Dar es Salaam. Wakati maambukizi ya virusi vya corona yakiendelea kutikisa dunia kutokana na watu zaidi kuugua na kupoteza maisha, mawaziri wa sekta ya afya katika nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) wanakutana leo Jumatatu Machi 9, 2020 jijini Dar es Salaam kujadili ugonjwa huo.
Akizungumza na Mwananchi leo mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, Zamaradi Kawawa amesema watalaam wa sekta hiyo watakutana kabla ya mawaziri. Mkutano huo unafanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
“Mkutano ni wa siku moja utakaokuwa na ajenda tatu ambazo ni uchambuzi wa kimazingira wa virusi vya corona kupitia taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kupokea taarifa za awali katika maandalizi ya nchi wanachama pamoja na mapendekezo ya ushiriki wa Sadc,” amesema Zamaradi.
Jumamosi Februari 15, 2020 Wizara ya Afya ya Misri, ilithibitisha kutokea kwa mgonjwa wa kwanza wa corona, kuwa nchi ya kwanza Afrika kubainika kuwa na ugonjwa huo.
Baada ya kikao hicho cha mawaziri, Zamaradi amesema watakuwa na mkutano na waandishi wa habari.
Endelea kufuatilia mwananchi kwa taarifa zaidi.