Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari aliyevuliwa cheo Arusha akataa malumbano

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha, Dk Japhet Kivuyo ambaye amevuliwa madaraka  ya kuongoza kituo cha afya cha Ngarenaro jijini Arusha baada ya kutotii wito wa wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM  kata ya Levolosi kutakiwa kurejea kazini  jioni amesema anamwachia Mungu suala hilo.

Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Dk  Maulid Madeni amesema  kuwa amemvua madaraka Dk Kivuyo na kumteua Dk David Mg’anya kushika nafasi hiyo kutokana na kutoa lugha ambazo sio za kiuongozi kwa wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM kata ya Revolosi.

Alisema Dk Kivuyo ambaye aliondoka kazini saa 9:00  jioni na kwenda shambani, baada ya kupigiwa simu na viongozi hao kutakiwa kurudi ofisini alipaswa kutoa lugha za kiuongozi ingawa ni kweli hadi mchana alikuwa kazini.

Wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM ya kata hiyo wakiongozwa na katibu mwenezi, Abubakar Hamis Nyangu walifika kituoni hapo siku ya Ijumaa Kuu majira ya saa 9:00 na kutomkuta Dk Kivuyo ofisini.

Nyangu akizungumza kwa simu alimtaka Dk Kivuyo kurejea ofisi ndani ya dakika chache. lakini hata hivyo daktari huyo  alieleza ameshatoka ofisini na asingeweza kurejea kwani kuna maofisa wengine wanaotoa huduma hasa za uzazi.

Dk Kivuyo akizungumza na Mwananchi jana amesema amepata taarifa za kuvuliwa madaraka lakini hana la kusema bali anamuachia Mungu.

“Mimi ninamuachia Mungu, mimi ni mtu mzima nakaribia miaka 60 sioni sababu ya kulumbana,” alisema.

Hata hivyo, akizungumzia tukio hilo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Dk Omar Chande amesema suala hilo bado lipo katika uchunguzi.

“Sisi kama madaktari tuna taratibu zetu kabla ya kutoa maamuzi hivyo suala hili lipo katika uchunguzi  na ukikamilika tutatoa taarifa, ” amesema.

Kituo cha afya cha Ngarenaro kimekuwa kikitoa huduma za uzazi  kwa wakazi wa jiji la Arusha hasa kwa wakazi wa maeneo ya kata za  Ngarenaro.



Chanzo: mwananchi.co.tz