Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari aeleza jinsi ya kupokea hedhi salama kwa mtoto wa kike

89383 Hedhi+pic Daktari aeleza jinsi ya kupokea hedhi salama kwa mtoto wa kike

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Balehe kwa mtoto wa kike inasifa mbalimbali hasa kupata hedhi, yaani kupata mzunguko wa mfumo wa uzazi kila mwezi.

Endapo viungo vya uzazi havitapata mbegu ya kurutubisha basi mfuko wa uzazi uliofanya maandalizi hujimenya na kutoka nje kupitia uke kwa mfumo wa damu na hii ni baada ya muda wa siku 21, 28 na kwa wachache au siku 35.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Japhet Simeo anasema mzunguko wa hedhi huathiriwa na vitu mbalimbali ikiwamo lishe, madhara ya kisaikolojia na mfumo wa maisha.

Dk Simei anasema inapotokea hivyo, husababisha mzunguko kujirudia kabla ya muda wake.

Anasema kwa kawaida binti anaweza kupata hedhi kwa siku tatu hadi tano lakini wapo wanaoweza kwenda hadi siku saba.

Pia, anasema wapo wanaopata damu ndogo na wengine nyingi kulingana na mtu.

Dk Simeo anasema binti anapoingia kwenye hedhi anapaswa kuimarisha hali yake ya usafi na lazima awe na vitu vya kumfanya kuwa safi ili kumuepusha na maambukizi kwenye via vya uzazi pamoja na kuweza kujichanganya na jamii inayomzunguka.

Dk Simeo anasema mtoto wa kike anapaswa kuipokea hedhi kwa kuihifadhi kwa kutumia taulo ya kike hasa zilizotengenezwa viwandani ambazo zimesafishwa vizuri na haziwezi kubeba wadudu wa nje.

Anasema uke wa mwanamke una bakteria rafiki ambao hushambulia bakteria wengine ambao si rafiki pindi wanapoingia.

Dk Simeo anasema endapo mwanamke atakuwa kwenye hedhi hapaswi kukaa na sodo zaidi ya saa nane kwa sababu damu inapokaa muda mrefu hugeuka na kuwa chakula cha bakteria rafiki waliomo ndani ya uke na inapobadilika inaweza kusababisha maambukizi kwenye sehemu za uzazi.

“Pia, damu hiyo inaposhambuliwa na bakteria huwa na harufu mbaya na inaweza kumnyima ujasiri wa kuchangamana na jamii .

“Inaweza kuvutia bakteria walioko nje kuingia na kushambulia sehemu za uzazi za mwanamke,”anasema Dk Simeo.

Pia, anasema endapo mwanamke au binti atakuwa hana uwezo wa kupata taulo za kisasa ni vyema akatumia kitambaa kisafi kilichotakaswa (kufuliwa na kunyooshwa)ili kuepuka madhara ya kupata bakteria ambao watashambulia via vyake vya uzazi.

“Najua kuna mazingira ambayo mtu hawezi kutumia taulo za kisasa kutokana na hali ya uchumi lakini ni vyema unapotumia taulo ya kienyeji yaani kitambaa ukahakikisha ni kisafi kimetakaswa na kikavu ili kuepuka maambukizi ndani ya uzazi,”anasema Dk Simeo.

Madhara ya kutumia nguo mbichi za ndani

Kwa kuwa baadhi ya watoto wa kike, hasa wanaotoka katika familia duni hutumia nguo mbichi za ndani kutokana na umaskini, Dk Simeo anasema mwanamke atakapotumia nguo hizo wakati wa hedhi sehemu zake za siri hushambuliwa na bakteria.

Anasema bakteria hao husababisha kupata maumivu ya tumbo, maumivu wakati wa tendo la ndoa na fangasi.

“Mwanamke anapotumia nguo mbichi au kujisitiri na doso ya kienyeji “taulo ya kike ya kienyeji” ambayo hupata michubuko, majipu na endapo anaishi maeneo yenye kemikali kama zinazotumika kwenye uchimbaji madhara yanaweza kuwa mabaya zaidi,” anasema.

Pia, anasema wanafunzi wanapokutana na changamoto ya kukosa hedhi salama hushindwa kwenda shule na ufaulu wao kuwa hafifu.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2016 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu , Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inakadiriwa kuwa msichana mmoja kati ya 10 kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara hukosa masomo pindi anapokuwa kwenye mzunguko wa hedhi.

Watoto wa kike wanasemaje?

Anna John (16) (sio majina kamili) mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Kishinda wilayani Geita anasema hupoteza masomo kwa siku tatu hadi tano kutokana na hedhi isiyo salama.

