Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari aeleza hatari kuchanganya majani kupiga nyungu

Fac233a7f0c5a5940543fda332f3a930.jpeg Daktari aeleza hatari kuchanganya majani kupiga nyungu

Fri, 5 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATAALAMU wa afya na dawa asili wameutaka umma kuwa makini wanapojifukiza na kuepuka kuchanganya vitu vingi wakati wa kutengeneza ‘nyungu’ kwa kuwa baadhi ya majani yanayochanganywa hayana faida yoyote na mengine ni sumu.

Akizungumza na HabariLEO jijini Dar es Salaam kuhusu madhara ya uchanganyaji vitu vingi wakati wa kuchemsha nyungu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Dawa Asili Muhimbili ( MUHAS),Dk Joseph Otieno, alisema upigaji nyungu unahitaji mchanganyiko wa vitu visivyozidi vitatu, na kwamba hata kimoja kinatosha.

“Mmea mmoja unatosha kwa sababu ndani yake kuna mchanganyiko wa vitu vingi yaani kwenye viambata, lakini ukiweka aina tatu za majini nayo sio mbaya ni nzuri pia ila sio zaidi ya hivyo, ukizidisha mimea mingine ni sumu na nyingine hazina chochote cha kusaidia”alisema Dk Otieno.

Alisema aina za majani ya asili yanayofaa kwa kujifukiza ni mchaichai, Kivumbasi (kashwagala) na mkaratusi, ambayo yamethibitika na kufanyiwa utafiti na yana machapisho ya ubora wake na yana mafuta tete.

Alisema majani au mti wa muarobaini una mafuta tete, lakini usalama wake haufahamiki duniani, na kwamba wataalamu wa afya duniani kote hawaridhii mti huo kutumika kama tiba asili kwa sababu una aina fulani ya alikaloidi yenye madhara kwenye miili ya binadamu.

“Wengine wanasema changanya majani ya mwembe, wengine ya mpera, ya mstafeli, muarobaini na mengine mengi, unakuta badala ya mtu kusaidika anazidi kuumia na wakati mwingine anapata madhara kwa sababu tu ya kuchanganya vitu vingi na wakati mwingine mchanganyiko wa majani mengi huua nguvu ya tiba, vilevile ukazidisha nguvu ikawa kali zaidi huleta madhara” alisema Dk Otieno.

Alisema ili kijufukiza mtu anaweza kutumia aina moja tu ya mmea kati ya hizo tajwa na ikafanya kazi wa usahihi na kushauri wakati wa kuandaa nyungu, maji yachemshe peke yake hadi yatokote kisha mchanganyiko wa majani uwekwa na kuepuliwa tayari kwa kujifukiza.

“Ukishaepua, koroga ili ile mvuke wa kwanza wa moto upungue alafu chukua blanketi au shuka zito jifunike na anza kujifukiza kwa dakika tano au 10 kulingana na afya yako’’alisema Otieno.

Akizungmzia kitunguu saumu na limau, Dk Otieno alisema watu wengi wanakosea namna ya kutumia na matokeo yake wanaua nguvu yote ya dawa na kula makapi, wakidhani wamekunywa dawa.

Alisema, kitunguu saumu hutumika kusaidia damu isigande kwenye mishipa ya damu wakati mwili ukipambana kwa mtu mwenye mafua makali au aliyepata maambukizi ya virusi vya corona, na vinatakiwa kupondwa pondwa kisha kuchanganywa na maji baridi na sio ya moto ili kuepuka kuua nguvu ya dawa.

Kadhalika, limau halitakiwi kuchemshwa, bali linatakiwa kuwekwa kwenye maji ya baridi ili vitamini C iliyopo iendelee kubaki.

Chanzo: habarileo.co.tz