Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DIT sasa wabuni mashine kusaidia wagonjwa kupumua

Ced63c7fa410078ace99600f0813422d.png DIT sasa wabuni mashine kusaidia wagonjwa kupumua

Thu, 23 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

INGAWA ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid- 19) umepungua sana nchini Tanzania, lakini unaendelea kusumbua mataifa mengi duniani wakiwemo majirani zetu wa Kenya.

Ni kwa mantiki hiyo, hatuwezi kusema kwamba ugonjwa huu umeisha au hautarudi tena bali ni vyema Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari mbalimbali dhidi ya corona. Inaelezwa kwamba dalili kuu za corona ni pamoja na homa kali, uchovu na kikohozi kikavu na zinatokea taratibu.

Lakini dalili kubwa na yenye hatari ni mtu kukosa pumzi na wengi inaelezwa kwamba hufa kutokana na tatizo hilo la kupumua. Zipo taarifa kwamba katika baadhi ya nchi, uchache wa mashine za kusaidia wagonjwa wa corona kupumua umechangia sana kusababisha vifo ambavyo vingeweza kuokolewa.

Ni katika muktadha huo, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), iliamua kuingia katika eneo hilo katika kusaidia nchi uwepo wa mashine za kusaidia wananchi kupumua. DIT kama ambavyo inajipambanua kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika kutatua changamoto za jamii imebuni na kutengeneza mashine ya kuwasaidia wagonjwa wa corona wenye shida ya kupumua.

Mashine hii ina uwezo wa kumsaidia mgonjwa mwenye matatizo ya kupumua kabisa au ambaye uwezo wake wa kupumua umepungua sana na hivyo kumsaidia kufidia kiasi ambacho kimepungua ili aweze kupumua kawaida.

Mashine hii kwa kuwa inatengenezwa hapa nchini huku sehemu kubwa ya vifaa ikiwa ya hapahapa nchini, gharama yake itakuwa nafuu na hata ukarabati wake utakuwa nafuu pia. Tayari mashine hizi kutoka DIT zitaanza kusambazwa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini.

Akizungumzia mashine hiyo, Mwalimu wa DIT, Idara ya Kompyuta, Haji Fimbombaya ambaye pia ni mmoja kati ya timu iliyoibuni anasema mashine hiyo ni msaada mkubwa kwa wagonjwa wenye tatizo la upumuaji.

“Mtu ambaye amepungukiwa uwezo wake wa kupumua mfano kwa asilimia kadhaa, mashine itatoa kiwango ambacho kimepungua ili aweze kupumua kwa uwezo unaotakiwa,” anasema Fimbombaya.

Mwalimu huyo pamoja na wanafunzi wake wametengeneza mashine hiyo kwa muda wa miezi miwili, wanafunzi hao ni, Innocent Douglas na Aiche Rogers ambao wote wanachukua diploma mwaka wa kwanza kozi ya Uhandisi Dawa na Bayolojia (Biomedical Engineering).

“Lilipotokea janga la corona na serikali kutangaza kwamba mashine tulizonazo nchini ni chache, na kisha tukafuatilia duniani na kugundua kwamba mashine hizi zitahitajika sana, mkuu wa DIT aliunda timu kuangalia ni namna gani tunaweza kusaidia,” anasema.

Anasema baada ya kubaini kuwa uwezo wanao wakaamua kubuni mashine hiyo ya kumsaidia mgonjwa kupumua endapo janga hili likiwa kubwa nchini iweze kusaidia. Anasema, ingawa mwanzoni walilenga mashine hiyo itumike kwa waathirika wa corona pekee, lakini baadaye wameona kuwa inaweza kuwasaidia hata wagonjwa wengine wenye tatizo la upumuaji.

“Kwa utafiti wetu tumebaini kwamba mashine hizi bado zinahitajika sana, kuna hospitali na vituo vya afya vingi serikali imejenga nchi nzima lakini bado hakuna vifaa kama hivi, hivyo pamoja na kwamba corona sio tishio tena nchini kwa sasa lakini tunaendelea na utafiti wetu, bado mahitaji ni makubwa hospitalini katika wilaya mbalimbali,” anasema Fimbombaya.

Fimbombaya anasema mashine waliotengeneza haijaanza kutumika hospitalini na kwamba wataipeleka katika mamlaka husika ili kujua kama kuna upungufu au maboresho mengine yanahitajika ili iweze kuboreshwa na kisha kuanza kuunda mashine nyingi zaidi.

