Serikali kupitia Wizara ya Afya imewaasa wananchi kuacha tabia ya kutumia dawa za macho kwa lengo la kutibu ugonjwa wa ‘Red Eyes’ zisizo rasmi kwa kuwa matumizi hayo yanaweza kupelekea upofu usiotibika kama ambavyo itakuwa kwa wengi wa wagonjwa waliokwisha kupata madhara kwenye kioo cha jicho kwa kutumia vitu hivyo.
Wito huo umetokewa leo Februari 8, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo alipokua anaongea na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar Es Salaam.
“Ugonjwa wa ‘Red Eyes’ hauleti upofu lakini matumizi ya dawa zisizo rasmi na zinazonunuliwa kiholela yanaweza kupelekea upofu usiotibika kama ambavyo inaweza kuwapata baadhi ya wagonjwa waliopata vidonda kwenye kioo cha Jicho baada ya kutumia dawa hizo zisizo rasmi” Amesema Prof. Ruggajo.
Amesema, Baadhi ya vitu vinavyotumika ni pamoja na dawa zenye vichocheo vya ‘steroids’ ambazo wananchi wanakwenda kununua wenyewe kwenye maduka ya dawa, tangawizi, chai ya rangi illiyokolea majani, mafuta tete yaliyokuwa yakitumika wakati wa janga la Covid - 19, maji ya chumvi na maziwa ya mama, ambavyo vitu vyote hivyo sio salama na havijaelekezwa na wataalamu.
Aidha, Prof. Ruggajo amesema hadi sasa takwimu zinaonesha ongezeko la kuenea kwa ugonjwa huu ambapo jumla ya wagonjwa 12,332 wameonwa katika vituo vyetu vya tiba na wagonjwa hawa wameonwa katika Mikoa 23 ya Tanzania Bara.