Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dawa ya viluwiluwi yasambazwa nyumba kwa nyumba

Ff374ff7058ac482fcf0c5ebc653efca Dawa ya viluwiluwi yasambazwa nyumba kwa nyumba

Sat, 13 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKAKATI wa kusambaza dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu zinazozalishwa nchini kwa lengo la kutokomeza malaria, umeanza kutekelezwa kwa vitendo kutokana na kampeni ya nyumba kwa nyumba inayotekelezwa nchi nzima.

Kampeni hiyo ya kitaifa iliyoanzia mkoani Dar es Salaam ni sehemu ya matunda ya mikakati ya kuhakikisha dawa hizo zinazozalishwa na Kiwanda cha Tanzania Biotech Product (TBP) Ltd kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani zinatumika ipasavyo kutokomeza malaria.

Watoa elimu kutoka Shirika la Kumekucha iliyopewa baraka na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusambaza dawa hizo, wanapita nyumba kwa nyumba wakielimisha namna ya kupata na kutumia dawa hizo.

Meneja Mdhibiti Ubora kutoka TBPL, Samwel Mziray alisema Shirika la Kumekucha limepata baraka kutoka Tamisemi kufanya kazi ya kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu matumizi ya dawa hizo za viuadudu.

Mziray alisema dawa inayozalishwa na TBPL ina uwezo wa kukaa kwa miaka mitano na kwamba uzalishaji wake ni

wenye kuaminika baada ya nchi kuweka uwekezaji mkubwa.

Mkurugenzi wa Shirika la Kumekucha Tanzania, Jackson Cyprian alisema uratibu wa kuweka mabalozi kwa ajili ya

kutoa elimu kwa Dar es Salaam na Pwani umeshafanyika kwa asilimia 80 na baada ya kukamilisha, wataelekeza nguvu katika mikoa mingine wakianza na yenye maambukizi makubwa.

Alitaja mikoa hiyo ni Kagera, Kigoma, Mwanza, Simiyu, Mara, Shinyanga, Katavi, Tabora, Ruvuma, Dodoma, Morogoro, Lindi na Mtwara.

Alisema ili kutekeleza kampeni hiyo, kila mtaa alitafutwa mtu mzalendo atakayetoa elimu kwa wananchi kuhusu dawa hizo lengo likiwa ni kuhakikisha chanzo cha mazalia ya mbu kinaharibiwa.

Msimamizi wa Waratibu wa Watoa elimu kutoka Shirika la Kumekucha, Edwin Bagenda aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kupitia matumizi ya dawa hizo.

Alisema dawa hizo ni salama kwa afya na mazingira na zinaweza kuwekwa katika vyombo vya kuhifadhia maji kudhibiti mbu kuzaliana.

Ili kukamilisha dozi katika maeneo hatarishi ya viluwiluwi, dawa inatumika kwa miezi mitatu kulingana na maelekezo ya watoa elimu watakaofika nyumba kwa nyumba.

“Ikumbukwe kuwa mbu hutaga mayai 200 kwa mara saba ndani ya mwezi mmoja,” alisema.

Licha ya malaria, magonjwa mengine yatokanayo na mbu ni dengue, chikungunya, Homa ya Bonde la Ufa, zika, mabusha na homa ya manjano.

“Tunawajibika kutokomeza chanzo, hivyo suluhisho ni kutumia dawa za viuadudu kutokomeza chanzo cha magonjwa hayo… mbu mmoja ana uwezo wa kuangua wastani wa viluwiluwi 1,400,” alisema Bagenda.

Ushirikiano wa Shirika la Maendeleo (NDC) na Kumekucha Tanzania wa kusambaza viuadudu hivyo ulifikiwa baada ya TBP kuzalisha viuadudu hivyo bila kununuliwa kwa kiwango kikubwa licha ya umuhimu wake wa kuteketeza mbu.

Ushirikiano wa NDC na Kumekucha Tanzania unategemewa kuwezesha dawa hizo kupatikana nchi nzima. Dawa hizo zimefungashwa kwa ujazo wa mililita 30, nusu lita, lita moja, lita tano, lita 10 na 20.

TBPL ni kiwanda pekee katika Afrika kilichoanzishwa Julai 2015 kutafuta suluhisho la kupambana na malaria kwa kuua viluwiluwi badala ya kusubiri kuangamiza mbu waliokomaa. Kilianza uzalishaji mwaka 2017 kwa thamani ya uwekezaji wa takribani Sh bilioni 50.6 kwa msaada wa teknolojia kutoka Cuba.

Chanzo: www.habarileo.co.tz