“Lakini hatuna wasiwasi na uwezo wa mashine kwani viwango vilivyotumika katika utengenezaji wake ni vya kimataifa,” anasema na kuongeza kwamba asilimia 80 imetengenezwa kwa vifaa vinavyopatikana hapa nchini, kupitia kitu anachoita design studio iliyopo hapa DIT.

Anasema kutokana na hofu kwamba mahitaji yangeweza kuwa makubwa, DIT pia imetengeneza vitanda vya wagonjwa ikiwa vingehitajika wakati huo viweze kupatikana kwa urahisi hapa nchini.

“Tanzania tuna uwezo wa kutengeneza vitu vingi hapa nchini, na uzuri ni kwamba tukitengeneza nchini hata ukarabati wake ni rahisi,” anasema Fimbombaya.

UTENDAJI WA MASHINE

Mashine hiyo inasoma mapigo ya moyo ya mgonjwa ili kuona yanafanya kazi kwa asilimia ngapi na hivyo kuifanya itoe hewa kwa kiasi kilichopungua. Fimbombaya anasema hatua hiyo inamfanya mgonjwa aendelee kupata nafuu na inaweza kupunguza au kuongeza kiwango cha hewa kinachohitajika kulingana na mahitaji ya mgonjwa. Mashine hiyo ina ‘screen’ ambayo inaonesha baadhi ya taarifa za mgonjwa ikiwa ni pamoja na mapigo ya moyo.

Pia kuna kifaa ambacho kinawekewa maji ya kawaida yaliyo safi yasiyowekwa kemikali. “Hewa inayokuja kwa mgonjwa inapaswa kuwa na unyevu hivyo maji hayo yanasaidia kutoa unyevu huo,” anafafanua Fimbombaya.

Mashine hiyo pia ina uwezo wa kutoa hewa ya oksijeni endapo mgonjwa atahitaji huduma ya kuwekewa hewa hiyo. Fimbombaya anafafanua kwamba kimsingi mashine hiyo inachukua hewa inapeleka kwa mgonjwa, na inayotoka kwa mgonjwa inarudi kwenye mashine ili kusafishwa na kurudi tena kwenye hewa ya kawaida.

Anasema mashine pia inatoa ishara kwa daktari kwa kutoa mlio endapo mgonjwa amepata uwezo wa kupumua mwenyewe kwa asilimia 100 au endapo uwezo umeshuka sana.

Mashine hiyo inayoweza kutumika kwa mtu mzima au mtoto inategemea namna itakavyosetiwa na mtumiaji ingawa inashauriwa mtoto chini ya miaka minane asitumie mashine ya aina hiyo (ventilator).

Kwa upande wake, mhadhiri umeme na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Viwanda, Dk John Msumba anasema design studio iliyopo DIT inatoa nafasi kwa walimu, wanafunzi pamoja na watu wengine kufanya shughuli za ubunifu katika kutatua changamoto zilizoko katika jamii.

“Sisi kama DIT dira yetu tunatamka kuwa taasisi inayoongoza katika kutatua matatizo ya jamii hivyo ni lazima wanafunzi na walimu waangalie jamii inahitaji nini, kama ambavyo unaona walivyofanya katika tatizo la Covid 19,” anasema Dk Msumba.

Anasema mwanafunzi anaweza kuja na wazo katika studio hiyo ambayo ina wataalamu wa taasisi pamoja na vifaa nao watamsaidia kulifanya wazo kuwa kitu kinachoonekana.

Aidha, Dk Msumba anasema vitu vingi vimekwishafanyika katika studio hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaohusika na jambo husika kama ambavyo ilifanyika wakati wa matengenezo ya mashine hiyo DIT ilishirikiana na sekta ya afya.

Anasema wanafunzi walioshiriki kutengeneza mashine hiyo ni wanafunzi wa diploma hivyo ni wazi kwamba wakifika katika ngazi ya shahada watafanya mambo makubwa zaidi. DIT ni taasisi kongwe nchini inayoongoza katika kutoa mafunzo ya Uhandisi na Teknolojia kwa zaidi ya miaka 60 hapa nchini.

Mbali na kufanya tafiti mbalimbali na kutumia teknolojia kubuni vitu mbalimbali imekuwa pia na jukumu la kuelimisha umma kupitia majukwaa mbalimbali kuhusu teknolojia sahihi zinazoweza kuleta tija.

Chanzo: habarileo.co.tz