Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Daktari: Mwanafunzi anayedaiwa kubakwa alikuwa mjamzito

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Dk Omary Mahizi, shahidi wa sita katika kesi ya kubaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la saba inayomkabili, Jamili Mohamedy (21), amedai vipimo alivyofanya vilionyesha ana ujauzito wa wiki 35.

Shahidi huyo ambaye ni daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Amana, alieleza hayo jana wakati akitoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala namna alivyompima mwanafunzi huyo aliyefikishwa hospitalini hapo na mzazi wake.

Dk Mahizi anayefanya kazi ya uratibu wa huduma za afya alieleza hayo mbele ya hakimu mkazi, Catherine Kiyoja.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Jacqueline Werema alidai Januari 7 mwaka jana alimpokea mzazi wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka 15, wakiwa na fomu ya polisi (PF3).

Dk Mahizi alidai mzazi wa mwanafunzi huyo alifika hospitalini hapo akihitaji udhibitisho kama mtoto wake ni mjanzito.

“Katika uchunguzi wa awali mtoto huyo alionekana ana tumbo kubwa, kipimo cha kwanza tulipima haja ndogo na kuthibitisha ujauzito,” alidai.

Aliendelea kuwa walifanya kipimo kingine (ultra sound) na kubaini ujauzito huo ni wa wiki 35.

Alibainisha kuwa awali mtoto huyo alidai tayari alishaanza kwenda kliniki na mimba ilikuwa na miezi minane. “Baada ya hapo nilijaza taarifa kwenye fomu ya PF3 kwa kuweka namba ya fomu na saini yangu,” alieleza Dk Mahizi.

Mshtakiwa ambaye ni mkazi wa Gongo la Mboto anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kumpa mwanafunzi ujauzito na kubaka.

Katika shtaka la kwanza la kumpa ujauzito mwanafunzi huyo, ilielezwa kuwa alitenda kosa hilo mwaka 2017 eneo la Gongo la Mboto wilayani Ilala.

Shitaka la pili, inadaiwa siku hiyo alimbaka mwanafunzi huyo wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 31.

Chanzo: mwananchi.co.tz