafanyika mwaka 2021 .

“Kwa nchi yetu wauguzi na wakunga ni zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi katika sekta ya afya na wanao mchango mkubwa katika utekelezaji wa malengo ya afya hasa upatikanaji wa afya ta msingi katika jamii ambapo zaidi ya watanzania asilimia 75 wanapatikana,”alisema.

Alisema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo kupitia upya kwa miundo ya maendeleo ya watumishi katika sekta ya afya, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na dawa ili wananchi wapate huduma bora za afya.

Pia kubuni mikakati mbalimbali ili kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga na vyenye umwi chini ya miaka mitano, kuangalia upya muundo wa viongozi katika sekta ya afya ili uweze kuwa jumuishi na kada nyingine.

“Wasiopenda kukaa pamoja marufuku, tunatengeneza mkakati wa kitaifa wa kusimamia maadili tunataka mataifa mengine yajifunze kyoka kwetu,” alisema na kuongeza kuwa mara nyingi kwenye kazi chuki inasababishwa kwa sababu ya madaraja.

Rais wa Chama cha Wauguzi, Alexender Bahuhya alisema malalamiko juu ya wauguzi yapo lakini si wauguzi wote wanaolalamikiwa na kuongeza wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Ofisa Muuguzi Mkuu na Msimamizi wa huduma za uuguzi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dinnah Atinda alisema kama viongozi atahakikisha wanashirikiana ili kuwa na matokeo chanya.

Chanzo: habarileo.co.tz