Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar yapata ICU zinazotembea

Icu Moving.png Dar yapata ICU zinazotembea

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali za rufaa za mikoa, zilizopo mkoani Dar es Salaam, zimekabidhiwa gari tatu za kubebea wagonjwa zenye huduma zote zitolewazo katika chumba cha uangalizi maalumu kwa wagonjwa (ICU).

Hospitali zilizopata gari hizo ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Temeke na Mwananyamala.

Magari hayo yenye thamani ya Sh502 milioni yamekabidhia leo Jumanne Novemba 28, 2022 jijini hapa, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kwa wakuu wa wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi magari hayo, Chalamila amesema kwa muda mrefu madaktari wamekuwa wakilalamikia magari ya wagonjwa kutotosha na yaliyopo yalikiwa chakavu.

"Rais Samia Suluhu baada ya kusikia vilio hivyo ameamua kuleta magari haya na mengine yatakuja kwani pia amefanya hivyo kwa Wizara ya Elimu na wiki ijayo anatarajia kufanya kwa Jeshi la Polisi. "Wito wangu vifaa hivi viende kutumika vizuri ili viendelee kuwasaidia wagonjwa leo na kesho,”amesema Chalamila.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema magari hayo yamekuja wakati muafaka ambapo Serikali inaboresha barabara za jiji hilo hivyo atakapopatikana mgonjwa atakuwa na uhakika wa kufikishwa salama hospitali.

Mpogolo ameahidi kuwa wataendelea kusimamia magari hayo ukizingatia tayari wameshakarabati magari mengine ya wagonjwa saba ambayo yataongeza nguvu katika kutoa huduma.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema magari hayo sio tu mashine yenye miguu minne bali ni ICU yenye huduma zote.

Akizungumza kwa niaba ya waganga wa hospitali zilizonufaika, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, Dk Bryson Kiwelu amesema magari hayo yametokana na fedha za Uviko-19 na ni kama ICU zinazotembea kwa kuwa zina huduma zote za kitengo hicho.

Dk Ķiwelu amesema wanashukuru kwa kutatuliwa kwa changamoto hiyo na kutumia nafasi hiyo kukumbusha changamoto ya uhaba wa majengo kuw anayo ifanyiwe kazi kwa haraka ili wafanye kazi kwa ufanisi zaidi kuliko ilivyo sasa.

"Mfano kwa Amana tuliomba jengo la Amana Centre, Temeke kuna eneo la wazi waliomba pembeni yao na Mwananyamala hivyohivyo kuna eneo pembezoni mwao pale na wote tulishafikisha maombi yetu kwa mamlaka husika lakini tunaona majibu yanachukua muda kutolewa," amesema daktari huyo.

Kwa upande wao wananchi akiwemo Sheila Hussein, ameomba wagonjwa wanapohitaji huduma za magari hayo iwe rahisi kuzipata kwa kuwa kukabidhiwa hospitali ni jambo moja lakini kupata huduma zake ni jambo jingine.

Elisha Gabriel amesema gari kama hizo zinahitajika nyingi ukizingatia hospitali hizo zinahudumia watu wengi wakiwemo wa mikoa jirani na kushauri Serikalli katika bajeti zake iliangalie na hilo, badala ya kusubiria fedha kutoka kwa wahisani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live