Anna anayeishi na bibi yake na wadogo zake wawili anasema awali hakuwa na chupi kabisa lakini baada ya kubalehe alifanya vibarua vya kulima na kupata Sh 3,500 iliyomuwezesha kununua nguo za ndani mbili.

“Sina hata tambara, nikiwa kwenye siku zangu naoga mara tano na nafua chupi na kuvaa ikiwa mbichi. Inapotokea nipo shule huwa naomba ruhusa kwa mwalimu wa afya ananipa ruhusa kwa siku tatu zikiisha ndio narudi shule hata walimu wameshanizoea.”

Mtoto mwingine Sikujua Juma (15) anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi Nyawilimwilwa anasema awali alipotokwa na damu alishtuka kwa kuwa alikuwa darasa la tatu na hakujua nini maana ya hedhi.

“Nilikuwa nacheza baadaye nguo zangu zikachafuka damu, sikujua nimefanya nini na hata sikumwambia mama niliogopa,kesho yake nilipoenda shule nilichafuka sana ndio wanafunzi wakamwambia mwalimu akaniita na kunifundisha jinsi ya kutumia kitambaa,”anasema Sikujua

Sikujua anasema licha ya kufundishwa namna ya kutumia vitambaa lakini ana chupi moja analazimika kuifua na kuivaa mbichi jambo lililosababisha kuwashwa na kutokwa vipele sehemu zake siri.

Neema Michael (16) anasema suala la kubalehe alilisikia kutoka kwa dada yake hivyo alipovunja ungo hakupata changamoto za kujisitiri. “Kwa kuwa hakuna chumba cha kujisitiri ninapopata hedhi nikiwa shuleni huwa narudi nyumbani na kutokana na umbali kati ya nyumbani na shule nakaa nyumbani siku tatu au tano inapoisha ndio naenda tena shule,”anasema Neema.

Walimu wazungumzia hedhi salama kwa wanafunzi

Mwalimu wa Shule ya Msingi Ihumilo Christina Raphael anasema kila baada ya wiki mbili hukaa na wanafunzi wa kike na kuwaelimisha nini maana ya balehe na namna ya kuwa wasafi wakati wote.

Anasema katika shule hiyo kipo chumba maalumu kwa ajili ya watoto wa kike ambacho hutumika kuhifadhia taulo za kike na pindi mwanafunzi anapohitaji hutoa taarifa kwake au kwa mwalimu yoyote wa kike na kupatiwa.

Anasema fedha kwa ajili ya kununulia taulo za kike hutolewa na mwalimu mkuu lakini pia wanao mradi wa kujitegemea wanaofanya biashara ya kuuza mandazi kwenye viwanja vya shule, fedha zikikusanywa hununulia taulo za kike kwa ajili ya wanafunzi.

Mwalimu Josephine Joseph wa Shule ya Msingi Mkapa anasema alipata elimu ya masuala ya hedhi salama kutoka shirika lisilo la kiserikali la Plan International na sasa anatumia elimu hiyo kuwafundisha wanafunzi namna ya kujisafisha na kumudu hedhi.

Kwa nyakati tofauti walimu wanasema hedhi kwenye jamii bado ni suala la usiri, watoto hawapo tayari kuwaeleza wazazi pindi wanapopata hedhi hivyo kuwa kwenye mazingira yasiyo rafiki kiafya.

“Mtoto hana nguo za ndani lakini hathubutu kumueleza baba na wakati baba ndio anamiliki kipato cha familia mwisho wa siku anavaa chupi ambayo haijakauka au anatumia tambara ambalo kiafya si nzuri mwisho wa siku anapata fangasi na hata akiwashwa hana uthubutu wa kusema na haendi pia hospitali,” anasema.

Ofisa Elimu Msingi wa halmashauri hiyo, Said Matiku anasema ana shule 196 za msingi na ili kuhakikisha mtoto wa kike anahudhuria vipindi vyote darasani tayari amewaelekeza wakuu wa shule kuwa na chumba maalumu kwa ajili ya wanafunzi kujisitiri.

Nini Kifanyike?

Mratibu wa Afya kwa Umma Mkoa wa Geita, Paskazia Madulu anasema ili kumuwezesha mtoto wa kike kuwa na hedhi salama ni wajibu wa mzazi au jamaa ya karibu kumuandaa binti pindi dalili za balehe zinapoanza.

Anasema wazazi hawapaswi kukwepa majukumu na ni wajibu wao kuhakikisha watoto wa kike wana nguo nne hadi tano za ndani ili kumuepusha kuvaa nguo mbichi ambazo zinamadhara kiafya.

Chanzo: mwananchi.co.tz