Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar, Pwani, Moro kuanza chanjo ya corona

84017f36ed09a8b66a2cf7f66f590869.jpeg Dar, Pwani, Moro kuanza chanjo ya corona

Fri, 30 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ameiagiza mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ichukue mgawo wa chanjo ya corona ili waanze kutoa huduma hiyo.

Pia ameagiza Bohari ya Dawa (MSD) ndani ya siku 10 kuanzia sasa iwe imeshasambaza chanjo hiyo nchi nzima.

Dk Gwajima alitoa maagizo hayo jana Dar es Salaam katika kikao cha afya na lishe kwa Mkoa wa Dar es Salaam, akisema kwa kuwa chanjo hiyo ipo tayari, ameiagiza wizara itoe kwa mikoa yote ili wananchi walio na utayari waipate.

“Dar es Salaam nendeni na magari yenu mkachukue mgawo wenu upo tayari wala hamhitaji kusubiri, ili mjipange siku gani mnaanza kuwapatia watu chanjo ile mikoa ya mbali ndio watapelekewa,” alisema Dk Gwajima.

“Pwani, Dar es Salaam, Morogoro wanaweza kuja wenyewe wakachukua migao yao inafahamika. Kwa hiyo mkuu wa mkoa ninawapongeza kwa kazi nzuri mlivyojipanga songeni mbele msimamie hatua ya chanjo tukishafikia Dar es Salaam asilimia 60, hiyo siyo hatua ndogo,” alieleza Dk Gwajima.

Alisema kama nchi wamejipanga kufikia asilimia 60 ndani ya miaka mitatu, lakini ikiwezekana kabla ya hapo ni vizuri zaidi. Alisema chanjo hiyo itakapopelekwa mikoani kisha watu wakawa bado wanajishauri kuchanja, wataihamisha kuipeleka maeneo wanayoihitaji.

“Niseme katika mikoa mingine tukiona tumepeleka chanjo kule halafu watu bado wanajishauri tutaona kwamba hatujafanya kazi sahihi, tutazichukua na kupeleka wanakozihitaji hiyo niseme wazi sipo tayari kuona zinakaa pale wakati sehemu nyingine watu wanazihitaji. Tukipewa tujitokeze kuchanja ziishe ili biashara iishe tufanye mambo mengine,” alisema Waziri wa Afya.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alimshukuru waziri kwa kufika kwenye kikao hicho cha afya na lishe katika mkoa huo.

Aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa ajili ya kupata chanjo ambayo haina athari zozote.

“Nasimama kifua mbele baada ya chanjo nimelala vizuri. Nimejiuliza hivi nilipozaliwa kama mitandao ingekuwepo Mzee Makalla angeruhusu nipate chanjo ya ndui, kifaduro na polio? Niwaulize Watanzania katika chanjo zote tulizozipata, ipi iliyotengenezwa Tanzania? Tusaidiane maana chanjo zote zinatengenezwa nje ya nchi,” alisema Makalla.

Alisema Rais Samia Hassan Suluhu alisema Tanzania haiwezi kuwa kisiwa ni lazima iungane na mataifa mengine duniani katika chanjo hiyo.

Makalla aliwataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watu wa lishe katika kila halmashauri kuhakikisha wanatenga fedha za kuwawezesha maofisa lishe kufanya kazi kwa ustadi, kuwepo na mafunzo na elimu kwa wananchi.

“Mbeya na Katavi imebarikiwa kwa chakula, lakini inasomeka udumavu na utapiamlo ndio upo mwingi tukaona kuwa elimu ni muhimu sana ya watu kula mlo kamili.

“Tutaendelea kukaa na kutoa mikakati kuhusu masuala ya lishe, wakuu wa wilaya na wakurugenzi zingatieni mikataba mliyoingia,” alisema Makalla.

Chanzo: www.habarileo.co.tz